Maduka, vibanda vya biashara vyachelewa kufunguliwa Dar

Muktasari:

Leo Jumanne, Agosti 23, 2022 ni siku ya Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Katika hali isiyotarajiwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamejikuta wakihangaika kupata mahitaji kwa kipindi cha asubuh ya leo Jumanne Agosti 23, 2022 kutokana na maduka mengi na sehmu za biashara kutofunguliwa kwa wakati.

Hali hiyo imeshuhudiwa maeneo ya Mwenge na Ubungo ambapo kwa kawaida maeneo haya pilikapilika za biashara huanza toka asubuhi ya saa 2 kwa lakini leo mpaka saa 4 maduka mengi yalikuwa yamefungwa kutokana na wamiliki kutulia nyumbani wakisubiri kuhesabiwa.

Hiyo ni kutokana na leo Jumanne Agosti 23, 2022 watu kushiriki Sensa ya Watu na Makazi.

Martha Tarimo, mmiliki wa duka la rasta maeneo ya Mwenge, amesema amejikuta yupo pekeyake katika eneo la biashara hali inayomtia wasiwasi endapo atafungua duka anaweza kukamatwa hivyo ameamua atulie kwaza mpaka saa 5 kama hali itakuwa hivyo basi atafunga maana hili ni tukio la kitaifa

“Mwenge ni maarufu kwa shughuli za ususi wa nywele za kimasai hivyo mara nyingi siku za mapumziko kama leo alfajiri wanawake huanza pilikapilika za kusukana na hapa dukani kwangu ndio sehemu ambayo huwa nawahi kufungua kwani naishi maeneo haya haya ya mwenge,” amesema Martha

Mmoja wa wateja wa kusuka ambaye ameomba hifadhi ya jina lake amesema yeye alikubaliana na msusi kukutana saa 1 asubuhi lakini, “tunashindwa kuanza kusuka kutokana na sehemu tunaponunua rasta kufungwa.”

Hali kama hiyo imeshuhudiwa katika maeneo mbalimbali jijini humo kwa wananchi kutumia nyumbani ili kushiriki sensa hiyo na ni siku ambayo imetangazwa kuwa ya mapumziko.