Maelfu hawajaripoti kidato cha kwanza
Dar/mikoani. Siku 16 tangu shule za sekondari zifunguliwe, mwitikio wa wanafunzi wa kidato cha kwanza walioripoti na kuanza masomo umekuwa wa kusuasua katika mikoa mingi nchini
Ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi katika mikoa mbalimbali nchini, umeshuhudia mwitikio mdogo ukilinganisha na idadi ya wanafunzi waliofaulu na kupangiwa shule katika mikoa hiyo.
Januari sita, shule hizo zilifunguliwa ambapo hadi jana Mwananchi lilizungumza na viongozi wa mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Mara na kubaini kuna tatizo. Hata hivyo, inawezekana baadhi ya wanafunzi walioshindwa kuripoti watakuwa wamejiunga na shule binafsi.
Oktoba 15 mwaka jana, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilitangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu msingi mwaka 2019 ambapo asilimia 81.50 ya watahiniwa 933,369 walifaulu mtihani huo, huku watahiniwa 909 wakifutiwa matokeo kwa sababu ya udanganyifu.
Ni asilimia 55 tu walioripoti
Kaimu Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahaba alisema hadi Januari 17 ni asilimia 55 pekee ya wanafunzi waliokuwa wamefika shuleni.
“Ukifuatilia mahudhurio ni mazuri kitaifa kwa sababu kuripoti wanafunzi wa kidato cha kwanza kunachukua siku 90, tumeanza Januari 6 na mpaka leo ni kama wiki mbili ambapo asimilia 55 wamefika shule kwa hiyo ni mahudhurio mazuri,” alisema.
Wakati Dk Mtahaba akieleza hayo, mkoani Ruvuma ni wanafunzi 6,636 pekee walioripoti shuleni kati ya 28,019 sawa na asilimia 23.68. Kati yao walioripoti wavulana ni 3,110 na wasichana 3,526.
Ofisa elimu mkoa huo, Ephraim Simbeye alisema wanafunzi wanaendelea kuripoti kidogo kidogo ambapo idadi inaendelea kuongezeka.
Simbeye alisema tayari baadhi ya viongozi wa elimu wameanza kufanya ufuatiliaji katika wilaya zote, ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanajiunga na masomo kwa muda mwafaka .
“Tumejipanga kuhakikisha wanafunzi wote ambao wamechaguliwa kuendelea na masomo wanapata nafasi. Tumeshajipanga kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa ili kuwasaidia watoto wote wasome, hivyo wazazi tunaomba wawalete watoto shule,” alisema Simbeye.
Nafuu mkoani Mara
Wakati Mkoa wa Ruvuma ukisuasua, hali ni afadhali mkoani Mara kwani karibu asilimia 80 ya wanafunzi 35,500 waliochaguliwa wameripoti.
Ofisa elimu wa Mkoa huo, Emmnauel Kisongo alisema awali wanafunzi hao walikuwa wakiripoti kwa kusuasua, lakini baada ya Serikali kuwatishia wazazi kuwapeleka mahakamani mwitikio umekuwa mkubwa.
“Hivi ninavyoongea na wewe (juzi) nipo Tarime huku vijijini na ziara yangu ni kuangalia kama wanafunzi wameripoti kama inavyotakiwa na hadi sasa ni takriban asilimia 80 wameripoti,” alisema Kisongo
Hata hivyo, aliomba kupewa muda kidogo hadi (jana) jioni ili aweze kutoa taarifa na takwimu kamili kuhusu hali halisi ambapo alisema kuwa hadi sasa amekwisha tembelea sekondari 30 katika wilaya nne kati ya sita za mkoa huo.
Wengi bado Lindi, Mtwara
Mkoani Lindi hali si nzuri kati ya wanafunzi 13,851 ni wanafunzi 6,233 pekee walioripoti.
Ofisa elimu wa mkoa wa Lindi, Vicent Kayombo alitoa mfano wa Wilaya ya Ruangwa ambayo kati ya wanafunzi 2,000 waliochaguliwa, walioripoti ni 511. Wilaya nyingine ni Nachingwea ambayo wanafunzi waliochaguliwa ni 3,281 lakini waliofika shule ni 1,618.
Alisema Wilaya Lindi Manispaa kuna wafunzi 1315 waliochaguliwa lakini ni wanafunzi 761 walioripoti, Lindi Vijijini wanafunzi waliochaguliwa ni 2,896 na walioripoti shuleni hadi jana ni 1434 huku 1,462 hawajulikani walipo.
Kayombo alisema wilaya Liwale wanafunzi 1,254 wamechaguliwa na walioripoti ni 560; Wilaya Kilwa kati ya wanafunzi waliochaguliwa 3,105 ni 1,349 pekee ndiyo wako shuleni na 1,756 bado hawajaripoti.
Kayombo amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka wanafunzi hao shuleni kabla ya Februari 9 na kwamba baada ya hapo Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa wazazi watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao shule.
Katika Mkoa wa Mtwara, wanafunzi 5,672 kati ya wanafunzi 22,810 wameripoti huku 17,138 wakiwa hawajulikani walipo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya elimu mkoa wa Mtwara, wanafunzi waliopangwa kuanza kidato cha kwanza katika shule mbalimbali wasichana walikuwa 12,066 na wavulana 10,744 lakini walioripoti hadi kufikia Januari 17 ni 5,672 ambapo wasichana ni 2,870 na wavulana 2,802.
Idadi ya halmashauri na walioripoti ni kama inavyoonekana katika mabano, Halmashauri ya wilaya Masasi (549) Masasi mji (400), halmashauri ya wilaya ya Mtwara (333) Manispaa ya Mtwara Mikindani (1,823),Halmashauri ya mji Nanyamba (268).
Halmashauri nyingine ni Nanyumbu (580) Halmashauri ya wilaya ya Newala (437) Newala mji (630) na Tandahimba (652)
Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali alisema bado wanaendelea kuwahamasisha wazazi ili watoto wao waripoti shuleni na kwamba wanaamini wataripoti.
Kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Newala, ofisa elimu taaluma sekondari, Mussa Mussoma alisema kutokana na baadhi ya wanafunzi kutoripoti wameweka mkakati wa kushirikiana na uongozi wa ngazi mbalimbali kupita nyumba kwa nyumba na hadi kufika Jumatatu iliyopita idadi ya wanaoripoti imeanza kuongezeka.
Hali si nzuri Geita
Mkoani Geita, kaimu ofisa elimu wa mkoa huo, Elysalver Nkanga alisema kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita ni wanafunzi 7,199 tu wa kidato cha kwanza walioripoti shuleni kati ya 31,881 waliochaguliwa.
Alisema Wilaya ya Nyang’hwale imepokea wanafunzi 136 tu sawa na asilimia sita ya wanafunzi 2,272 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza.
Alisema katika halmashauri ya wilaya ya Geita wanafunzi walioripoti ni 1,686 sawa na asilimia 19 ya wanafunzi 8,870 waliochaguliwa huku Wilaya ya Chato ni wanafunzi 2,168 sawa na asilimia 29 ya wanafunzi 7,453.
Wilaya ya Bukombe wanafunzi 1,146 wameripoti sawa na asilimia 24 ya wanafunzi 4,823. Wilaya ya Mbogwe imepokea wanafunzi 745 ambao ni asilimia 21 ya wanafunzi 3,487 waliochaguliwa na halmashauri ya Geita mji imepokea wanafunzi 1,348 sawa na asilimia 27 ya wanafunzi 4,976.
Kwa upande wake, Katibu tawala mkoa Arusha, Richard Kwitega alisema wanafunzi 29,770 waliofaulu mitihani wamejiunga na sekondari.
“Bado tunakusanya takwimu kwani kuna ambao tumewapangia shule za Serikali wameenda binafsi ila kwa ujumla wangi wapo shule,” alisema
Ofisa elimu mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu alisema hadi kufikia Januari 17, wanafunzi walioripoti shuleni ni 45,752 sawa na asilimia 65 ya wanafunzi 69,907 waliotarajiwa.
“Katika asilimia 35 iliyobakia, kuna wanafunzi 1400 wamehama Dar es Salaam kwenda kuishi mikoa mingine, halafu kuna wanafunzi 168 tumewapeleka shule za bweni nje ya mkoa wa Dar es Salaam, lakini ukomo wa kuripoti shule ni Machi kwa hiyo tunahimiza sana wazazi wapeleke watoto shule,” alisema Lissu.
Hali ilivyo Dodoma, Mbeya
Jijini Dodoma wanafunzi 33,803 waliofaulu mtihani huo wote walipangiwa shule na hakuna aliyekosa nafasi na wamekuwa wakiripoti katika shule zao ikiwamo ya Viwandani na Dodoma.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Viwandani, Kaizirege Tehingisa amesema kuwa shule hiyo ilipangiwa wanafunzi 402 lakini walioripoti shuleni hapo mpaka jana walikuwa wanafunzi 220.
“Wanafunzi wengi niliopangiwa katika shule yangu ni kutoka shule binafsi. Kwa mfano, wanafunzi kutoka shule ya Martin Luther ni 154 lakini walioripoti mpaka leo ni 40 tu na wengine zaidi ya 50 wameombewa uhamisho kwa hiyo hawawezi kuja kusoma hapa,” alisema Tehingisa.
Hata hivyo, alisema nafasi zilizoachwa na wanafunzi wanaohamia shule nyingine zinatoa nafasi kwa wanafunzi wengine wanaohamia katika shule hiyo kwa sababu uhamisho hufanywa kwenye ngazi ya wilaya na mkoa kwa sababu wakuu wa shule hawana mamlaka ya kutoa uhamisho.
Mkoani Mbeya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busokelo, Eston Ngilangwa alisema halmashauri hiyo ilitarajia wanafunzi 2,204 lakini mpaka Jumatatu iliyopita wanafunzi 508 walikuwa bado hawajaripoti. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi alisema kati ya wanafunzi 4,800 waliotakiwa kuripoti shuleni wanafunzi 3,120 sawa na asilimia 65 ndiyo walioripoti
Imeandikwa na Beldina Nyakeke (Mara), Haika Kimaro (Mtwara), Joyce Joliga (Ruvuma), Rachel Chibwete (Dodoma), Yonathan Kossam (Mbeya), Mwanja ibadi (Lindi), Rehema Matowo (Geita), Mussa Juma (Arusha), Joseph Lyimo (Manyara) na Kelvin Matandiko (Dar).