Maelfu wamuaga Celine Kombani
Mama Maria Nyerere akitoa heshima ya mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani kwenye Uwanja wa Karimjee, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame
Muktasari:
Atazikwa leo nyumbani kwao mkoani Morogoro
Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal jana aliongoza mamia ya waombolezaji waliofurika kwenye viwanja vya Karimjee kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
Kombani ambaye alikuwa mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki alifariki dunia Alhamisi iliyopita katika Hospitali ya Andhraprasth Appollo ya mjini Delhi, India alikokuwa amelazwa akitibiwa saratani ya kongosho.
Mwili wa Kombani uliwasili nchini Jumamosi iliyopita na baada ya kuagwa jana, ulisafirishwa kwenda Morogoro ambako utazikwa leo.
Viongozi waliofika kuuaga mwili huo ni pamoja na mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma, mke wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, mawaziri na viongozi wengine wa Serikali.
Chama cha Mapinduzi (CCM), kiliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula, Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Zakia Meghji.
Kiongozi wa chama cha upinzani aliyefika kuuaga mwili huo ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi.
Ilivyokuwa Karimjee
Jeneza jeupe lililofunikwa kwa bendera ya Taifa lililokuwa na mwili wa Kombani liliwasili uwanjani hapo saa tano asubuhi likiwa katika gari aina ya Mercedes Benz yenye rangi nyeusi.
Wakati gari hilo likiwasili kwenye lango la viwanja hivyo lilipokewa na mawaziri wakiongozwa na Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta ambao walilisindikiza hadi sehemu maalumu iliyoandaliwa.
Akitoa salamu za Bunge, aliyekuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema Kombani aliugua kwa mara ya kwanza akiwa kwenye mkutano wa kujadili muundo mpya wa utumishi wa Bunge kilichofanyika katika Hoteli ya Bahari Beach Agosti 16.
“Alitupa ushauri wake kwenye kikao kile baadaye alitoka nje na nikaletewa taarifa kwamba Kombani anajisikia vibaya na anataka apelekwe kwa daktari wake,” alisema Makinda.
Alisema alilazwa katika Hospitali ya TMJ na baadaye alihamishiwa India kwa matibabu zaidi.
Makinda alisema kilichowavutia kutaka ushauri wake ni kutokana na waziri huyo kufanya mageuzi kwenye sekta ya utumishi wa umma hasa katika udhibiti wa mishahara hewa tatizo ambalo lilidumu kwa muda mrefu. “Tumepoteza mwanamke mchapakazi, mnyenyekevu na mtu wa watu,” alisema Makinda.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema chama hicho kimepoteza mwanachama mpambanaji aliyekuwa akigombea na kulitetea Jimbo la Ulanga Mashariki.
“Alikuwa mtu mwenye uwezo, hakusubiri kuteuliwa kupitia Viti Maalumu, alikwenda kugombea na kushinda mara kadhaa kwenye jimbo lake,” alisema Kinana.