Mafundisho ya kutambua ukatili kuwasaidia watoto
Muktasari:
- Kijana mmoja mwenye umri wa miaka (37) mkazi katika Kijiji cha Senjele, Kata ya Nanyala wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe (jina limehifadhiwa) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa akituhumiwa kuwabaka watoto wadogo watatu wenye umri chini ya miaka 8.
Songwe. Kijana mmoja mwenye umri wa miaka (37) mkazi katika Kijiji cha Senjele, Kata ya Nanyala wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe (jina limehifadhiwa) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa akituhumiwa kuwabaka watoto wadogo watatu wenye umri chini ya miaka 8.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, ACP Alex Mukama amesema taarifa ya tukio hilo ilitolewa Septemba 27 mwaka huu ambapo hatua za kiuchunguzi zilichukuliwa mara moja ikiwa ni pamoja na kumpeleka kituo cha afya ambako ripoti ilionesha watoto hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo vya kikatili mara kwa mara.
Ametaja umri wa watoto waliofanyiwa ukatili huo kuwa mmoja ana umri wa miaka 5, mwingine miaka 6 na watatu ana umri wa miaka saba (7) watoto hao wote ni wanafunzi katika Shule ya Msingi Senjele.
Mmoja wa wazazi wa watoto hao Ezekiel Nerbat amesema alipogiwa simu na mzazi mwenzake (mke wake) majira ya saa kumi jioni akijulishwa kuhusu tukio hilo na kuwa mtoto huyo alifanyiwa uchunguzi wa awali na dada zake (shangazi wa mtoto) ambao walithibitisha kuhusu tukio hilo.
Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Senjele, Maiko Katekile amesema Septemba 27 mwaka huu muda wa saa nne asubuhi alipokea watoto watatu wakiwa na walimu ili wapimwe baada ya kuhisi kuwa wanajihusisha na masuala ya mapenzi ambapo aliwashauri waende kituo cha Polisi ili wapate fomu namba 3 PF 3 waende kuchunguzwa katika kituo cha afya.
Akizungumzia tukio hilo Afisa Elimu kata, hiyo Ayub Chimela amesema kujulikana kwa kijana huyo kufanya ukatili huo ni pale mwalimu wa nidhamu na malezi alipokuwa akiwafundisha namna ya kutambua vitendo vya ukatali ndipo mmoja wa wanafunzi hao alimfuata mwalimu wake wa darasa kimweleza jinsi ambavyo amekuwa akitendewa na jirani yao huyo.
"Mafundisho hayo ndiyo yaliyoamsha mmoja wa watoto hao kutoa siri ya jinsi ambavyo amekuwa akitendewa kwa kuingizwa kitu sehemu zake za Siri na kuwataka wenzake wawili," amesema Chimela.
Baada ya kuelezea hayo Mwalimu aliwaeleza wenzake na hatua zikachukuliwa na kisha kukamatwa mhusika haraka na kumfikisha kituo cha Polisi.