Mafuta yazua kilio kila kona nchini

Friday August 05 2022
mafuta pic
By Waandishi Wetu

Mikoani. Wakati wananchi wakiugulia maumivu ya kupanda kwa gharama za vyakula, bei mpya za mafuta zilizoanza kutumika jana nchi nzima zinachochea zaidi ugumu wa maisha katika shughuli zao za kila siku.

Vilio hivyo vya kila kona, vinatokana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za ukomo wa mafuta zikionyesha Jiji la Dar es Salaam lita moja ya petroli ni Sh3,410 na Sh3,322 kwa dizeli, huku mafuta ya taa yakifika Sh3,765.

Bei hizo mpya zilizoanza kutumika juzi nchi nzima, kwa Dar es Salaam zimepanda tena na kuivuka ile ya mwezi uliopita ambapo petroli imepanda kwa Sh190 kwa kila lita na Sh179 kwa kila lita ya dizeli, huku mafuta ya taa yakipanda kwa Sh323 kwa kila lita.

Aidha, bei hizo ni baada ya kuwekwa kwa ruzuku ya Serikali ya Sh100 bilioni inayoitoa kila mwezi. Hivyo, endapo ruzuku isingewekwa lita moja ya petroli ingekuwa Sh3,630, dizeli Sh3,734 na mafuta ya taa Sh3,765.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Laizer alisema bado ruzuku inayotolewa haijaleta matunda yaliyokusudiwa.

Wakati TPSF wakisema hayo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), John Priscus alisema kuendelea kupanda kwa bei za mafuta kutafanya wanachama wake kushindwa kutoa huduma kutokana na gharama za uendeshaji kuongezeka kuliko faida.

Advertisement

“Tangu tulipopewa nauli mpya mafuta yameshaongezeka kwa zaidi ya asilimia 75, sasa unaongezewa nauli ya Sh3,000 halafu mafuta yanapanda kwa kiasi hiki unapata nini. Wakati mafuta yako Sh2,000 mtu alikuwa anatumia Sh1 milioni kwa ajili ya mafuta hadi Mwanza, lakini sasa zidisha lita 500 kwa Sh3,322 (dizeli).

“Utaona gharama ilivyoongezeka, ile Sh3,000 iliyowekwa katika nyongeza ya nauli kwa watu 60 ni Sh180,000 pekee, hivyo kilichoongezeka ni kidogo kuliko tunachotumia kutoa huduma,” alisema Priscus.

Aliitaka Ewura kuwa na utaratibu wa kufanya makadirio ya kuongezeka kwa bei za mafuta walau kila baada ya miezi mitatu ili Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) itumie bei hizo kufanya ongezeko la bei za nauli.

Kilio kilipazwa zaidi na madereva wa daladala na bajaji kutoka sehemu mbalimbali nchini, wakitaka nauli ziongezeke ili waweze kukabiliana na ugumu wa maisha.

Musa Juma, ambaye ni dereva wa daladala mkoani Morogoro aliiomba Serikali kudhibiti ongezeko la bei ya mafuta, huku Latra ipandishe bei za nauli ili waweze kupata faida tofauti na sasa wanapofanya kazi kwa hasara.

Dereva Mohammed Abdul alisema umefika wakati sasa wanafanya kazi kwa ajili ya kulinda vibarua vyao na si kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

“Kama ulikuwa unabeba mzigo hadi Ubungo kutoka Buguruni kwa Sh30,000, sasa hivi ukimuambia mteja mafuta yamepanda bei akuongeze Sh10,000 hakuelewi kabisa, mwisho wa siku unapata wateja na fedha kidogo, jambo ambalo halina afya,” alisema Abdul.

Madereva wengine waliamua kuuliza msimamo wa vyama vyao kufuatia ongezeko la bei za mafuta, wakiwemo Chama cha wasafirishaji abiria mikoa ya Kilimanjaro na Arusha (Akiboa).

“Tatizo tunaloliona na hili tulishawaambia Latra. Kwamba wao wanapanga nauli elekezi bila kuangalia nini kinakuja mbele. Ewura wakitangaza bei leo kesho imeanza kutumika sisi tunaambiwa tusubiri Latra. Tunawasikilizia,” alisema Hussein Mrindoko ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho.

Dereva wa gari ndogo ya abiria mjini Kigoma, Peter Salim alisema bei mpya iliyotangazwa na Ewura hailingani na ongezeko la Sh100 kwenye nauli, hali anayoamini itawalazimisha kupandisha nauli.

Kilio kilifika mpaka kwa madereva bodaboda, wakisema ongezeko la bei limeongeza ugumu katika biashara zao.

“Ilikuwa ni rahisi sehemu ya Sh2,000 mtu anaomba umpeleke kwa Sh1,500, sasa hivi ni gumu, mimi mwenyewe nikienda kituo cha mafuta na Sh2,000 nikiomba mafuta kama zamani sipati, hivyo lazima nione nakabiliana na hali hii vipi,” Peter Ignas, dereva wa bodaboda jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Chama cha kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama alisema bado hajaona matokeo ya ruzuku, huku akionyesha shaka kuwa huenda kuna hujuma zinafanyika.


Vilio vya wananchi

Kupanda kwa mafuta kumewaibua pia watumishi wa umma ambao waliongezewa kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 23.3, wakisema ni kama ongezeko hilo limetolewa na mkono mmoja na kuchukuliwa na mkono wa pili.

“Katika mshahara wangu iliongezeka Sh12, 000 tu. Yaani haijapita hata mwezi mafuta yameongezeka, leo (jana) hapa Moshi nimenunua lita ya petroli kwa Sh3,481. Yaani naona kuna kitu hakiko sawa,” alidai mtumishi mmoja.

Mwajuma Ally aliiomba Serikali kuangalia namna ya kupanga bei ya mafuta ili kuzia mfumuko wa bei za chakula.

“Bei inavyozidi kupanda wanaoumia ni wananchi wa hali ya chini, hivyo serikali iangalie namna ya kuweka bei moja ambayo itakuwa haipandi wala haishuki,” alisema Mwajuma.


Mtizamo wa wachumi

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara mjini Moshi, Conrad Kabewa alisema athari za kupanda huko kwa bei ya mafuta zinakwenda kuathiri sekta zote kuanzia usafiri hadi uzalishaji kuathiri pia bei za bidhaa sokoni.

“Athari obviously (kwa vyovyote) za kupanda bei ya mafuta ni mbaya. Tukiendelea hivi malengo mengi yaliyopangwa kufikiwa kiuchumi katika bajeti hii (2022/23) hayatafanikiwa. Serikali ichukue hatua ikibidi ipunguze tozo,” alisema Kabewa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Repoa, Dk Donald Mmari alisema suala hili huweza kusababisha mfumuko wa bei hivyo kupunguza thamani ya vipato vya wafanyakazi na wazalishaji, pia inaweza kupunguza kasi ya kukua kwa uchumi.

Imeandikwa na Aurea Simtowe, Kelvin Matandiko, Halili Letea (Dar), Daniel Mjema, Alodia Dominic, Hamida Shariff, Fina Lyimo, Beldina Nyakeke (Musoma), Damian Masyenene (Mwanza), Happiness Tesha (Kigoma) na Samira Yusuph (Bariadi).

Advertisement