Magaidi yawateka madaktari wa Cuba nchini Kenya

Muktasari:

  • Walienda kutoa huduma katika kaunti ya Mandera, wamewatoroshea nchini Somalia huku wakiwafyatulia risasi polisi waliokuwa wakiwalinda madaktari hao na kuua mmoja

Mandera, Kenya. Watu wanaoaminika kuwa magaidi wa Al-Shabaab waliwavamia na kuwateka nyara madaktari kutoka nchini Cuba waliokuwa wakitoa huduma za mataibabu kaunti ya Mandera.

Madaktari hao walikuwa wakielekea kazini wakitumia gari la Serikali ya kaunti hiyo saa tatu asubuhi, huku wakiwa wamelindwa na Polisi  wawili mpaka walipovamiwa barabarani, eneo la Banisa.

Walioshuhudia uvamizi huo walisema, baada ya kuzuia gari lililokuwa likisafirisha madaktari hao, magaidi hao walianza kuwafyatulia risasi polisi na walimuua ofisa wa AP, Hussein Katambo Ngala. Ofisa mwenzake kutoka idara ya polisi wa kawaida alifanikiwa kutoroka.

Magaidi hao waliwalazimisha madaktari hao kuingia katika gari lao, kisha wakaondoka haraka.

“Walizuiwa na magari mawili aina ya Toyota Probox njiani. Kwa bahati mbaya, ofisa wetu wa AP alipigwa risasi na akafariki papo hapo,” amesema msemaji wa Polisi, Charles Owino.

Amesema magaidi hao walivuka mpaka na kuelekea Somalia, na kudai kwamba polisi wanamshikilia dereva aliyekuwa akiwasafirisha madaktari hao kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.

“Maafisa wetu wote wa usalama na jeshi wanashirikiana na wanaendelea kufuata hao magaidi katika mpaka wetu wa Kenya na Somalia,” amesema Owino.

Hata hivyo polisi hawakuwataja madaktari hao waliotekwa nyara, kwa mujibu wa taarifa kutoka wizara ya afya, daktari wa upasuaji Landy Rodriguez na Dkt Assel Herera Correa ndio walitumwa katika kaunti hiyo, ambayo inapakana na Somalia.