Magari sita ya shule Morogoro yarudishwa gereji baada ya kukosa sifa
Muktasari:
- Jeshi la Polisi limekagua magari 21 ya shule kabla ya muhula mpya kuanza huku magari sita yakizuiwa kubeba wanafunzi hadi yatakapofanyiwa matengenezo
Morogoro. Siku chache kabla ya shule kufunguliwa, Jeshi la Polisi Wilaya ya Morogoro kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limekagua magari 21 ya shule huku sita yakizuiwa kubeba wanafunzi baada ya kubainika kutokidhi vigezo vya usalama na kuelekezwa kufanyiwa matengenezo.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wanafunzi wanatumia vyombo vya usafiri vilivyo salama na kupunguza hatari ya ajali zinazoweza kuepukika wakati wa kwenda na kutoka shuleni.
Akizungumza na madereva wa magari hayo baada ya shughuli hiyo leo Jumamosi Julai 4, 2026 mjini hapa, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Morogoro, Paschal Mwakabungu amesema ukaguzi huo unalenga kuhakikisha magari yote yanayobeba wanafunzi yako katika hali nzuri kabla ya kuanza kutoa huduma.
Mwakabungu amesema Jeshi la Polisi halitaruhusu gari lolote la shule kubeba wanafunzi bila kukaguliwa na kuthibitishwa kuwa linakidhi viwango vya usalama.
“Tunataka kuhakikisha watoto wetu wanasafirishwa kwa usalama. Hivyo, hakuna gari la shule litakaloruhusiwa kubeba wanafunzi bila kukaguliwa na kuthibitishwa kuwa linafaa kwa matumizi,” amesema Mwakabungu.
Mmoja wa madereva wa magari yaliyokaguliwa, Abedi Nasoro kutoka Shule ya Ndetembia amesema pamoja na ukaguzi huo, madereva wamepatiwa elimu kuhusu usalama barabarani, ikiwamo umuhimu wa kutofuata mwendokasi, kutopakia wanafunzi zaidi ya uwezo wa gari na kuhakikisha vifaa vya huduma ya kwanza vinapatikana muda wote.
“Tumepata maelekezo yatakayosaidia kuboresha utendaji wetu wa kazi wa kila siku na kuongeza umakini na usalama wa wanafunzi tunaowasafirisha,” amesema.
Mmoja wa mzazi wa wanafunzi, Jackson Busanda ameipongeza polisi kwa kufanya ukaguzi huo, akieleza unawapa wazazi utulivu wa moyo wakijua watoto wao watatumia magari yaliyothibitishwa kuwa salama.
Joseph Mwarida, mzazi wa mwanafunzi anayesafiri kwa gari la shule, aliwataka wamiliki wote wa shule kuhakikisha magari yao yanapelekwa kukaguliwa kabla ya kuanza kubeba wanafunzi ili kulinda maisha ya watoto.
Amesema usalama wa wanafunzi unapaswa kupewa kipaumbele na wadau wote wa elimu, akieleza kuwa ukaguzi wa mara kwa mara wa magari ya shule ni hatua muhimu ya kuzuia ajali zinazoweza kuepukika lakini hata daladala nazo zinapaswa kukaliwa mara kwa mara.