Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mageuzi makubwa tiba ya moyo

Wataalamu wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Hospitali ya Starcare ya India wakifanya upasuaji mdogo wa moyo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) bila kufungua kifua katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo inayofanyika JKCI.

Muktasari:

  • Wagonjwa wenye umri kuanzia miaka 70 kutofunguliwa kifua kubadilisha valvu, ngozi ya ng’ombe au nguruwe kutumika kutengeneza valvu

Dar es Salaam. Wagonjwa wenye tatizo la kuziba mshipa mkubwa wa damu ndani ya moyo wameanza kutibiwa bila kufungua kifua katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Kupitia teknolojia hiyo mpya ambayo kifaa maalumu huingizwa hadi kwenye mshipa husika na kuanza tiba,  wagonjwa watatu wameshatibiwa.

Awali, wagonjwa waliobainika kuwa na maradhi hayo ya moyo walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu.

Imeelezwa huduma ya kutibu kwa kufungua kifua itaendelea lakini itawahusu vijana pekee.

Daktari bingwa wa matibabu kwa njia ya tundu dogo kutoka JKCI, Dk Khuzeima Khunbhui, amesema leo Desemba 14,2023 kuwa, tiba kwa njia hiyo itawanufaisha watu kuanzia miaka 70 na kuendelea.

"Kipindi cha nyuma tulifanya upasuaji kufungua kifua na kuweka valvu kwenye mshipa wa moyo kwa watu wa miaka 70 na kuendelea, sasa tutatumia njia ya tundu dogo kuweka valvu hiyo kwenye mshipa wa moyo ulioziba,” amesema na kuongeza:

Valvu hiyo inayotengenezwa kwa ngozi ya ng’ombe au nguruwe ina uwezo wa kudumu miaka 15 kwenye mshipa wa moyo.”

Amesema tafiti zinaendelea duniani kuangalia iwapo valvu zinazowekwa sasa zinaweza kudumu zaidi ya miaka 15 kama vijana watawekewa.

Amefafanua kuwa, tiba wanayopata vijana wenye matatizo hayo ni kuwekewa chuma ndani ya mshipa wa moyo ambao hudumu kwa muda mrefu, huku mgonjwa akitakiwa kutumia dawa kwa maisha yake yote.

Dk Khunbhui amesema iwapo vijana watatibiwa kwa njia ya tundu dogo, itawahitaji kufanyiwa mabadiliko ya valvu watakayowekewa baada ya miaka 15.

 Donald Lema, mkazi wa Machame mkoani Kilimanjaro, amesimulia namna alivyobaini ugonjwa huo, akisema alianza kujisikia mwili kukosa nguvu na akitembea mita 100 lazima apumzike, hivyo alienda kufanya uchunguzi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC, alikoambiwa valvu moja ya moyo imelegea.

“Niliambiwa matibabu ni India au JKCI, nilikuja JKCI na nimepatiwa matibabu, sasa naendelea vizuri. Sikuhisi maumivu eneo lolote la mwili,” anasema.

Anasema gharama ya matibabu alipaswa kulipa Sh80 milioni lakini alilipa Sh25 milioni, nyingine zikigharimiwa na Serikali.

Kiini cha tatizo

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI, Tatizo Waane amesema ugonjwa huo hutokana na mabadiliko ya mwili.

Amesema kwa watu wazima tatizo hilo huchangiwa na umri mkubwa, ambao valvu husababisha kuzalishwa madini chokaa ndani ya mshipa wa moyo.

“Chokaa hizo hujikusanya na baadaye hufanya damu kushindwa kutoka na kuingia kwenye moyo; hivyo figo, ubongo na viungo vingine mwilini huanza kupata damu kidogo. Mhusika huanza kupata maumivu ya kichwa na kifua,” amesema.

Dk Waane amesema kupitia njia ya tundu dogo daktari humhudumia mgonjwa ndani ya saa moja hadi mbili, na mgonjwa kuondoka wodini siku inayofuata tofauti na upasuaji wa kufungua kifua ambao mgonjwa hutumia zaidi ya wiki wodini.

Kuhusu gharama ya matibabu anasema mgonjwa mmoja nchini atatibiwa kwa Sh80 milioni tofauti na nje ya nchi ambako anatibiwa kwa Sh150 milioni.

Uwezo wa watalaamu

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema uwezo wa wataalamu ndani ya taasisi hiyo uliwezeshwa na wenzao wa Hospitali ya Starcare ya nchini India.

Amesema hivi sasa madaktari wa JKCI kwa asilimia 90 wana uwezo wa kutoa huduma hiyo ambayo kwa Afrika inapatika Tunisia, Afrika Kusini na Morocco.

JKCI imesema inaendelea kuwa kituo cha utalii tiba na kwamba, wagonjwa kutoka nchi 20 za Afrika wanafika kwenye taasisi hiyo kupokea matibabu.

Kutokana na wigi wa wagonjwa, Dk Kisenge ameiomba Serikali jengo lingine kwa ajili ya kuwahamishia wagonjwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk John Jingu, amesema ombi hilo linafanyiwa kazi.

Dk Jingu amesema uwekezaji kwenye sekta ya afya una umuhimu mkubwa, akisema kwa mwaka huu, Serikali imeweka Sh7 trilioni kwenye sekta ya afya.

Kuhusu wataalamu, amesema zaidi ya Sh10.9 bilioni zimewekezwa na Serikali kusomesha wataalamu kwenye nchi mbalimbali, ambao watakuja kutoa matibabu ya kibingwa nchini.

Amesema kati ya Julai hadi Desemba, mwaka huu, JKCI imehudumia zaidi ya wagonjwa 3,000 na kuingiza Sh920 bilioni.