JKCI waokoa Sh100 milioni

Mtaalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa kutoka nchini Poland, Prof Tomasz Mroczek (wa pili kulia) akifanya upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu ya moyo ambayo haijakaa katika mpangilio wake.
Muktasari:
- JKCI wameokoa Sh 100 milioni baada ya kufanyika kwa upasuaji mkubwa kwa watoto watano kupitia madaktari bingwa kutoka Poland walioweka kambi ya siku tano katika taasisi hiyo.
Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wameokoa Sh100 milioni kwa kutopeleka watoto wenye matatizo ya moyo nje ya nchi baada ya kufanyiwa upasuaji hapa nchini.
Watoto hao ambao wamefanyiwa upasuaji mkubwa na madaktari bingwa kutoka Poland endapo wangepelekwa nje ya nchi kila mmoja angetumia Sh20 milioni kwa ajili ya upasuaji.
Ujio wa madaktari hao ambao mmoja ni bingwa katika mabingwa wa kufanya upasuaji duniani umeenda kufungua milango ya mafunzo kwa madaktari hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Septemba 22,2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji JKCI Daktari, Peter Kisenge kwenye hafla ya kuwaaga madaktari hao.
Amesema madaktari hao walikuwepo nchini tangu Septemba 17,2023 kwa ajili ya kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto, kurekebisha mishipa ya damu ya moyo ambayo haijakaa katika mpangilio wake tundu dogo na kutoa mafunzo na ujuzi kwa madaktari wa taasisi.
Pia Kisenge amesema hiyo ni fursa kwa taasisi katika mashirikiano ambayo inakwenda kufungua milango ya kufanya tafiti mbalimbali zitakazoleta manufaa kwa nchi ikiwepo uingizaji wa fedha za kigeni.
"Walipofika wametuonyesha vitu ambavyo kwetu sisi ilikuwa ni vigunu kufanya kwani wamekuja kutuonyesha namna ya kutumia mitambo iliyopo ikiwepo kurekebisha mishipa ya damu kwenye moyo," amesema Kisenge.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo wa watoto, Prof Tomasz Mroczek amesema madaktari wa Tanzania wapo tayari kujifunza kwa ajili ya kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo na kufanyakazi kwa bidii na umakini zaidi.
"Tutaendelea kushirikiana katika kufanyakazi ya kutibia watoto na kufanya tafiti zitakazosaidia katika matibabu.
"Pia hii ni mara yangu ya kwanza kuja Tanzania sikutarajia kuona nilichokikuta lakini naahidi kuendeleza ushirikiano kwa hawa madaktari," amesema Mroczek.
Awali Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI, Angela Muhozya amesema uwepo wa madaktari hao ambao ni daktari bingwa wa moyo na daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto umetoa fursa kwa wao kujifunza mambo makubwa zaidi katika upasuaji wa moyo.
"Tangu tumeingia nao mkataba ni mwaka sasa na tulipopata nafasi ya kuwatembelea wenzetu katika chuo chao tuliona ni namna gani wanafanya upsauaji wa mishipa ya damu pamoja na moyo tukatumia fursa hiyo kuomba waje nchini ili na sisi tuweze kufaidika," amesema Angela.
Hata hivyo, Muhozya amesema hadi sasa kuna madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo wawili ambao wamehitimu chuo nchini Uswis na katika mpango wao wa miaka mitano wanampango wa kupeleka tena madaktari watatu ili kuongeza idadi ya madaktari bingwa kwenye taasisi.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto wa JKCI, Godwin Sharau amesema uwepo wa madaktari bingwa kutoka Poland umesaidia kwa wao kujifunza zaidi kwani madaktari hao ndani ya siku tatu wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji mkubwa watoto watano ambao ulikuwa mgumu kwa wao kufanya.
"Wamekutana na madaktari ambao wanaamini tunaweza kufika kwenye viwango vya juu kutokana na utendaji wetu na pia kwetu ni fursa kwani daktari huyo anatumiwa na watu wengi duniani katika kusaidia watoto hivyo walivyofundisha tutavitumia kwa jaili ya kusaidia wananchi," amesema Sharau.