Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Wenye shinikizo la damu hatarini kupata ugonjwa wa moyo’

Baadhi ya wananchi waliofika Hospitali ya Mawenzi kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo

Muktasari:

  • Madaktari bingwa wa Moyo kutoka JKCI kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa Mawenzi, wameweka kambi ya siku tano kuanzia Agosti 21 hadi 25 mwaka huu katika Hospitali ya Mawenzi kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa za moyo, lengo likiwa ni kuwasogeza wananchi huduma karibu na kujengeana uzoefu.

Moshi. Wagonjwa wa shinikizo la juu la damu, wametajwa kuwa hatarini zaidi kupata magonjwa ya moyo, kutokana na ugonjwa huo kudaiwa kusababisha moyo kutanuka.

Hayo yamebainishwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo katika mikoa 11 iliyokwenda kutoa huduma za matibabu ya moyo, kila watu 10 waliogundulika kuwa na magonjwa ya moyo, watu sita walikutwa na shinikizo la juu la damu.

Madaktari bingwa wa Moyo kutoka JKCI kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa Mawenzi, wameweka kambi ya siku tano kuanzia Agosti 21 hadi 25 mwaka huu katika Hospitali ya Mawenzi kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa za moyo, lengo likiwa ni kuwasogeza wananchi huduma karibu na kujengeana uzoefu.

Akizungumza leo Jumanne Agosti 22, 2023 wakati wa utoaji wa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka JKCI, Dk Petro Pallangyo amesema katika kambi ambazo wamekwenda kwenye mikoa 11 nchini, ugonjwa ambao umeongoza ni shinikizo la juu la damu.

Amesema pia kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya shinikizo la juu la damu kwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 ambapo utafiti umeonyesha kuwa, sababu hatarishi ni unywaji wa pombe uliokithiri, uvutaji wa sigara, uzito uliopindukia, ulaji usiofaa na kutofanya mazoezi.

"Katika mikoa 11 tuliyopita tuliweza kubaini mambo mbalimbali ambapo kwa upande wa watoto, tumeweza kuwapa rufaa  watoto 156 ambao walikutwa na matatizo ya moyo ambapo asilimia 80 walikutwa na magonjwa ya kuzaliwa nayo ikiwemo matundu kwenye moyo na asilimia 20 yaliongozwa na magonjwa ya valvu za moyo," amesema.

Ameongeza kuwa "Kwa watu wazima magonjwa matatu ambayo yameongoza katika kila eneo tulilokwenda la kwanza ni shinikizo la juu la damu ambapo kila watu 10 tuliowagundua kuwa na ugonjwa wa moyo, watu sita walikuwa na shinikizo la juu la damu na asilimia iliyobaki magonjwa yaliyoongoza yalihusisha moyo kutanuka na mishipa mikubwa ya damu kuziba, na wagonjwa hawa zaidi ya 700 tumeweza kuwapa rufaa kwenda JKCI," amesema.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema madaktari bingwa wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Mawenzi watatoa huduma kwa siku tano  ikiwa ni mwendelezo wa tiba mkoba ya Rais Samia Suluhu Hassan yenye nia ya kuwafikishia wananchi huduma bobezi katika maeneo waliyopo.

Kisenge ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, amesema taasisi hiyo tayari imefikia mikoa 11 na kuona watu zaidi ya 7,000 ambapo kati yao zaidi ya 700 wamepewa rufaa za kwenda JKCI baada ya kubainika kuwa na matatizo ya Moyo.

"Nia ya taasisi yetu ni kuhakikisha tunaleta ujuzi kwenye Hospitali ya Mawenzi lakini pia kuwaletea wananchi huduma karibu, na wagonjwa wengi ambao wanakuja hapa, wanashinikizo la damu, na hili tumeliona pia kwenye kambi nyingine  ambazo tumezifanya maeneo mengine nchini na hili limeleta madhara ya moyo kutanuka,"amesema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi, Dk Edna-Joy Munisi amesema muitikio wa watu umekuwa mkubwa ambapo katika siku mbiki za wwanzo watu zaidi ya 600 wamejitokeza kupata huduma za matibabu ya moyo.

"Naishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia kwa kuweza kuleta huduma karibu na wananchi, watu wamejitokeza kwa wingi, jana siku ya kwanza wamejitokeza watu 300 na leo siku ya pili wamejitokeza tena zaidi ya 300, hivyo mwitikio ni mkubwa sana," amesema.