Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Magonjwa 10 yaliyosumbua mwaka 2023 haya hapa

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya sekta ya afya kwa mwaka 2023, jana jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Serikali imetaja magonjwa 10 yaliyowatikisa Watanzania kwa mwaka 2023, huku maambukizi ya njia ya mkojo na mfumo wa hewa yakitajwa kuwakumba wananchi wengi zaidi.

Dar es Salaam. Serikali imetaja magonjwa 10 yaliyowatikisa Watanzania kwa mwaka 2023, huku maambukizi ya njia ya mkojo na mfumo wa hewa yakitajwa kuongoza.

Kwa mwaka 2023, maambukizi ya mfumo wa hewa yaliwaathiri Watanzania milioni 4,901,844 sawa na asilimia 18.9, huku matatizo ya njia ya mkojo (UTI) ikiathiri Watanzania milioni 4,095,104 sawa na asilimia 15.8.

Magonjwa hayo yalitajwa leo Januari 10, 2023 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akieleza mafanikio na mikakati ya Wizara ya Afya mwaka 2024.

Katika orodha yake Ummy  ametaja ugonjwa mwingine kuwa ni malaria iliyoathiri  watu milioni 1,772,523 sawa na asilimia 6.9, shinikizo la damu watu milioni 1,455,165 sawa na asilimia 5.6, vidonda vya tumbo watu 963,520 sawa na asilimia 3.7.

Magonjwa mengine ni yale yasiyo ya kuambukiza ambayo yaliathiri watu 830, 059 sawa na asilimia 3.2 huku homa ya mapafu ikiathiri watu 703,666 sawa na asilimia 2.7.

Ugonjwa wa kisukari pia umetajwa na waziri huyo kuwa umeathiri  watu 652,455 sawa na asilimia 2.5, minyoo watu 611,538 sawa na asilimia 2.4 pamoja na magonjwa mchanganyiko ambayo yameathiri watu 552,661 sawa na asilimia 2.1.

 “Magonjwa yalioongoza kwa wagonjwa wa nje kuwa ni mafua na kikohozi, yakiathiri watoto 5,410,576, huku tatizo la kuharisha likiwapata watoto 1,168,763, na malaria watoto 1,483,845,

"Pia yapo maambukizi kwa njia ya mkojo UTI ambayo iliathiri watoto 1,050,723, homa ya mapafu watoto 1,029,548, maambukizi ya ngozi watoto 526, 983, huku magonjwa mengine ya mfumo wa chakula yakiathiri watoto 524, 698," ameeleza.

Kuhusu vipimo vya UTI kutiliwa shaka usahihi wake, Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu amesema majibu ya ugonjwa huo hayapaswi kuwa ya papo kwa papo.

Amesema ili kubaini vimelea vya ugonjwa huo ni lazima sampuli ioteshwe kwa saa 24.

Amewataka wataalamu kuhakikisha vipimo vya ugonjwa huo vinaingia maabara kufanyia uchunguzi ndipo wagonjwa wapewe dawa, kwani pasipo kufanya hivyo ni kuongeza tatizo la usugu wa dawa kwa wananchi.

“Wataalamu wote wa maabara wahakikishe kimelea cha UTI wanachokibaini kinaendana na dawa inayotolewa kwa mgonjwa,” amesema.

Akizungumzia namna ya kujikinga na matatizo hayo, Waziri Ummy ameitaka jamii kutoyapuuza mafundisho ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mohamed Janabi, kuhusu ulaji unaoshauriwa kiafya.

“Watu wanafanya mzaha na Profesa Janabi na mafundisho anayotoa japo wakati mwingine hata mimi ananitisha, mimi ni mwanafunzi wake na ameniharibu tangu Mei mwaka jana sinywi chai yenye sukari," amesema.

Naye Mtaalamu Mshauri wa Afya ya Jamii, Festo Ngadaya amesema kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni muhimu jamii ikapunguza ulaji wa vyakula vya wanga kupita kiasi na kuzingatia mazoezi.

Kwa magonjwa ya mlipuko na homa ya matumbo amesema usafi na kuepuka vyakula vibichi ni njia ya kujikinga nayo.

Kuhusu wajawazito

Akitoa takwimu za wajawazito waliojifungulia vituo vya afya, Ummy amesema kiashiria kikuu cha ubora wa huduma za afya katika nchi yoyote duniani ni kiwango cha wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutoa huduma za afya.

“Mwaka 2023 wajawazito 2,391,427 sawa na asilimia 97.5 walihudhuria kliniki  mara nne katika kipindi  cha ujauzito wao, lengo la nchi ni kufikia asilimia 80 mwaka 2030 kama inavyoelekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO),”amesema.

Mgawanyo alioutoa Waziri huyo kuhusu wajawazito, amesema mwaka 2022 waliojifungua vituo vya kutoa huduma ni asilimia 81, mwaka 2023 waliojifungulia vituo hivyo waliongezeka kufikia asilimia 85.

Ongezeko hilo analitaja kuwa ni hatua nzuri kufikia asilimia 95 kwa nchi kuwa na wanawake wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ifikapo mwaka 2030.

Magonjwa ya mlipuko

Kwa takwimu za mwaka jana, ugonjwa wa kipindupindu uliathiri mikoa 12 nchini,   watu 927 wakiupata ugonjwa huo huku kukishuhudiwa vifo 27.

Mikoa iliyobainika kuwa na ugonjwa huo mwaka jana ni  Arusha iliongoza kwa wagonjwa 214 , Mara wagonjwa 193 na vifo vinane, Simiyu wagonjwa  184 na vifo viwili  na sasa kuna mikoa sita inaendelea na mlipuko ambayo ni Shinyanga, Ruvuma, Tabora, Simiyu, Mwanza na Kagera

Utalii tiba

Akizungumzia utalii wa tiba nchini Waziri Ummy amesema  kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuboresha huduma za kibingwa na bobezi, Tanzania mwaka 2022 ilivutia  watu 1,699 kuja kupata matibabu nchini.

"Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha kuwa jumla ya wagonjwa 1,937 waliotoka nje ya nchi walikuja kutibiwa nchini. Wagonjwa hawa wanatoka katika nchi za Comoro, Malawi, Burundi, Zambia, Congo DRC, Uganda, Zimbabwe na Kenya.

Wagonjwa hawa walihudumiwa katika Hospitali sita ikiwamo  Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa MOI, Aga Khan na Saifee.

Vikwazo kwenye sekta ya afya

Akieleza changamoto kwenye sekta ya afya, Ummy amesema wanakabiliwa na upungufu watumishi hasa wataalamu wa maabara, misuli na usingizi.

“Tuna changamoto ya ubora wa huduma kwa baadhi ya maeneo zinakotolewa  kutokana na usimamizi usioridhisha kwa baadhi ya watumishi, pia kuna mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga na mifuko wa bima ya afya, hivyo kushindwa kugharamia huduma wanazozihitaji,”amesema.

Changamoto nyingine ni kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza mfano ugonjwa wa kisukari, tatizo lingine ni kuibuka kwa magonjwa ya watoto yanayozuilika kwa chanjo kama vile surua, polio na  tetekuwanga. “Hali hii inasababishwa na watoto wengi  kutopata chanjo kwa wakati.

“Mwaka 2023 kulitolewa taarifa ya ugonjwa wa Polio kwa mtoto katika Manispaa ya Mpanda ambapo kwa kipindi kirefu ugojwa huu ulikuwa umedhibitiwa hapa nchini,”amesema.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Ummy amesema Serikali katika sekta ya afya imeweka kipaumbele kuimarisha afua za kinga.

Amesema lengo ni kuwawezesha wananchi kujikinga na magonjwa na kuyatambua mapema.

Pia Ummy amesema kipaumbele kingine ni kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ili kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma za afya bila ya kikwazo cha fedha

“Tutaongeza idadi ya watumishi wa afya katika ngazi zote sambamba na kuwajengea uwezo watumishi walio kazini, kwa kuwapeleka madaktari bingwa walioko hospitali za rufaa za mikoa katika vituo vya afya na hospitali za wilaya, kutoa  mafunzo kwa vitendo kuhusu utoaji wa  huduma bora za afya kwa wajawazito na watoto,”amesema.

Maeneo mengine ni kuongeza uwezo wa ndani wa kuzalisha vifaa, vifaa tiba na dawa, kukamilisha mwongozo wa gharama wa utoaji huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya za umma, ili kuwa na uwiano sawa wa bei za utoaji wa huduma.

Kuhusu wizi wa dawa, Mfamasia Mkuu wa Serikali,  Daudi Msasi amesema dawa zote zinazotolewa na Serikali zina nembo maalumu na endapo kuna uchepushaji Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) inafanya ukaguzi mara kwa mara kubaini uhalifu huo.