Magonjwa matatu yaliyowaathiri zaidi watu

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/24 jana Ijumaa Mei 13, 2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Waziri wa Afya Tanzania, Ummy Mwalimu ametaja magonjwa yaliyoongoza kuwaathiri kwa watu katika kipindi cha kati ya Julai 2022 hadi Machi 2023.
Dar es Salaam. Serikali imesema maambukizi katika mfumo wa hewa ni miongoni mwa magonjwa yaliyoongoza kwa kuwaathiri watu wengi katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2023/24.
“Magonjwa yaliyoongoza katika kuwaathiri zaidi wananchi na kuwasababishia kwenda katika vituo vya huduma kupata matibabu ni maambukizi katika mfumo wa hewa (asilimia 24), maambukizi ya njia ya mkojo (asilimia 13) na malaria (asilimia 7),”amesema.
Amesema magonjwa yaliyoongoza kwa watu wengi kulazwa ni malaria (asilimia 11), homa ya mapafu (asilimia 10) na anemia (asilimia 6.2) ikilinganishwa na na kipindi kama hicho mwaka 2021/22 ambapo homa ya mapafu (asilimia 11.6), malaria (asilimia 11.5) na anemia (asilimia 6.4).
Amesema magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi hadi kufikia kuwemo katika orodha ya magonjwa kumi yanayoongoza kusababisha watu kuhudhuria katika vituo vya kutolea huduma za afya.