Serikali kuweka ahueni gaharama za matibabu

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/24 jana Ijumaa Mei 13, 2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Baada ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu gharama kubwa za matibabu katika vituo vya afya vya umma, Serikali imesema imekamilisha mapitio ya mwongozo wa bei wa uchangiaji gharama za huduma za afya katika vituo vya umma vya utoaji huduma za afya.
Dodoma. Serikali imekamilisha mapitio ya mwongozo bei ya uchangiaji gharama za huduma za afya katika vituo vya huduma za afya vya umma ambao utawapunguzia mzigo wa matibabu wananchi.
Mwongozo huo utawezesha uwepo kwa bei ambazo ni sawa kwa nchi nzima kwa ngazi ya utoaji huduma za afya inayofanana.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2023/24, waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu amesema mwongozo huo umeainisha bei za huduma mbalimbali ambazo wananchi wasio na bima ya afya watapaswa kuchangia kupitia utaratibu wa papo kwa papo.
Amesema bei hizo zimejumuisha ngazi zote za utoaji huduma kuanzia katika ngazi ya afya ya msingi hadi Taifa.
“Kukamilika kwa mwongozo huo kutawapunguzia wananchi mzigo wa matibabu na kuwepo kwa bei ambazo ni sawa kwa nchi nzima kwa ngazi ya utoaji huduma inayofanana,”amesema.
Amesema mwongozo huo pia utawaondolea watu adha ya kutojua gharama za matibabu au kutozwa fedha zaidi ya matibabu yaliyotolewa.