Magonjwa haya 10 yanavyoongoza kwa vifo

Muktasari:
Ripoti ya WHO ya mwaka 2016 iliyotolewa Mei 24, kwa kuangalia nchi zenye vipato mbalimbali imeeleza kuwa vifo katika nchi za kipato cha chini duniani, magonjwa yanayoongoza ni ya mfumo wa upumuaji, kuhara na moyo.
Dar es Salaam. Magonjwa mbalimbali husababisha vifo vya binadamu duniani lakini kuna haya kumi ambayo Shirika la Afya Duniani (WHO) limeyaeleza kuwa yanaongoza kuua katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.
Ripoti ya WHO ya mwaka 2016 iliyotolewa Mei 24, kwa kuangalia nchi zenye vipato mbalimbali imeeleza kuwa vifo katika nchi za kipato cha chini duniani, magonjwa yanayoongoza ni ya mfumo wa upumuaji, kuhara na moyo.
Mbali na hayo pia imeutaja Ukimwi, kiharusi, malaria na kifua kikuu.
Mengine ni matatizo ya uzazi kabla ya kujifungua, matatizo ya uzazi baada ya kujifungua na ajali za barabarani.
Kwa mujibu wa WHO, magonjwa yanayosababisha vifo katika nchi maskini ni yale ya kundi la kwanza.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa nia ni kuzikumbusha nchi kuweka mfumo bora zaidi wa afya ili kukabiliana na magonjwa yanayotajwa kuwaathiri zaidi watu.
Serikali yajipanga
Akizungumzia ripoti hiyo, naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema jana kuwa Serikali imeanza mikakati ya kudhibiti magonjwa ya mfumo wa hewa hususan kwa watoto.
Kutokana na hilo, alisema tayari kuna utaratibu wa chanjo ili kuhakikisha watoto wote wanaepukana na magonjwa hayo.
“Katika hili tulipata tuzo ya kuwa wa tatu kidunia kwa kuwapa chanjo watoto na hadi sasa asilimia 97 wameshapata chanjo hiyo, ”alisema Dk Ndugulile.
Kuhusu Ukimwi alisema wameweka msisitizo na kuja na mpango wa 90 90 90 kuhakikisha watu wanapima, wanaanza tiba na kugundua maambukizi mapya.
“Takwimu zinaonyesha kati ya watu 1.4 milioni walio na virusi vya Ukimwi, ni milioni moja pekee ndiyo wameanza kunywa dawa, hivyo juhudi zinaendelea kuwapata 400,000,” alisema Dk Ndugulile.
“Wagonjwa wa kifua kikuu kila mwaka wanagundulika 150,000, changamoto iliyopo ni kuwafikia ambapo wanafikiwa 60,000 bado 90,000 hatujawafikia na juhudi kuhakikisha na wao wanaanza dawa zinaendelea.”
Alisema Serikali iko katika hatua nzuri kukabiliana na magonjwa hayo na takwimu nyingine zikitoka zitakuwa na matokeo mazuri zaidi.
Kauli za watalaamu
Akizungumzia taarifa hiyo, Dk Phelemon Kalugira kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga alisema kuwa inawezekana ikawa kweli kutokana na baadhi ya magonjwa kama kifua kikuu na Ukimwi kuhitaji tiba ya muda mrefu.
Alisema magonjwa ya mfumo wa hewa kama nimonia, kifua kikuu huhitaji kupata tiba mapema, lakini kutokana na miundombinu maeneo mengi hususan ya vijijini ni ngumu wahusika kupata huduma haraka. “Wengi wao wanachelewa kutambulika na hufika hospitalini wakiwa katika hali mbaya, jambo ambalo huharakisha vifo vyao,” alisema.
“(Wapo) wanatumia dawa bila kufuata utaratibu na wengine huacha, kuwatafuta au kubaini walipo inakuwa ngumu, matokeo yake wanapoteza maisha.”
Alisema yapo maradhi yanayosababishwa na mtindo wa maisha kama moyo, kisukari na kiharusi ambayo zamani yalikuwa yakiwasumbua watu wa nchi zinazoendelea. “Yamevamia nchi zetu kutokana na elimu duni kama nilivyosema, mtindo wa maisha watu siku hizi hawatembei umbali mrefu, hawafanyi mazoezi vitu vingi vinafanywa na mashine,” alisema.
Aliongeza kuwa bahati mbaya maradhi hayo huua watu wengi katika nchi zinazoendelea kutokana na kuhitaji vipimo vya haraka na kuanza tiba ya muda mrefu.
Daktari wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Billy Haonga alisema umaskini unachangia watu wanaoishi katika nchi zinazoendelea kufa kwa maradhi hayo.
Haonga ambaye aliwahi kuwa rais wa Chama cha Madaktari (Mat), alisema mtu akiwa maskini anakuwa maskini wa elimu ya afya pia na maskini wa kufika vituo vikubwa vya afya.
Alisema mfano ni maradhi ya kuhara, malaria, mfumo wa hewa na kifua kikuu ambayo yanahitaji usafi, lakini mtu akiwa maskini anaweza asiwe na nyenzo za kumwezesha kutimiza hilo.
Dk Haonga alisema maradhi ya Ukimwi yanahitaji lishe bora na elimu juu na kwamba kikikosekana kimoja katika hivyo ni rahisi mgonjwa kupoteza maisha.
“Hayo mengine yatokanayo na mtindo wa maisha kama moyo, kiharusi yanahitaji elimu ya kutosha jinsi ya kujikinga, kupima afya mara kwa mara na kufanya mazoezi.
“Kwa bahati mbaya tunarudi kulekule maskini aache kutafuta ugali wa familia akapime afya bila kuumwa siyo rahisi,” alisema.