Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Magonjwa, vitendeakazi inavyoathiri mifugo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvivu, Profesa Elisante Ole Gabriel (aliyevaa miwani) akishuhudia ng’ombe akipandikizwa mitamba kwa njia ya kisiasa kwa kutumia mbegu za kwenye chupa, jijini Mwanza. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Baadhi ya magonjwa ya ng’ombe yaelezwa kuambukizwa kwa watu

Mwanza. Licha ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo ikilinganishwa na mikoa mingine, inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Miongoni mwa changamoto hizo ni uhaba wa vitendea kazi, miundombinu hafifu, elimu ndogo kwa wafugaji na wataalamu wachache ikilinganishwa na ukubwa wa kanda hiyo yenye mikoa sita.

Mikoa hiyo ni Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Kagera na Geita ambayo ina zaidi ya ng’ombe milioni 6.89 sawa na asilimia 25 ya idadi ya kitaifa; mbuzi milioni 3.64 sawa na asilimia 21 ya idadi ya kitaifa; na kondoo milioni 1.228 sawa na asilimia 14 ya idadi ya kitaifa.

Kaimu ofisa mfawidhi Kituo cha Uchunguzi na Kutambua Magonjwa ya Wanyama Kanda ya Ziwa (ZVC), Dk Subira Mwakabumbe anasema kutokana na changamoto hizo wanashindwa kutimiza malengo ya kudhibiti kikamilifu magonjwa hususan ya mlipuko.

Dk Mwakabumbe anasema magonjwa yanayosumbua zaidi katika ukanda huo hasa ni homa ya mapafu kwa ng’ombe (CBPP), sotoka ya mbuzi, homa ya nguruwe, kichaa cha mbwa, magonjwa yaenezwayo na kupe, kideri, mapele ngozi na ugonjwa wa miguu na midomo.

Anasema kwa mwaka 2016/17 walikufa ng’ombe 178 kati ya 866 walioripotiwa kuugua homa ya mapafu huku ng’ombe 56,420 wakichinjwa kuzuia ugonjwa huo kwa baadhi ya wilaya.

Pia, nguruwe 2,430 wameripotiwa kufariki kwa ugonjwa wa homa ya nguruwe katika wilaya za Nyamagana, Ilemela na Manispaa ya Bukoba.

“Mbwa 47,602 na paka 1,554 wamechanjwa kuzuia ugonjwa huo, halmashauri zimeshauriwa kuchanja mbwa wote kwenye wilaya zote,” anasema Dk Mwakabumbe.

Anataja magonjwa yaenezwayo na kupe kuwa ndilo tatizo kubwa kwa Kanda ya Ziwa na kwamba, husababishwa na wanyama kutoogeshwa tatizo ambalo linachangiwa na kutokuwapo na majosho ya kutosha.

Kwa kipindi hicho ng’ombe 43,971 waliugua magonjwa hayo kati ya hao, 2,692 walikufa huku ng’ombe milioni 2.2; mbuzi 480,194; na kondoo 239,803 waliogeshwa. Kuku 49,202 walikufa kwa kideri huku wengine milioni 1.02 wakichinjwa dhidi ya ugonjwa huo.

Kuhusu ugonjwa wa miguu na midomo wamekufa ng’ombe 108, wengine 14,617 waliugua huku ng’ombe 16,281 wakichinjwa ili kudhibiti ugonjwa huo. Matukio 929 ya ugonjwa wa mapele ngozi yalitolewa taarifa.

Watumishi na vitendeakazi

Kituo hicho kinachodumia mikoa sita yenye halmashauri 41 kwa ajili ya kuchunguza na kutambua magonjwa mbalimbali ya wanyama kina madaktari watano; wakaguzi wa mifugo na mazao 16 (zoo sanitary); wataalamu wa minada na maeneo ya kuhifadhi mifugo watano; na idara ya utawala wapo wawili.

Dk Mwakabumbe anasema licha ya kituo hicho kuwa na magari mawili tu, moja limechakaa na linahitaji fedha nyingi kukarabatiwa hivyo hivyo kukwaza ufuatiliaji magonjwa ikizingatia inatakiwa kuzunguka kanda nzima.

Waziri anena

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiwa ziarani Mwanza alitembelea ZVC na kukiri kuwapo changamoto kadhaa ikiwamo upungufu wa dawa za mifugo.

Ulega anasema kuna fursa kubwa za uwekezaji wa viwanda vya mazao na dawa za mifugo. Anasema wafugaji wengine hawaoni umuhimu wa kuchanja mifugo yao na kwamba magonjwa yanapunguza ubora na tija ya mifugo.

“Kwa sasa Serikali tumejipanga kudhibiti matatizo haya, wafugaji watumie vituo hivi kupata elimu, tunataka kuja na programu ya nchi nzima kuchanja mifugo iwe lazima kulingana na sheria namba 17 ya magonjwa ya mifugo,” anasema Ulega.

Bila kutaja kiwango cha fedha, Ulega anasema bajeti ya 2018/19 zimetengwa fedha za kuendeleza miundombinu ya ufugaji huku akiwaomba wadau wa mifugo kwa kushirikiana na halmashauri kuchangia uimarishaji wa majosho.

Naye mkurugenzi msaidizi wa kitengo cha afya ya veterinari, Dk Sero Luwango anasema ugonjwa wa utupaji mimba kwa ng’ombe nao umekuwa changamoto kwa wafugaji na mbaya zaidi ugonjwa huo unaambukizwa na binadamu.

“Mara nyingi ng’ombe huwa anatupa mimba inapofika miezi saba, wakati wa kutoa kondo kama hakuna kinga kwa wafugaji ndiyo anapata maambukizi zaidi unasababisha malaria kali, kuumwa kichwa na viungo vingine vya mwili,” anasema Dk Luwango.

Baada ya kutupa mimba wanyama hao hawawezi kuzaa tena, hivyo wanatakiwa kuondolewa kwenye kundi la wanyama wengine.

Kwa sasa tunakuwa na juhudu za namna ya kujikinga na kutoa elimu, wale ambao wamechunguzwa na kubainika lazima watolewe kwenye kundi kwa sababu hana faida yoyote maana hawezi kuzaa tena badala yake ni kusababisha athari ya kuambukiza magonjwa.