Magufuli: Sitaki watendaji, makandarasi kusingizia corona

#LIVE​: RAIS MAGUFULI AKIZINDUA FLYOVER YA UBUNGO || KITUO CHA MABASI MBEZI LUIS

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaagiza watendaji wanapotembelea miradi mbalimbali wasiwe na kisingizio cha ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona na kuwataka wananchi kuendelea kuchapa kazi.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaagiza watendaji wanapotembelea miradi mbalimbali wasiwe na kisingizio cha ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona na kuwataka wananchi kuendelea kuchapa kazi.

Ameeleza hayo leo Jumatano Februari 24, 2021 katika uzinduzi wa daraja la juu la Ubungo jijini Dar es Salaam.

“...,Barabara njia nane kwenda Kibaha, hatutaki visingizio na niwatake watendaji wangu pasiwe na kisingizio chochote cha ugonjwa wa corona wanapokagua miradi, viongozi wa CCM msikubali utetezi wowote ikiwemo kisingizio cha corona,” amesema.

Amewashukuru makandarasi waliofanya kazi ya ujenzi wa daraja hilo lililopewa jina la Kijazi Interchange kuwa  wamefanya kazi kubwa licha ya ugonjwa wa corona kuwepo mwaka 2020.

“Nitoe wito kwa makandarasi wengine nchi nzima wasitafute visingizio vya kuchelewa kazi mara corona mara sijui nini, hawa wamemaliza na corona ilikuwepo na daraja limekamilika,” amesema.

Ameiomba Wizara ya Ujenzi kuhakikisha wanachukua hatua makandarasi wanaochelewesha kazi kwa sababu ya corona.

“Ukienda site ukamkuta mkandarasi anasema amechelewa sababu ya corona mtoe akakoromee hukohuko, sisi kazi yetu iende haiwezekani tukawa tumeweka pesa halafu watu watafute visingizio.”

“Mara wataalamu wetu wapo nje, vifaa haviingii kwa sababu ya corona ni wizi unaofanywa na makandarasi na ndiyo maana mnaona daraja hili limekamilika na corona ipo lakini sisi tunaendelea na ndiyo maana mnaona hata daraja la Salender linaendelea kujengwa na wanasema mwezi wa 11 au 12 nalo linakamilika,” amesema Rais Magufuli.