Prime
Mahakama ilivyohalalisha Tume ya Jaji Lila
Muktasari:
- Mahakama hiyo ilihalalisha tume hiyo leo Ijumaa Julai 17, 2026 baada ya kutupilia mbali hoja za shauri la kupinga uhalali wake.
Kigoma. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Kigoma, imehalalisha Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mahakama hiyo ilihalalisha tume hiyo leo Ijumaa Julai 17, 2026 baada ya kutupilia mbali hoja za shauri la kupinga uhalali wake.
Uamuzi huo umetolewa jana, Ijumaa, na Jaji Wilbert Chuma aliyelisikiliza shauri hilo baada ya kukubaliana na hoja za mawakili wa Serikali waliowawakilisha wajibu maombi katika shauri hilo.
“Kwa muktadha huo, Mahakama hii inaona kwamba maombi haya yamekosa mashiko na inayatupilia mbali. Kila upande utabeba gharama zake,” amesema Jaji Chuma akihitimisha uamuzi huo baada ya kujadili hoja za pande zote na msimamo wa sheria husika.
Tume hiyo maarufu kama Tume ya Jaji Lila, ambayo mwenyekiti wake ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shabani Ally Lila, imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wake ulitangazwa rasmi Mei 18, 2026.
Rais Samia aliunda tume hiyo kutokana na mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, iliyowasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026.
Hata hivyo, uamuzi wake wa kuunda na kuteua makamishna wa tume hiyo ulipingwa mahakamani na mwanaharakati Bubelwa Ephraim Bubelwa na mwenzake Joseph Daudi Mabugo, kupitia shauri la mapitio ya kimahakama (Judicial review) lililofunguliwa.
Walalamikiwa katika shauri hilo walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Lila, na makamishna wake watatu.
Makamishna hao wa tume hiyo ambao pia walikuwa walalamikiwa katika shauri hilo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Katika shauri hilo, walalamikaji hao walikuwa wanaiomba Mahakama hiyo itengue uamuzi wa Rais Samia wa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo na kutoa amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.
Pamoja na mambo mengine, wanapinga uamuzi wa Rais wa uteuzi wa makamishna hao wa tume hiyo wakidai kuwa Rais amefanya nje ya mipaka ya mamlaka yake ya kisheria na kinyume cha sheria.
Pia, wanadai kuwa uamuzi huo hauna msingi wa kimantiki, unakwenda kinyume na matarajio halali ya waombaji na ya wananchi kwa ujumla, unahusisha matumizi mabaya ya mamlaka ya hiari, na unapingana na masharti ya Katiba.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo jana, mawakili wa walalamikaji waliieleza Mahakama kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32 (R.E. 2023), Rais hana mamlaka ya kuunda tume nyingine baada ya Tume ya Jaji Chande kutoa ripoti yake.
Wakili Mpale Mpoki, akisaidiana na Wakili Hekima Mwasipu, alifafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 21(1)(a) na (b) cha sheria hiyo, Rais baada ya kupokea na kuisoma ripoti ya Jaji Chande alikuwa na njia mbili tu za kufanya.
Alifafanua zaidi kuwa Rais, baada ya kupokea ripoti hiyo, alipaswa kuelekeza wale waliotajwa katika ripoti hiyo wachukuliwe hatua za kisheria.
Pia, alidai kuwa Rais hana mamlaka ya kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio ya Kijinai, bali hilo ni jukumu la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Alisisitiza kuwa DPP ndiye pekee aliyepewa mamlaka kikatiba na kisheria, kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Mashtaka, Sura ya 430 (Marejeo ya mwaka 2023), kuratibu na kusimamia upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai bila kujali sheria nyingine zozote nchini.
Hivyo, alidai kuwa kama Rais, baada ya kusoma ripoti ya Jaji Chande, anaona kuna haja ya kuchunguza zaidi, anatakiwa kumuagiza DPP kuliagiza Jeshi la Polisi kupeleleza zaidi.
Mawakili hao walidai kuwa kitendo cha Rais kuunda tume ya kuchunguza matukio hayo ni ukiukwaji wa dhahiri wa sheria na Katiba kuhusiana na mamlaka ya DPP katika masuala ya kesi za jinai.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo, walipinga madai na hoja hizo.
Pamoja na mambo mengine, Wakili Kalokola alidai kuwa alichokiunda Rais ni Tume ya Uchunguzi na si Tume ya Upelelezi, na kwamba kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi kinampa mamlaka hayo.
Wakili Kalokola alifafanua kuwa Tume ya Jaji Chande katika mapendekezo yake, hasa pendekezo la nane, ilipendekeza iundwe tume nyingine ya upelelezi, lakini Rais ameamua kuunda Tume ya Uchunguzi na kwamba hizo ni tume mbili tofauti.
Wakili Kalokola alidai kuwa kwa sababu hizo, nafuu zinazoombwa katika shauri hilo haziwezi kutolewa na akaiomba Mahakama ilitupilie mbali shauri hilo.
Pia, alisema kuwa kifungu cha 21(1) kinampa utashi mwenye mamlaka wa kuanzisha na kuteua tume nyingine pale atakapoona inafaa.
Hivyo, alisema Rais alifanya uteuzi huo akiwa na mamlaka na kwamba sheria hiyo haimzuii wala haimwekei idadi ya tume ambazo anaweza kuziunda kwa tukio hilohilo.
Uamuzi wa Mahakama
Jaji Chuma katika uamuzi wake amesema kuwa kifungu cha 3(1) cha Sheria ya Tume za Uchunguzi kinatoa maelezo ya jumla kuhusu mamlaka ya Rais kuanzisha tume na kuteua makamishna kufanya uchunguzi wa tukio lolote lenye maslahi.
Amesema Rais ana mamlaka ya kuunda tume kuchunguza matendo yote ya kijinai au mambo mengine yote ambayo ataona, kwa maoni yake, yana maslahi ya umma.
Amefafanua kuwa kifungu cha 21(1) cha sheria hiyo kinaelekeza nini kinaweza kufanyika baada ya kupokea ripoti ya tume.
Amesema kwa mujibu wa kifungu hicho, Rais baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa tume, akijiridhisha kuwa uchunguzi zaidi unapaswa kufanyika au mashtaka yafunguliwe, anaweza kumwelekeza DPP awaelekeze Polisi nini cha kufanya.
“Au kama ataona kwa maoni yake kwamba kuna njia nyingine zinaweza zikafanyika, anaweza akaamuru hatua hizo zichukuliwe,” amesema Jaji Chuma.
Jaji Chuma amesema kuwa kwa kusoma vifungu hivyo vyote havihitaji tafsiri ya sheria kuelewa maana yake, huku akifafanua kuwa kwa jinsi vifungu vilivyo, Rais hazuiliwi kuanzisha tume nyingine kwa uchunguzi zaidi.
Jaji Chuma amesema mtazamo wa walalamikaji kwamba Rais hana mamlaka na kwamba ameingilia mamlaka ya DPP unaonekana kuvutia, lakini akasema kuwa ukiangaliwa kwa undani unaacha maswali.
Amesema hoja ya Rais kuanzisha tume nyingine na kuwateua makamishna haitokani na mapendekezo ya tume ya awali, bali ni mamlaka ya kisheria yaliyo katika kifungu cha 3 cha sheria hiyo.
Pia, Jaji Chuma amesema kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha sheria hiyo, ili tume yoyote iwe na nguvu ya kisheria lazima iwe imetangazwa katika Gazeti la Serikali na itaanza kufanya kazi siku ya kutangazwa kwake.
“Kwa kifungu hicho hakuna ubishi mpaka leo, hiyo tume inayobishaniwa bado haiko kisheria kwa sababu bado haijatangazwa na makamishna wake bado hawajaapishwa kama ambavyo sheria inaelekeza,” amesema Jaji Chuma.
Ameongeza kuwa kwa muktadha huo, mawanda na majukumu yake bado hayafahamiki kwani haiwezi kuanza kazi bila hadidu za rejea ambazo ndizo zitaonyesha mawanda yake.
“Hivyo, ni mtazamo wa Mahakama kwamba kuanzisha tume ya mwaka 2025 na kuteua makamishna, Rais alifanya akiwa ndani ya mamlaka na sheria na hakuna ushahidi kwamba kwa kufanya hivyo ameingilia mamlaka ya DPP,” amesema Jaji Chuma na kusisitiza:
“Kutokana na mazingira hayo na kama ambavyo mawakili wa Serikali walieleza, malalamiko haya juu ya uhalali wa tume hiyo yameletwa kabla ya wakati.”
Amesema kwa muktadha huo, amri zilizoombwa za kutengua uamuzi wa Rais na kumzuia kufanya hivyo haziwezi kusimama.