Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama ilivyomwachia huru mganga aliyefungwa miaka 30 kwa ubakaji

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita imemwachia huru mganga wa kienyeji, Salvatory Richard, baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha bila shaka yoyote kuwa ndiye aliyewabaka wasichana wawili wa familia moja wenye umri wa miaka 11 na 16, licha ya Mahakama ya Wilaya ya Bukombe kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela kwa kila kosa.

Arusha. Mganga wa kienyeji, Salvatory Richard amenusurika kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita kubaini kuwa ushahidi uliotumika kumtia hatiani uliacha mashaka makubwa kuhusu utambulisho wake na mazingira ya matukio hayo.

Mahakama hiyo imebatilisha hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Bukombe iliyokuwa imemhukumu kwa makosa mawili ya ubakaji na kuagiza aachiliwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine ya kisheria.

Uamuzi huo ulitolewa Julai 24, 2026 na Jaji Griffin Mwakapeje, baada ya kusikiliza rufaa ya Richard aliyepinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Bukombe katika kesi ya jinai Namba 7264 ya 2026.

Awali, Richard alitiwa hatiani kwa makosa mawili ya ubakaji chini ya vifungu vya 130(1), (2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kila kosa, huku adhabu hizo zikitumikia kwa wakati mmoja.


Kesi ya msingi

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita ambapo mama wa waathiriwa hao (shahidi wa kwanza) aliiambia mahakama kuwa watoto wake walimfahamu Richard kwa kuwa alikuwa jirani yao na mganga wa jadi katika Kijiji cha Maganzo.

Amedai mmoja wa watoto hao alikuwa akimtembelea kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa macho, huku mwingine akimfahamu kutokana na ukaribu wa makazi na shughuli za biashara za familia yao.

Waathiriwa hao wawili, waliotajwa mahakamani kama shahidi wa kwanza na wa pili kwa ajili ya kulinda utambulisho wao, walitoa ushahidi kuhusu matukio hayo.

Mmoja alidai kufanyiwa vitendo vya kingono mara kwa mara kati ya Novemba 2025 na Machi 2026 wakati akimtembelea Richard kwa ajili ya matibabu, huku mwingine akidai alishawishiwa kwenda katika eneo la shughuli za tiba za jadi kwa kisingizio cha kusaidia kuandaa dawa, ambako alidai kubakwa.

Waathirika hao walidai pia kuwa Richard aliwatishia wasifichue matukio hayo, huku mmoja akidai alikuwa akimpa fedha ili asimweleze mtu yeyote.

Kwa mujibu wa mama yao, madai hayo yalibainika Machi 19, 2026 baada ya kumuuliza mmoja wa watoto wake kuhusu fedha alizokuwa akitumia shuleni. Mtoto huyo alidaiwa kumtaja Richard kama aliyekuwa akimpa fedha hizo na baadaye kufichua madai ya kufanyiwa vitendo vya kingono.

Baada ya kumhoji mtoto mwingine, ambaye pia alitoa madai kama hayo, mama huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa Kitongoji.

Utetezi

Katika utetezi wake, Richard aliiambia mahakama kuwa Novemba 2025 mama wa waathiriwa alimfuata kwa ajili ya kuwatibu watoto wake na wakakubaliana malipo ya Sh500,000, ambapo alilipwa Sh200,000 na kubaki na deni la Sh300,000.

Alidai kesi hiyo ilitungwa baada ya kuanza kudai malipo yaliyobaki.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mahakama ya Wilaya ya Bukombe ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela kwa kila kosa, adhabu zikitumikia kwa wakati mmoja.


Rufaa

Akiwa hajaridhishwa na uamuzi huo, Richard alikata rufaa akidai Mahakama ya Wilaya ilikosea kumtia hatiani wakati upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi bila kuacha shaka.

Alidai pia kuwa mahakama hiyo ilitegemea ushahidi dhaifu na wa uongo wa waathiriwa, haikutoa uzito unaostahili kwa utetezi wake na ilimtia hatiani bila ushahidi wa kutosha kuthibitisha umri wa waathiriwa, hasa kwa kuwa vyeti vya kuzaliwa havikuwasilishwa.


Uamuzi wa Mahakama

Baada ya kupitia upya ushahidi wote, Mahakama Kuu ilisema suala kuu lilikuwa kama upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka yoyote kwamba Richard ndiye aliyefanya makosa hayo.

Mahakama ilisema ingawa ushahidi wa mwathiriwa unaweza kutosha kuthibitisha kosa la kingono, unapaswa kutathminiwa kwa kuangalia uthabiti, uaminifu na namna unavyolingana na ushahidi mwingine.

Jaji alisema kulikuwa na mashaka kuhusu kuchelewa kwa waathiriwa kumtaja Richard, kwani madai yalianza Novemba 2025 lakini jina lake lilihusishwa na tuhuma hizo Machi 2026, takriban miezi minne baadaye.

Mahakama pia iliona umuhimu wa kutokuitwa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maganzo, ambaye alikuwa mtu wa kwanza kuhusishwa na malalamiko hayo na kuwa kutokuwepo kwake kuliacha pengo muhimu katika kesi ya mashtaka.

Mahakama ilisema pia kulikuwa na maswali ambayo hayakujibiwa kuhusu namna matukio hayo yalivyodaiwa kutokea kwa kipindi cha miezi kadhaa, huku Richard akiwa jirani wa familia ya waathiriwa na mmoja wao akidaiwa kumtembelea mara kwa mara kwa ajili ya matibabu.

Kwa kuzingatia upungufu huo, Mahakama imesema haijaridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake bila shaka yoyote.

Kutokana na dosari hizo, Mahakama iliruhusu rufaa ikafuta hukumu na adhabu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Bukombe na kuamuru Richard aachiliwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine ya kisheria.