Mahakama kupitia upya shauri la madai ya mahari

Simiyu. Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imeitisha jalada la shauri la madai ya mahari lililotolewa hukumu na Mahakama ya Wilaya ya Meatu Machi 14 mwaka huu, kwa ajili ya kulipitia upya.

Mahakama hiyo ya Meatu, Mkoa wa Simiyu iliamuru nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Nkoma mkoani humo, Selemani Mussa (65) kuuzwa ili kulipa deni la Sh1.1 milioni analodaiwa ili kukamilisha mahari ya kijana wake.

Uuzwaji wa nyumba hiyo ni kufidia Sh2.2 milioni walizokubaliana kabla ya ndoa ya kimila kufungwa mwaka 2019, ikiwa ni makubaliano ya ng'ombe 15 kwa thamani ya Sh150,000 kwa kila ng'ombe mmoja.

Julai 28 mwaka huu, gazeti hili liliripoti habari hiyo na kuibua mjadala kwenye maeneo mbalimbali juu ya suala hilo. Mwishoni mwa wiki Saidi Kisamba anayemuwakilisha mdaiwa Seleman Mussa alisema Mahakama imeliagiza jalada kutoka Mahakama ya wilaya ili kulifanyia kazi, hivyo baada ya kulipitia wanaweza wakatoa maelekezo mengine.

Hukumu ya shauri la madai namba 81 ya mwaka 2020 ilitolewa na hakimu F. F. Madungu ikiamuru kukamata nyumba namba 27 B ya Seleman Mussa iliyopo kijiji cha Nkoma wilayani Meatu mkoani Simiyu kufidia deni la mahari la Sh1.1 milioni kati ya Sh2.2 milioni walizokubaliana.

Akizungumza na gazeti hili, Kisamba alisema “Mahakama Kuu ina mamlaka ya kuita jalada la kesi kufanyia mapitio, baada ya hapo litarudishwa mahakama ya wilaya kwa ajili ya utekelezaji kwa amri itakayokuwa imetolewa na jaji.

Alisema alipigiwa simu kutoka Mahakama Kuu akiarifiwa hatua hiyo kwa ajili ya kumtaarifu mteja wake na kwa sasa wanasubiri uamuzi wa Mahakama.

Gazeti hili lilizungumza na Seleman Mussa ambaye ni mdaiwa katika shauri hilo alisema Septemba 4, mwaka huu alipokea taarifa kwa njia ya simu akiambiwa shauri lake lipo Mahakama Kuu.

"Niliambiwa kesi yangu imefika kule kwa hiyo nisubiri maamuzi yatakayotolewa na jaji," alisema Seleman.

Alisema amri ya mahakama ya kuuzwa kwa nyumba yake bado haijatekelezwa kwani amri hiyo ilielekeza nyumba iuzwe Julai 30, mwaka huu.

Kwa upande wake mdai Mwita Kati, alisema hadi sasa hakuna kinachoendelea katika utekelezaji wa amri ya mahakama na anatamani deni lake lilipwe kwa wakati.

"Mwandishi naomba unisaidie hela yangu nilipwe, huyu mtu tunaonana hapa kijijini lakini kunilipa hataki na amepuuza amri ya mahakama," alisema Mwita.

Tangu kuoana kwa vijana hao mwaka 2019, wamebahatika kupata mtoto mmoja na wanaendelea kuishi pamoja.

Mussa alipozungumza na gazeti hili Julai mwaka huu alisema kijana wake ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari mkoani Shinyanga alimuoa binti wa Mwita Kati (Justina), wana mtoto mmoja na maelewano mazuri.

Kijana huyo alimuoa Justina mwaka 2019, “Tulikubaliana mahari ya ng’ombe 15 kwa thamani ya Sh150,000 kila mmoja, baada ya maridhiano walikuja nyumbani wakasema wanataka mahari yote, lakini tuliwaomba wachukue nusu (Sh1.1 milioni) na inayobaki tutailipa baadaye,” alisema Mussa.

Akisimulia alisema ilipofika mwaka 2020, baba mzazi wa mwanamke huyo alianza kudai mahari iliyosalia, ndipo alipoomba muda wa kuendelea kutafuta pesa kwa kuwa hakuwa nazo wakati huo na ndipo ugomvi ulipoanzia.

“Hakuelewa, alitaka nimlipe pesa yote iliyobaki Sh1,125,000, tukaanza kutafuta muafaka katika vikao vya familia nikiomba kuongezewa muda ili nitafute pesa ya kumlipa,” alisema Mussa.

Pia, alisema walianza na vikao vya familia, viliposhindwa kupata muafaka walihamia katika ngazi ya Serikali ya kijiji hadi wakafikia hatua ya kupelekana mahakamani, huku yeye (mtuhumiwa) akikimbilia katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Meatu kutafuta suluhu.

“Novemba 10, 2022 tulifika kwa Mkuu wa Wilaya Meatu, Fauzia Hamidu, huko niliahidi kupunguza na akatushauri turudi kwenye familia tukayamalize, nilipopata pesa nilienda kupunguza deni mbele ya Serikali ya kijiji kama mashahidi,”alisema.