Nyumba hatarini kuuzwa kisa deni la mahari

Meatu. Katika hali isiyo ya kawaida, nyumba ya Seleman Mussa (65), Mkazi wa Kijiji cha Nkoma, wilayani Meatu, Mkoa wa Simiyu, iko hatiani kuuzwa kama fidia ya deni la Sh1.1 milioni, analodaiwa baada ya kutokamilisha deni la mahari ya kijana wake.

Kijana wake ambaye ni mwalimu wa shule moja ya sekondari mkoani Shinyanga, alimuoa binti wa Mwita Kati, toka mwaka 2019 kwa ndoa ya kimila, kwa makubaliano ya mahari ya ng'ombe 15.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mussa amekiri juu ya makubaliano hayo kwa kusema: “Tulikubaliana mahari ya ng'ombe 15 kwa thamani ya Sh150, 000 kila mmoja, baada ya maridhiano walikuja nyumbani wakasema wanataka mahari yote lakini tuliwaomba wachukue nusu na inayobaki tutailipa baadae," amesema Seleman.

Hata hivyo kwa mujibu wa Seleman, ilipofika mwaka 2020 baba mzazi wa binti alianza kudai mahari iliyosalia, ndipo alipoomba muda wa kuendelea kutafuta pesa ili kukamilisha deni hilo, na hapo ndipo ugomvi ulipo anzia.

"Hakuelewa alitaka nimlipe pesa yote iliyobaki Sh1.5 milioni….pale vikao vya familia viliposhindwa kupata muafaka walihamia katika ngazi ya Serikali ya kijiji hadi mahakamani. Huku mimi nikikimbilia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Meatu kutafuta Suluhu,” amesema na kuongeza;

"…nikiahidi kupunguza….na nilifanikiwa kulipa Sh500, 000 na hivyo kubaki na deni la Sh 1.1 ambayo licha ya Mkuu wa Wilaya kututaka tumalize kifamilia, wao waliendelea na kesi mahakamani na hukumu kutolewa.”

Katika shauri hilo la madai namba 81 la mwaka 2020, hukumu ilitolewa ambayo ilitaka kukamata nyumba ya Seleman namba 27B iliyopo kijiji cha Nkoma ili kufidia kiasi cha Sh1.21 na hivyo kukamilisha kiasi cha Sh2.255 milioni zilizokuwa zilipwe kama mahari.