Mahakama Kuu yasitisha mkutano mkuu wa dharura TLS

Muktasari:

  • Baraza la uongozi la wanachama wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) limetangaza kuahirishwa kwa mkutano mkuu wa dharura uliokuwa umepangwa kufanyika kesho kutokana na amri ya Mahakama.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imeagiza kusitishwa kwa mkutano mkuu wa dharura wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) uliopangwa kufanyika kesho Jumamosi, Desemba 16, 2023.

Taarifa iliyotolewa leo jioni, Desemba 15, 2023 na Rais wa TLS, Harold Sungusia  imeeleza kuwa wamepokea taarifa hiyo saa 12 jioni wakiwa katika kikao cha Baraza la Uongozi, Makao Makuu ya TLS (Wakili House).

Amesema amri hiyo imetolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam ‘Registry’ kwenye maombi madogo namba 27673 ya mwaka 2023 katika shauri la Baltazary Bosco Mahai dhidi ya TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Miongoni mwa mambo mengine, Mahakama Kuu imeamuru TLS kusitisha mkutano mkuu wa dharura uliokuwa umepangwa kufanyika kesho Desemba 16, 2023. Shauri tajwa limesikilizwa leo upande mmoja bila kushirikisha TLS,” amesema.

Sungusia amesema kwa sababu hiyo, Baraza la Uongozi limetekeleza amri hiyo kwa kusitisha mkutano huo mpaka itakapotolewa taarifa nyingine.

“Chama cha Sheria Tanganyika inawasihi wanachama wake wote kuendelea kuwa watulivu na kushikamana kwa maslahi mapana ya haki na utawala wa sheria,” amesema.