Mahakama ya Rufaa yahitimisha mgogoro wa Bakwata, Umoja wa Waislamu Arusha
Eneo la Msikiti mkuu wa Ijumaa maarufu kama 'Msikiti wa Bondeni' ambalo lilikuwa na mgogoro likiwa limezungushiwa uzio wa mabati kwa ajili ya ujenzi wa maduka. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Mahakama ya Rufaa imeitupilia mbali rufaa ya Wadhamini wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) iliyokuwa ikipinga hukumu ya Mahakama Kuu kuhusu umiliki wa Kiwanja Na. 34, Kitalu G, Eneo F jijini Arusha
Arusha. Mahakama ya Rufaa imetupilia mbali rufaa ya Wadhamini wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), iliyokuwa ikiomba kutambuliwa kuwa mmiliki halali wa Kiwanja Namba 34, Kitalu G, Eneo F jijini Arusha, ikisema taasisi hiyo haikuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yake ya umiliki.
Hukumu hiyo imetolewa Juni 29, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo walioketi Arusha ambao ni Dk Gerald Ndika, Omar Othuman Makungu na Mustafa Ismail na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Rufaa hiyo ya madai namba 508/2024 ilikuwa imekatwa na wadhamini hao wa Bakwata dhidi ya Wadhamini wa Umoja wa Waislamu Arusha, ikipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ya Machi 13, 2020 katika kesi ya ardhi namba 29/2012.
Mahakama imesema ingawa ilikubaliana na baadhi ya hoja za Bakwata kuhusu dosari za usajili wa awali wa Umoja wa Waislamu wa Arusha, dosari hizo hazikuthibitisha kuwa Bakwata ndiyo mmiliki halali wa mali hiyo inayobishaniwa.
Mgogoro huo unahusu umiliki wa kiwanja hicho ambapo Bakwata ilidai kuwa, baada ya kuanzishwa mwaka 1968 ilirithi mali zote za Msikiti wa Swahili jijini Arusha, kikiwamo kiwanja hicho.
Ilidai kuwa kupitia upekuzi wa kumbukumbu za ardhi ilibaini kwamba Umoja wa Waislamu wa Arusha ulipata hati ya umiliki wa kiwanja hicho kwa njia ya udanganyifu, wakati haukuwa na uwezo wa kisheria wa kumiliki ardhi.
Bakwata iliomba Mahakama itangaze kuwa hati ya umiliki wa Umoja wa Waislamu wa Arusha ni batili na badala yake itambuliwe kuwa ndiyo mmiliki halali wa kiwanja hicho, pamoja na kupewa amri ya kuzuia upande wa pili kuingilia matumizi ya eneo hilo.
Katika rufaa hiyo, Bakwata iliwasilisha sababu nne za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, ikidai ilikosea kumtambua Umoja wa Waislamu wa Arusha kuwa mmiliki halali wa kiwanja kinachogombaniwa.
Kwa upande wake, Umoja wa Waislamu wa Arusha ulikana madai hayo na kueleza kuwa eneo hilo lilikuwa wakfu wa Msikiti wa Swahili na Shule ya Waislamu wa Kiafrika tangu miaka ya 1960, na baadaye mali hizo zikahamishiwa kwenye umoja huo.
Mahakama ilielezwa kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto za usajili katika miaka ya nyuma, umoja huo ulisajiliwa rasmi Juni 13, 2007 na siku iliyofuata ukasajiliwa kama Bodi ya Wadhamini kwa mujibu wa sheria.
Mahakama ilibainisha kuwa usajili wa awali wa Umoja wa Waislamu wa Arusha wa mwaka 1964 haukuwa halali kwa kuwa haukutanguliwa na usajili wa chama kama sheria inavyotaka.
Hata hivyo, ilisema kasoro hiyo ilirekebishwa mwaka 2007 baada ya taasisi hiyo kusajiliwa rasmi kama chama na baadaye kuingizwa kama Bodi ya Wadhamini.
Majaji walisema pamoja na kasoro hizo, Bakwata ilibeba jukumu la kuthibitisha umiliki wake wa kiwanja hicho lakini haikuwasilisha ushahidi wa kutosha unaoonesha jinsi mali hiyo ilivyohamishiwa kwake.
Mahakama ilieleza kuwa, ushahidi wa Bakwata wa kukusanya kodi, kuomba kibali cha ujenzi na kuwa msimamizi wa masuala ya Waislamu nchini haukutosha kuthibitisha umiliki wa kisheria wa kiwanja hicho.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama ya Rufaa iliunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupilia mbali kesi ya Bakwata kwa kuwa taasisi hiyo ilishindwa kuthibitisha madai yake.
Majaji walihitimisha kuwa, ingawa baadhi ya hoja za Bakwata zilikuwa na msingi wa kisheria, hazikubadili matokeo ya shauri kwa sababu ushahidi wa umiliki haukukidhi kiwango kinachotakiwa na sheria.
Kwa kuzingatia kuwa mgogoro huo unahusisha taasisi mbili za kidini zenye uhusiano wa karibu, Mahakama ya Rufaa iliamuru kila upande ubebe gharama zake za kesi.