Mahakama yabariki mkataba bandari, yataja sababu
Mbeya. Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imetoa uamuzi mkataba wa Ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA) hauna tatizo hivyo pingamizi lililowekwa na walalamikaji halina mashiko.
Uamuzi huo umesomwa leo Alhamisi Agosti 10, 2023 na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.
Madai yaliyotolewa uamuzi na mahakama hiyo ni pamoja na: Kama ibara ya 2, 4(2)... zinakiuka Ibara namba 1, 8 na 28(1) na (3) za Katiba ya nchi na pia kama IGA ni mkataba kwa muktadha wa Sheria ya Mikataba.
Katika madai hayo mahakama imesema IGA si mkataba unaoweza kusimamiwa na sheria ya mkataba.
“Mahakama imekubali kuwa Dubai ina mamlaka ya kuingia mikataba kama hiyo. Walalamikaji hawajaeleza kama Dubai imezuiliwa kuingia mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji kwani ni suala la ushahidi,”amesema Jaji Ndunguru.
Kuhusu kama IGA inakiuka kifungu cha 64 cha Sheria ya Manunuzi, mahakama imesema; “mahakama imeikataa hoja hiyo ikisema IGA ni mkataba wa kimataifa na kwamba katika mkataba huo hakuna manunuzi yaliyofanyika. Kama walalamikaji wakiona TPA (Mamlaka ya Bandari) iliingia katika manunuzi basi walipaswa kuiunganisha TPA katika kesi hii, kwa hiyo hoja nayo Mahakama imeikataa.”
Kuhusu kama umma uliarifiwa na kupewa muda wa kutosha kutoa maoni yao mahakama imesema: “mahakama inatambua Ibara ya 63 inaipa Bunge mamlaka ya kuridhia mikataba ya kimataifa kama ilivyo IGA. Mahakama haikubaliana katika mazingira ya sasa, njia iliyotumiwa kutoa taarifa kwa mitandao ni sahihi.
“Msimamo wa mahakama ni kwamba Bunge halipaswi kuingiliwa katika utendaji wake wa kazi wa ndani, msimamo ambao umetokana na maamuzi ya kesi mbalimbali za nje.”
“Na hitimisho letu kwamba, licha ya athari za utaratibu lakini tunajizuia kuona kama upungufu huo uliathiri mkataba huo. Mahakama inajizuia kuvuka mipaka yake. Hivyo hoja hii pia mahakama imekataa,”amesema Jaji Ndunguru.
Aidha, mahakama imesema; “Tunakubali kwamba Ibara ya 20 (1) ya IGA inakiuka Sheria za Ulinzi wa Raslimali maana inataka hata mikataba itakayosainiwa ya utekelezaji wa miradi migogoro ipelekwe nje. Tumeshangaa kwa nini uandishi huo wa Ibara hiyo. Hata hivyo Ibara ya 22 ya IGA inatoa nafasi ya kufanya marekebisho hivyo kasoro ndogo hiyo haiwezi kuufanya mkataba kuwa batili.
“Kama baadhi ya ibara zinakiuka mamlaka ya hadhi ya nchi, tafsiri siyo sahihi. Kukiukwa ulinzi na usalama ni tafsiri isiyo sahihi maana Ibara ya 28 inahusu uvamizi wa kivita hivyo tunaikataa,” amesema.
“Kwa ujumla tunaamua kuwa malalamiko yaliyoletwa na walalamikaji hayana mashiko na tunayatupilia mbali. Kwa hiyo kwa uamuzi huo mkataba wa IGA ni halali,” amesema Jaji Ndunguru.
Kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 ilifunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na mawakili wanne akiwamo, Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus dhidi ya Serikali
Wadaiwa katika kesi hiyo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania, ambaye ni mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Bunge.
Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023, wanasheria hao wanapinga makubaliano hayo wakidai kuwa ni batili kwa kuwa masharti ya baadhi ya Ibara zake yanakiuka Sheria za Nchi za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi na Katiba ya Nchi.
Vile vile wanadai kwamba yanahatarisha mamlaka ya Nchi na usalama wa Taifa na kwamba yaliridhiwa na Bunge kinyume cha utaratibu bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao.
Makubaliano hayo yalisainiwa Oktoba 25, 2023 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, baada ya kupewa nguvu ya kisheria na Rais Samia Suluhu Hassan, huku Katibu Mkuu wa Wizara hiyo akishuhudia na yaliridhiwa na Bunge Juni 10, 2023.