Mahakama yajivunia mafanikio matumizi ya Tehama kufungua kesi

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria nchini.

Muktasari:

Mashauri mengi yanayofungliwa mahakamani katika ngali mbalimbali za Mahakama ya Tanzania nchni kote sasa yanasajiliwa kwa njia ya mtandao

Dar es Salaam. Mahakama ya Tanzania imejivunia mafanikio katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) hasa katika ufunguaji wa mashauri mbalimbali mahakamani kupitia mfumo wa ufunguaji mashauri kwa njia ya mtandao uitwao Judicial Stastics Dashboard System 2 (JSDS2) au e-fill-in.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa Januari 14, 2022 kuhusu maandaliz ya maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria yatakayofanyika jijini Dodoma, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma amesema kuwa mfumo huo umekuwa na mfanikio makubwa.

Profesa Juma amesema kuwa wadau wameupokea vema kwani wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kufungua mashauri mbaimbali kwa njia hiyo badala ya kulazimika kwenda mahakamani.

“Inaonekana wanachi wamekubali utaratibu wetu wa kusajili mashauri kwa njia ya mtandao ambayo imeonesha mafanikio makubwa sana, kwamba wananchi wamekubali kubadilika na sasa wengi wanatumia mtandao kusajili mashauri badala ya kujazana katika majengo ya mahakama.”, amesema Profesa Juma.

Ametoa mfano wa mashauri yaliyofunguliwa jana, Januari 13, 2022 akisema kuwa saa 5 asubuhi alitembelea mfumo wa kusajili na kutoa takwimu za mashauri kwa njia ya mtandao na kwamba amegundua kuwa asilimia kubwa ya mashauri yanafunguliwa katika Mahakama ya Tanzania katika ngazi zote yanasajiliwa kwa njia ya mtandao.

“Kwa hiyo safari ya Mahakama Mtandao imeanza na iko katika hatua nzuri. Katika muda huo wa saa 5 jana Asubuhi, kati ya mashauri 102 yaliyosajiliwa hadi muda huo, mashauri 101 au asilimia 99 yalifunguliwa kwa njia ya mtandaoni shauri moja tu ambalo lililikuwa limewasilishwa mahakamani kwa njia ya mkono.”, amesema Profesa Juma na kuongeza:

“Na kuanzia tarehe Moja hadi jana jumla ya mashauri 1717 yalkuwa yamesajiliwa katika ngazi zote za Mahakama ya Tanzania. Kati ya hizi, mashauri 1650 au asilimia 96 yalikuwa yamesajiliwa kwa njia ya mtandao na ni mashauri 67 tu ndio wananchi waliingiza mahakamani kyasajili.”