Mahakama yakataa risiti ya malipo kesi ya vigogo CWT

Muktasari:

  • Risiti ya malipo katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wawili wa Chama cha Walimu (CWT), Katibu Mkuu, Deus Seif na mweka hazina, Abubakar Allawi zimeibua utata ambao umesababisha Mahakama ya Hakimu Mkazi, mkoa wa Dar es Salaam kuzikataa.


Dar es Salaam. Risiti ya malipo katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wawili wa Chama cha Walimu (CWT), Katibu Mkuu, Deus Seif na mweka hazina, Abubakar Allawi zimeibua utata ambao umesababisha Mahakama ya Hakimu Mkazi, mkoa wa Dar es Salaam kuzikataa.

Upande wa mashtaka kupitia kwa shahidi wake wa tano katika kesi hiyo, Prosper Mzava uliiomba Mahakama hiyo izipokee kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Mzava, ambaye ni shahidi wa tano kati ya mashahidi saba ambao washatoa ushahidi mpaka sasa, alilazimika kuitwa kizimbani kutoa ushahidi kwa mara ya pili ili kuwasilisha nyaraka hiyo kama kielelezo kwa kuwa yeye ndiye aliyeziandaa, baada ya mawakili wa utetezi kuzipinga kutolewa na shahidi mwingine.

Hata hivyo, mawakili wa utetezi, Nesto Mkoba na Nashon Nkungu, waliipinga tena risiti hiyo kwa madai kuwa si halisi, bali ni kivuli.

Mawakili hao walidai kuwa shahidi pia hajafuata utaratibu wa kisheria kuwasilisha nyaraka ambazo ni kivuli pamoja na kasoro katika kuandika jina la mshtakiwa wa kwanza (Seif), kwa kuandikwa Dues badala ya Deus.

Hakimu Mkazi Mkuu, Rashid Chaungu anayesikiliza kesi hiyo, alikubaliana na hoja za pingamizi la utetezi na akakataa kuzipokea nyaraka hizo kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka katika kesi hiyo.

Hakimu Chaungu alisema kuwa shahidi huyo ndiye aliyeandaa nyaraka za malipo hayo, alitakiwa aieleze Mahakama sababu ya kuwasilisha kivuli cha nyaraka badala ya nyaraka halisi. Awali shahidi huyo ambaye alikuwa mkuu wa mafunzo wa CWT alidai kuwa aliagizwa na Seif akatoe Sh14 milioni kwa mtoa fedha (cashier), Godluck Matal ili afanye malipo ya safari ya kwenda kuangalia mpira wa miguu Cape Verde pamoja na malipo ya posho yao ya kujikimu.