Mahakama yamfutia hukumu Mfalme Zumaridi

Mwanza. Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetengua hukumu ya kifungo cha miezi 12 aliyopewa Diana Bundala maarufu kama "Mfalme Zumaridi" na wenzake wanane baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza kwa kosa la kuzuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao.

Uamuzi wa rufaa hizo zilizosajiliwa kwa namba 72/2023 (upande wa mleta maombi, Zumaridi) na namba 32/2023 iliyowasilishwa na upande wa mjibu maombi (Jamhuri) umetolewa leo Ijumaa Agosti, 25 2023, na Jaji Dk Cleoface Morris.

Katika kesi hiyo ya rufaa, upande wa mjibu maombi ulikata rufaa kupinga adhabu hiyo kuwa ndogo kwa mujibu wa sheria, huku upande wa ‘Zumaridi’ nao ukikata rufaa kupinga adhabu hiyo ukidai haikustahili kutolewa.

Jaji Morris amesema baada ya kupitia vielelezo na maelezo ya mashahidi yaliyotumika kuwatia hatiani waleta maombi katika kesi ya jinai namba 10/2023, Jamhuri ilishindwa kuthibitisha pasi na shaka kuwa waleta maombi walitenda kitendo kiovu na walikuwa na nia ovu kwa maofisa wa Serikali wanaodai kushambuliwa nyumbani kwa mhubiri huyo.

"Kwenye maelezo na vielelezo vilieleza kwamba maofisa wa Polisi, Wakili wa Serikali na Ofisa Ustawi wa Jamii walifika katika makazi ya mleta maombi namba moja (Zumaridi) wakati wakitambua kuwa mbali na kuwa makazi, pia ni eneo la ibada hivyo kwenye ushahidi hawakuthibitisha iwapo walienda kufanya kitu gani, kwa ajili ya nani na kwa nini.

"Kuna uwezekano watenda wa kitendo kile walidhani kuwa maofisa hao wa Serikali ni waumini hivyo kitendo cha kujaribu kufanya kinyume na shughuli zinazotendeka pale bila kuweka bayana kilichowapeleka haikuwa sahihi," amesema

Ameendelea, "Rufani imekubaliwa ya waleta maombi, upande wa hatia nimezitengua na adhabu nimezifuta. Amri imetolewa upande ambao haujaridhika ukate rufaa."

Kwa taarifa zaidi endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi.