Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yampa kibali askari aliyefukuzwa kazi kupinga uamuzi wa IGP

Muktasari:

  • Katika maombi hayo, ofisa huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi alikuwa akiiomba Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Moshi, kufanya mapitio ya uamuzi wa kesi zake za kinidhamu zilizosababisha afukuzwe kazi.

Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Moshi, imempa kibali aliyekuwa askari wa Jeshi la Polisi, Msalika Maagi, kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama kupinga uamuzi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) uliomfukuza kazi baada ya kuridhika kuwa ameibua hoja zenye msingi wa kisheria zinazostahili kusikilizwa.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Safina Simfukwe Julai 10, 2026, huku nakala yake ikiwekwa kwenye mfumo wa Mahakama.

Jaji amesema katika hatua ya kuomba ruhusa, wajibu wa Mahakama si kuamua iwapo mwombaji yuko sahihi au la, bali kujiridhisha kama kuna hoja zinazoweza kujadiliwa katika shauri la msingi.

Maagi aliwasilisha maombi hayo akiomba Mahakama impe ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya kimahakama kupinga uamuzi wa Februari 3, 2020 uliomfukuza kazi pamoja na uamuzi wa rufaa wa Oktoba 7, 2025 uliodumisha kufukuzwa kwake.

Katika maombi hayo dhidi ya IGP na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Maagi pia aliiomba Mahakama itoe amri ya kumlazimisha IGP kumrejesha kazini bila kupoteza haki zake kama mtumishi wa umma.

Kupitia wakili wake, mwombaji huyo alieleza kuwa aliajiriwa katika Jeshi la Polisi mwaka 2009 kabla ya kufukuzwa kazi mwaka 2020.

Alidai hakukabidhiwa nakala ya uamuzi wa kumfukuza kazi wala hakuelezwa kuhusu haki yake ya kukata rufaa, hali iliyomfanya ashindwe kutumia haki hiyo kwa wakati.

Kwa mujibu wa maelezo yake, ni mwaka 2024 ndipo alipofanikiwa kupata nakala ya uamuzi huo kupitia msaada wa askari mwenzake na baadaye akakata rufaa kwa IGP, ambayo iliamuliwa Oktoba 7, 2025.

Alidai kuwa IGP alichelewa kutoa uamuzi wa rufaa nje ya muda wa siku 60 unaotakiwa na sheria. Pia, alidai IGP alitegemea ushahidi uliokuwa umetolewa katika kesi ya jinai iliyofutwa kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Kwa mujibu wa wakili wake, kesi hiyo iliondolewa na upande wa mashtaka kutokana na ukosefu wa ushahidi, lakini bado ushahidi huohuo ulitumika katika mchakato wa kinidhamu uliopelekea kufukuzwa kwake.

Akitoa uamuzi, Jaji Simfukwe amesema katika hatua ya kuomba ruhusa ya mapitio ya kimahakama, Mahakama haitoi uamuzi kuhusu ukweli wa madai, bali huangalia kama mwombaji ana maslahi ya kutosha, ameleta maombi ndani ya muda na kama ameonyesha kuwepo kwa hoja zinazoweza kujadiliwa.

Mahakama ilibaini kuwa Maagi ana masilahi ya moja kwa moja kwa kuwa maamuzi anayoyapinga ndiyo yaliyosababisha kupoteza ajira yake.

Jaji pia alikubaliana kuwa maombi yaliwasilishwa ndani ya muda unaotakiwa kisheria, akizingatia kuwa sababu ya msingi ya shauri ilitokana na uamuzi wa rufaa uliotolewa Oktoba 7, 2025 huku maombi ya mapitio ya kimahakama yakifunguliwa Machi 12, 2026.

Kuhusu hoja za msingi, Mahakama ilisema mwombaji ameibua masuala yanayostahili kuchunguzwa, ikiwemo madai kwamba IGP hakutathimini ushahidi ipasavyo, alitegemea ushahidi uliokuwa umeachwa katika kesi ya jinai na alichelewesha kutoa uamuzi wa rufaa kinyume cha matakwa ya sheria.

Jaji Simfukwe alisema hoja hizo hazihitaji kuthibitishwa katika hatua ya kuomba ruhusa, bali zinahitaji kuonyesha kuwa zina msingi wa kujadiliwa katika shauri la mapitio ya kimahakama.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama Kuu ilikubali maombi hayo na kumpa Maagi ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya kimahakama dhidi ya IGP na AG.

Mahakama haikutoa amri yoyote kuhusu gharama za maombi hayo, hivyo kila upande utajigharamia.