Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MJEMA: Nakuunga mkono Rais wangu, ila Polisi nao wafanye haya

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu,  Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Polisi kabla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi hilo, Kurasini Jijini Dar es Salaam, Mei 28, 2026.



Takribani siku 10 zilizopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alizungumzia umuhimu wa kuimarisha Polisi Jamii na kujenga imani ya askari polisi kwa jamii, ninamuunga mkono Rais wangu kwa asilimia 100.

Lakini nia hii nzuri ya Rais Samia inaweza kutimia tu endapo Jeshi letu la Polisi litajirudi na kutafakari uhusiano baina yake na raia wema kwani ni moja ya taasisi ya Serikali ambayo kama ni alama katika mitihani, ipo chini ya asilimia 12.

Kwa hiyo Rais Samia kama Rais na Amiri Jeshi mkuu kuona umuhimu wa Serikali kuimarisha Polisi Jamii ikiwa ni  njia ya kuboresha ulinzi na usalama kupitia ushirikiano na wananchi ni jambo jema sana na lenye dhamira njema kwa nchi.

Kauli ya Rais Samia aliitoa Mei 28,2026 akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya maofisa na wakaguzi wasaidizi wa Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam.

Rais alisema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake ya mwaka 2000, ulinzi na usalama ni jukumu la kila Mtanzania, na Polisi Jamii ni nguzo muhimu katika kutekeleza wajibu huo kwa ufanisi mkubwa.

Alitumia fursa ya kusanyiko hilo kutoa wito kwa Jeshi la Polisi kujenga imani kwa jamii ili kuhakikisha kuwa linakuwa karibu zaidi na wananchi kwenye kubaini, kukabiliana na kuzuia uhalifu hukohuko kwenye mitaa yetu kabla haujatokea.

Pamoja na dhamira hii njema, kwenye ukweli tuuseme kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu na ukweli una sifa moja, hata kama ukiukataa, hauwezi kugeuka kuwa uongo, jeshi letu limepoteza imani kwa wananchi walio wengi.

Kuna mambo machache ambayo nitayasema hapa ili Jeshi letu la Polisi kama lina dhamira kweli ya kujenga imani kwa wananchi ni lazima iyafanye ili kulirejesha katika misingi ile waliyoiacha Inspekta Jenerali (IGP) mstaafu,  Said Mwema.

Moja ambalo pengine limelifanya Jeshi letu la Polisi kuchukiwa na wananchi tofauti na kipindi cha IGP Said Mwema, ni kutekeleza majukumu yake nje kabisa ya Katiba ya Tanzania, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na PGO.

Sheria mama ya ukamataji ni CPA Sura ya 20 kama ilivyorejewa mwaka 2023 Japo kuna zingine zinazoendana na hiyo ikiwa ni pamoja na Katiba ya Nchi na Kanuni za Jeshi la Polisi (PGO) na zimeainisha kinagaubaga haki za mshukiwa wa uhalifu.

Miongoni mwa haki hizo ni haki ya kuambiwa kuwa uko chini ya ulinzi, haki ya kumtambua anayekukamata, haki ya kuambiwa sababu ya kukamatwa kwako, haki ya Kutotoa maelezo yoyote na haki ya  kutokulazimishwa kukiri kosa lolote.

Lakini haki ya kudhaniwa hujatenda kosa lolote hadi pale utakapotiwa hatiani na mahakama na haki ya kukamatwa kwa kufuata utaratibu na kujulishwa pia haki ya kuwasiliana na wakili wako, ndugu au jamaa uwapo mikononi mwa polisi.

Mbali na haki hizo, lakini kuna haki ya kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 ambayo ni ya msingi ya kisheria na kikatiba inayomlinda mtu anayeshikiliwa na vyombo vya dola ili kuzuia kuwekwa kizuizini kiholela bila kufunguliwa mashtaka.

Si tunakubali msema kweli ni mpenzi wa Mungu?, tujiulize Polisi wetu wanatenda majukumu yao kwa kuzingatia haki hizo za kisheria? Au siku hizi tunashuhudia watu wakikamatwa kininja, wamejiziba sura na bila hata kujitambulisha.

Lakini leo hii tunashuhudia washukiwa wa uhalifu wakikamatwa kama vile utekaji licha ya kwamba wanajitambulisha kama Polisi, wamebeba silaha za kivita na pingu, lakini ndugu wanahangaika weee! Kujua ni wapi ndugu yao amepelekwa.

Haya wala hayahitaji mabadiliko ya kisheria kwa sababu tayari sheria zipo ni kubadili tu mitizamo (mind set) kutoka Jeshi la maguvu na kuwa Jeshi linaloheshimu utawala wa sheria muone kama hamtapendwa na wananchi.

Jambo lingine ambalo limejenga chuki kubwa ni masuala ya utekaji wa raia, kupotezwa kwa watu (enforced disappearance) na mauaji na namna jeshi letu linavyochunguza, kuyazungumzia na kuyatolea mrejesho wa uchunguzi.

Ukitazama sana jambo hili, Polisi hawawezi kujitenga nalo kwa sababu hakuna raia anayemiliki bunduki ya Sub Machine Gun (SMG) au Avtomat Kalashnikova (AK-47) ili ihesabiwe kuna watu wanatekana, hizi zinamilikiwa na vyombo vyetu vya dola.

Sasa ili wananchi wasilihusishe Jeshi letu la Polisi na mambo hayo ni lazima warudi kwenye mstari kwa kusimamia sheria za nchi ili wananchi sasa wajue kabisa huu ni ukamataji wa Polisi, na huu sio ukamataji wao na wachukue hatua.

Nakubaliana na Rais Samia kuwa Polisi Jamii ni nguzo muhimu katika kutekeleza wajibu wa ulinzi na usalama kwa ufanisi mkubwa, lakini kama polisi wasiporudi kwenye mstari nina wasiwasi huko tunapokwenda yanaweza kutokea maafa.

Ndio, kwa sababu jamii inaishi kwa hofu kwa hiyo iko siku wananchi wataamua kukabiliana wenyewe na watekaji kumbe ni polisi kukatokea maafa, mambo ambayo tusipochukua hatua sasa huenda huko mbele tunapokwenda ni giza nene.

Lakini jambo lingine ambalo limeweka mwanya mkubwa (gap) kati ya raia na Jeshi la Polisi ni namna linavyoshughulikia migogoro ya kisiasa, katika nchi ambayo Katiba inatambua kuwa inaendeshwa chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Ndio maana kuna dhana hasi inajengeka kuwa Polisi ni CCM B na huwezi kuwazuia wananchi kujenga hisia hizo kwani kuna kauli zinatolewa na baadhi ya viongozi au wanachama wa CCM sio kosa, lakini kauli hiyo ikitolewa na mpinzani ni kosa.

Lakini matukio ya Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi na siku zilizofuata licha ya kwamba Tume ya Jaji Chande iliyochunguza ghasia hizo imesema nguvu iliyotumika ilikuwa kwa mujibu wa sheria, bado ni kama ilitonesha jeraha.

Haya mambo pamoja na mengine ambayo wananchi wana dukuduku nayo ndio ambayo yamelifikisha jeshi letu la Polisi hapo lilipo na ndio maana nimetangulia kusema pamoja na dhamira njema ya Rais, kuna mambo ya polisi wenyewe wanatakiwa wayafanye tena mengine wala hayahitaji mabadiliko ya sheria.

Tunatamani uhusiano kati ya Polisi na raia urudi kama zamani enzi za IGP Mwema kwa sababu tumeishi vizuri na Polisi huku mitaani bila tatizo lolote kuliko hivi sasa ambapo baadhi ya wananchi wanaona urafiki wao na polisi ni wa paka na panya.

Wala hili la kuzorota kwa mahusiano kati ya polisi na raia sio mimi pekee nimelisema, hata aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene aliyehudumu kwa siku 52 tu aliwahi kugusia suala hili.

Simbachawene alitolea mfano wa Polisi akipata ajali sasa hivi badala ya wananchi kumsaidia, wao wanashangilia. Hili linajitokeza hata Polisi wetu wanapopata madhila ikiwamo kifo wapo wananchi wanashangilia kupitia mitandao ya kijamii.

Hata kifungu cha 3.1 cha Muhtasari wa Tume ya Haki Jinai kinasema wazi kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya Jeshi la Polisi na ikayataja malalamiko hayo.

Malalamiko hayo yanahusu kushindwa kuzuia uhalifu (kama ilivyo kwenye utekaji), matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi na vitendo vya rushwa na mali za watuhumiwa kupotea mikononi mwa polisi, hali hiyo inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa.

Kwa hiyo ili wananchi watoe ushirikiano ni lazima changamoto nilizozieleza zipatiwe ufumbuzi wa haraka na kulifanya Jeshi letu la Polisi liwe kipenzi cha wananchi katika kufanikisha ulinzi wa raia na mali zao na usalama wao.

Lakini mabadiliko haya yanahitaji utashi wa kisiasa wa viongozi wetu ili mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai yatekelezwe kwa ukamilifu, lakini kunahitajika mabadiliko ya Polisi wetu wenyewe kifikra na kiweledi.

Kwa hiyo mchawi wa ushirikiano kati ya raia na Polisi ni polisi wenyewe. Ukamataji wao ufuate sheria, watu washikiliwe kwa mujibu wa sheria waone kama hawatapendwa na kupewa ushirikiano na Polisi Jamii itafanikiwa kwa asilimia 100.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900