Polisi Jamii walivyofungua uchumi wa saa 24 Kinondoni
Askari wa Polisi Jamii wakishiriki mkutano wa pamoja na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ulioandaliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, jijini Dar es Salaam, katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Jumamosi Mei 9, 2026.
Muktasari:
- Mfumo wa walinzi shirikishi ulioanzishwa kusaidia Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam sasa unatajwa kubadili sura ya usalama Kinondoni, ukifungua biashara za usiku na kurejesha imani ya wananchi kufanya kazi bila hofu.
Dar es Salaam. Manispaa ya Kinondoni, Wilaya ya Kaskazini mwa jiji la Dar es Salaam iliyoaminika kwa matukio ya kihalifu miaka mingi sasa hofu hiyo haipo tena baada ya kuimarishwa kwa mtandao wa Polisi Jamii uliosaidia kupunguza matukio ya uporaji, wizi wa mitaani na hofu ya wananchi kufanya shughuli zao nyakati za usiku.
Mabadiliko hayo yamejadiliwa leo Mei 9, 2026 katika warsha iliyowakutanisha jumla ya Polisi Jamii 624 na askari polisi 100 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ulinzi na usalama katika ukanda huo wa Kaskazini mwa jiji.
Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wakishiriki mkutano wa pamoja wa Polisi Jamii na Jeshi la Polisi ulioandaliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi, katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Jumamosi Mei 9, 2026.
Kwa miaka mingi maeneo ya Kigogo, Tandale, Mzimuni, Mikoroshoni na Bonde la Mpunga yalitajwa mara kwa mara katika simulizi za uhalifu wa mitaani, uporaji wa simu, vibaka wa mchana na hofu ya wananchi kutembea nyakati za usiku.
Lakini sasa hali inaanza kubadilika huku biashara za usiku, usafiri wa bodaboda, mama lishe, baa, maduka na shughuli nyingine za kiuchumi zikiongezeka hadi nyakati za alfajiri katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo yenye zaidi ya wakazi milioni moja.
Akizungumzia juhudi zilizoleta hali hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Saad Mtambule amesema usalama uliopo sasa ni matokeo ya ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, Polisi Jamii na wananchi wenyewe waliokubali kushiriki moja kwa moja katika ulinzi wa maeneo yao.
“Mifano ya mataifa yaliyopoteza amani inaonesha jinsi amani ikitoweka ni vigumu kuirejesha. Pamoja na changamoto mbalimbali wilaya yetu ya Kinondoni imeendelea kuwa salama wakati wote,” amesema Mtambule.
Askari wa Polisi Jamii wakishiriki mkutano wa pamoja na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ulioandaliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Jumamosi Mei 9, 2026.
DC huyo amesema kuimarika kwa hali ya usalama kumeruhusu wananchi kufanya shughuli za kiuchumi kwa muda mrefu zaidi tofauti na miaka ya nyuma ambapo baadhi ya maeneo yalitawaliwa na hofu ya uhalifu wa usiku na hata mchana.
“Aidha, kwa sasa watu wanafanyakazi masaa 24. Hii ni kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Polisi Jamii katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama muda wote,” amesema.
Katika kile kinachoonekana kuwa mkakati mpya wa kushusha vita ya uhalifu mpaka ngazi ya mtaa, Mtambule amesema Serikali haitaki tena kila tukio dogo la uhalifu kusubiri nguvu ya makamanda wakubwa wa polisi badala yake jamii yenyewe inapaswa kuwa mstari wa mbele kupitia mfumo wa Polisi Jamii.
“Hivi kweli matukio ya mtu anayekwapua nguo, anayeiba kuku hapo mtaani yanamhitaji RPC? Hapana, hii ndiyo kazi ya Polisi Jamii. Tuyaibue hayo na kuwakamata wahusika kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Hata hivyo, amesema maeneo ya Kigogo, Tandale, Mzimuni, Mikoroshoni, Makangira, Bonde la Mpunga, Bunju, Madale, Manyanya na Hananasifu bado yanaendelea kutajwa katika taarifa za viashiria vya uhalifu hivyo yanahitaji kuongezewa nguvu ya ulinzi shirikishi ili kuzuia kurudi kwa mazingira ya zamani ya hofu.
Msisitizo wa maadili kwa walinzi Shirikishi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi amesema mafanikio yanayoonekana sasa hayawezi kutenganishwa na mchango wa Polisi Jamii ambao wamekuwa sehemu ya mtandao wa kiusalama unaosaidia Jeshi la Polisi kufika kwa haraka katika maeneo ya wananchi.
“Katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao, Jeshi la Polisi linatambua mchango wa wakaguzi kata uliowezesha amani na utulivu katika mitaa yote zaidi ya 106 ya wilaya ya Kinondoni,” amesema Kitinkwi.
Kamanda huyo amesema Polisi Jamii wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kushirikiana moja kwa moja na Jeshi la Polisi ili kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza kutoka kwa wananchi.
“Jukumu letu ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Lakini tunataka mfumo huu ufanye kazi kwa weledi, uaminifu na kwa kufuata sheria,” amesema.
Katika kuonesha ukubwa wa operesheni hiyo ya ulinzi shirikishi, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamishina Msaidizi Ali Wendo amesema jumla ya Polisi Jamii 624 kutoka Kawe, Mabwepande, Kimara, Magomeni na maeneo mengine walikutana kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha usalama katika ukanda wa Kaskazini mwa Dar es Salaam.
“Lengo ni kuunganisha nguvu ya wananchi na Jeshi la Polisi ili kukabiliana na uhalifu kabla haujaleta madhara makubwa kwa jamii,” amesema Wendo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Uhamasishaji Polisi Jamii Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Emmanuel Malila amesema mfumo huo umeanzishwa kwa lengo la kuifanya jamii yenyewe kuwa sehemu ya ulinzi wa maeneo yao badala ya kuiachia kazi hiyo Jeshi la Polisi pekee.
“Sisi kama Polisi Jamii wajibu wetu tunaelekezwa kutenda kazi kwa uaminifu. Tunapokamata mtu tunapaswa kuwa na RB ya kukamatia na kuwafikisha polisi tunaowakamata,” amesema.
Malila ameonya kuwa baadhi ya watu wanaotumia jina la Polisi Jamii vibaya kwa kufanya ukamataji holela au operesheni zisizo rasmi wanaharibu taswira ya mfumo huo na kusisitiza kuwa kila operesheni lazima ifanyike kwa ushirikiano na Polisi Kata.
Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Kinondoni, Lazarous Mwakiposa amesema mfumo huo umeleta mapinduzi makubwa kwa kusogeza huduma za kiusalama karibu zaidi na wananchi.
“Mfumo huu umetuletea huduma za polisi kwenye mitaa. Sisi wenyeviti wa mitaa tunawategemea sana Polisi katika jukumu letu la ulinzi na usalama,” amesema.
Amesema mbali na kusaidia usalama, mfumo huo pia umekuwa sehemu ya kuwajengea vijana nidhamu, mafunzo na ushiriki wa moja kwa moja katika kulinda maeneo yao badala ya kujiingiza katika vitendo vya kihalifu.
Katika hatua nyingine, mwakilishi wa wamiliki wa makampuni ya ulinzi Kanda ya Dar es Salaam, Julieth Mathayo amesema ukuaji wa sekta binafsi ya ulinzi ni ishara kuwa jamii imeanza kutambua umuhimu wa uwekezaji katika usalama.
“Mwaka 1980 kulikuwa na makampuni manne tu ya ulinzi lakini leo yapo zaidi ya 2000 nchini. Hii inaonesha namna ambavyo jamii imeamua kushiriki moja kwa moja katika mapambano dhidi ya uhalifu,” amesema.