Mahakama yamrejesha kazini ofisa Bandari Z’bar

Muktasari:
Ofisa huyo alifukuzwa kazi Februari 4,2010, kutokana na hasara ya wizi uliotolea katika eneo lake la kazi, Agosti 11,2009 usiku
Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imemrejesha kazini ofisa wa Shirika la Bandari Zanzibar, Juma Issa Ramadhani, aliyekuwa amefukuzwa kwa tuhuma za wizi katika eneo lake la kazi.
Pia, Mahakama imeamuru alipwe stahiki zake zote baada ya kujiridhisha kuwa alifukuzwa kazi isivyo halali.
Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa yake, Sivangilwa Mwangesi (kwa sasa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi), aliyekuwa kiongozi wa jopo hilo, Winfrida Korosso na Mary Levira.
Katika rufaa hiyo, Ramadhani alikuwa akipinga uamuzi wa Mahakama ya Kazi Zanzibar, Vuga iliyotupilia mbali malalamiko yake dhidi ya mwajiri wake, kumfukuza kazi isivyo halali.
Ramadhani alifukuzwa kazi Februari 4,2010, kutokana na hasara ya wizi uliotolea katika eneo lake la kazi, Agosti 11,2009 usiku, baada ya kushindwa kufika kazini, wakati ilikuwa zamu yake, kwa maelezo kuwa alikuwa mgonjwa bila kumtaarifu mkuu wake wa kazi.
Kutokana na hasara hiyo alitakiwa kutoa maelezo, lakini hakufanya hivyo ndani ya muda ulioelezwa.
Hivyo, Februari 5, 2010 alipewa barua ya kuachishwa kazi, iliyoeleza kwamba bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo, imeamua kumwachisha kazi kuanzia Februari 4,2010.
Kutokana na hatua hiyo Ramadhani aliwasilisha malamiko yake Mahakama ya Kazi akipinga uamuzi wa mwajiri wake akidai kuwa sababu iliyotolewa sio halali na ya haki.
Hivyo, aliiomba Mahakama hiyo iamuru arejeshwe kazini na kulipwa stahiki zake zote.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Mkusa Isaac Sepetu baada ya kutathmini ushahidi wote uliowasilishwa kwake, aliridhika kwa kiwango cha uwelekeo kwamba kuachishwa kazi wa mlalamikaji kulifanyika kwa haki.
Ramadhani hakuridhika na uamuzi huo, ndipo akakata rufaa Mahakama ya Rufani, iliyosikilizwa Desemba 8, 2020, akiwakilishwa na mawakili Salum Bushiri Khamisi na Haji Suleima Tetere, huku, Shirika likiwakilishwa na wakili Rajabu Abdallah Rajabu, ambaye aliunga mkono rufaa hiyo.
Mahakama ya Rufani katika hukumu yake hiyo iliyotolewa Desemba 16, mwaka jana, imekubaliana na hoja za mawakili wa pande zote kuwa kuachishwa kazi kwa mrufani hakukuwa kwa haki na hakukufuata taratibu za kisheria.
Mahakama hiyo imesema kwamba kifungu cha 11(5) cha Sheria ya Uwekezaji kilichotumiwa na bodi kumwachisha kazi mrufani hakihusiki kwa vyovyote na uamuzi huo.
Imefafanua kwamba kuachishwa kazi kwa mfanyakazi kwa namna yoyote, sheria inayotumika ni Kanuni za Watumishi, kwa minajili ya kesi hiyo ni Kanuni za Watumishi wa Shirika la Bandari Zanzibar.
Hata hivyo, imesema wakati Ramadhani akiachishwa kazi mwaka 2010 kanuni hizo hazikuwepo, lakini haziipi bodi mamlaka ya kutangaza kupunguzwa kwa mfanyakazi.
Badala yake Mahakama hiyo imesema sababu ambazo mwajiri anaweza kutangaza kumpunguza mfanyakazi zinatolewa chini ya masharti ya kifungu cha 121(2) cha Sheria ya Ajira, Namba 11 ya mwaka 2005.
Hivyo, Mahakama hiyo inasema kwa kuwa masharti ya kifungu hicho hayakuzingatiwa, hakuna namna ambayo uamuzi huo unaendelea kusimama.
Pia, Mahakama hiyo imekubaliana na hoja ya rufaa kwamba jaji alikosea kuamua mgogoro huo bila kuainisha masuala au hoja zinazobishaniwa.
Inasema kuwa hilo ni takwa la kisheria katika kuamua mashauri ya madai, kwa kuwa ndio huiongoza Mahakama kufikia uamuzi wa masuala ya kisheria na ya kiushahidi, isipokuwa tu pale watakapokubaliana kuachana na hitaji hilo, makubaliano ambayo hayakuwepo. Hivyo, imesema inadhani kama jaji huyo angeandaa hoja hizo kabla ya kuamua shauri hilo, hapana shaka asingeamua kuwa kuachishwa kazi kwa mrufani kulifanywa kwa haki kwa kuwa uamuzi huo haukuzingatia masharti ya kisheria.
“Kwa kuzingatia hayo, tuliyoyasisitiza hapo juu, tunakubaliana na maombi ya mawakili wa pande zote kutengua uamuzi wa Mahakama ya awali na hali kadhalika tunatupilia mbali amri zilizotokana nao. Kwa hiyo badala yake tunaamuru mrufani kurejeshwa kwenye ajira yake,” inasomeka hukumu hiyo.
“Kwa nyongeza yake anaapaswa kulipwa haki zinazohusiana na stahiki za kurejeshwa kwake kazini baada ya kupunguza kiasi alichokuwa tayari ameshalipwa kuhusiana na kuachishwa kazi ambako tumeamua kwamba si halali.”