Mahakama yamwachia aliyeshtakiwa kwa mauaji ya mtoto
Muktasari:
- Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama ilihitimisha kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa na mashaka makubwa na haukuweza kufikia kiwango cha kuthibitisha hatia ya mshtakiwa bila shaka yoyote na hivyo kumwachia huru mshtakiwa huyo.
Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo wa Bukoba imemwachia huru Malecha Mashala maarufu kwa jina la Ngosha, aliyeshtakiwa kwa mauaji ya mtoto, Iranyishyuye Stephano, ambaye mwili wake ulikutwa shambani akiwa amechinjwa.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kuridhika kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukufikia kiwango kinachotakiwa kisheria cha kuthibitisha hatia bila shaka yoyote.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Immaculata Banzi aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo.
Mauaji hayo yalidaiwa kutokea Machi 16, 2024 katika Kijiji cha Ngando, wilayani Missenyi, Mkoa wa Kagera.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa alimuua mtoto huyo kwa kutumia kitu chenye ncha kali, jambo ambalo alilikanusha tangu mwanzo wa kesi.
Upande wa mashtaka, uliowakilishwa na uliwasilisha mashahidi wanne na vielelezo vitatu kuthibitisha shtaka hilo huku mshtakiwa akiwa shahidi pekee wa utetezi.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Banzi alisema suala kuu lililokuwa mbele ya mahakama ni iwapo upande wa mashtaka umefanikiwa kuthibitisha kosa la mauaji dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote, kama inavyotakiwa katika sheria za jinai.
Mahakama ilisema kweli mtoto huyo alikufa kifo kisicho cha kawaida, jambo lililothibitishwa na ushahidi wa kitabibu uliotolewa na shahidi wa kwanza, ambaye alifanya uchunguzi mwili wa marehemu na kubaini kuwa chanzo cha kifo ni kupoteza damu nyingi kufuatia jeraha kubwa shingoni.
Hata hivyo, changamoto kubwa ilijitokeza katika kipengele cha pili cha kuthibitisha kama ni mshtakiwa aliyesababisha kifo hicho.
Shahidi wa pili ambaye ni baba wa marehemu, alidai siku ya tukio alirudi nyumbani kwake usiku saa nne lakini hakumkuta mwanaye (marehemu) na alipomuuliza mkewe ambaye kwa wakati huo alikuwa mjamzito, alimjulisha amemtuma kwa mshtakiwa ampelekee sabuni.
Alidai alimtuma mkewe kwenda kumtafuta binti yake lakini hakumpata, ndipo aliamua kwenda na majirani na walipomuuliza mshitakiwa alipo mtoto huyo, alijibu kwa hasira akiuliza baisikeli yake ilipo.
Alidai mshtakiwa alianza kupiga panga chini kwa hasira.
Alidai baadaye, kwa msaada wa majirani, walimkamata mshtakiwa ambaye kwa mujibu wa shahidi huyo, mshtakiwa alikiri kuwa amemuua mtoto huyo na kuwaongoza hadi eneo la tukio ambako mwili ulikutwa shambani.
Shahidi wa tatu, ambaye ni kiongozi wa eneo hilo, alithibitisha kupokea taarifa za kupotea kwa mtoto na kufika eneo la tukio.
Alidai alipofika, alikuta tayari taarifa za kifo zimesambaa na mshtakiwa akihusishwa moja kwa moja na tukio hilo. Hata hivyo, maelezo yake yalionyesha kuwepo kwa mkanganyiko kuhusu wakati halisi wa kupatikana kwa mwili na iwapo mshtakiwa ndiye aliyewaongoza watu hadi eneo hilo.
Shahidi wa kwanza aliyefanyia mwili uchunguzi, alieleza mahakama kuwa uchunguzi wa mwili wa marehemu ulionyesha alikatwa shingoni kwa kitu chenye ncha kali, hali iliyosababisha kupoteza damu nyingi hadi kifo chake.
Shahidi wa nne ambaye ni askari polisi Morris alieleza jinsi alivyorekodi maelezo ya onyo kutoka kwa mshtakiwa, ambayo yalitumika kama kielelezo mahakamani ambapo katika maelezo hayo, mshtakiwa alidaiwa kukiri kuhusika na mauaji hayo.
Hata hivyo, upande wa utetezi ulipinga uhalali wa maelezo hayo ukidai yalitolewa chini ya shinikizo baada ya mshtakiwa kupigwa na kujeruhiwa kabla ya kufikishwa kituoni.
Katika utetezi wake, mshtakiwa alikana kuhusika na mauaji hayo na kuwa siku ya tukio alikuwa akifanya kazi shambani kwake kabla ya kundi la watu kuvamia na kuanza kumpiga, wakimlazimisha kukiri kosa ambalo hakulifanya.
Uamuzi Jaji
Jaji Banzi amesema mahakama ilibaini kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaomuonyesha mshtakiwa akitenda kosa hilo, hivyo upande wa mashtaka ulitegemea ushahidi wa mazingira pamoja na madai ya kuwepo kwa maungamo ya mshtakiwa.
Katika uchambuzi wake, mahakama ilieleza kuwa ushahidi wa mazingira unahitaji kuwa thabiti na usioacha nafasi ya uwezekano mwingine wowote isipokuwa hatia ya mshtakiwa.
Alieleza katika kesi hiyo, ushahidi uliotolewa ulikuwa na mapungufu makubwa, miongoni mwa mapungufu hayo ni kauli ya shahidi muhimu, Ismail Ramadhan, ambaye alidai kumuona marehemu akiwa na mshtakiwa kabla ya tukio, lakini hakufika mahakamani kutoa ushahidi wake badala yake, kauli yake ilipokelewa kama kielelezo, jambo ambalo mahakama ilisema haliwezi kupewa uzito mkubwa kwa kuwa hakupata nafasi ya kuhojiwa.
Mahakama pia ilieleza kuwa ushahidi wa kuwa mshtakiwa alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu haukuthibitishwa kikamilifu, kwani kulikuwa na uwezekano wa watu wengine kuwepo katika eneo la tukio.
Aidha, jaji alibainisha kuwa kulikuwa na utata mkubwa katika ushahidi wa wa upande wa mashtaka, hususan kuhusu tukio la mshtakiwa kudaiwa kuwaongoza hadi mahali mwili wa marehemu ulipopatikana, pamoja na suala la panga lililodaiwa kutumika katika mauaji.
Mahakama pia ilieleza kuwa kulikuwa na ushahidi muhimu ambao haukuwasilishwa, ikiwemo wa mama wa marehemu ambaye angeweza kuthibitisha kama kweli mtoto alitumwa kwa mshtakiwa, jambo ambalo lingeimarisha hoja ya upande wa mashtaka.
Kutokana na kukosekana kwa ushahidi huo muhimu, mahakama ilisema inalazimika kutoa hitimisho lisilo na faida kwa upande wa mashtaka na kumuachia huru mshtakiwa huyo.