Mahakama yatengua uamuzi wa Fatma Karume kufutiwa uwakili
Muktasari:
- Kwa ufupi: Mahakama Kuu imetengua uamuzi wa Kamati ya Mawakili wa kumfuta wakili Fatma Karume baada ya kukubaliana na rufaa yake.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu imetengua uamuzi wa Kamati ya Mawakili iliyomfuta Fatma Karume katika orodha ya mawakili nchini.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Juni 21, 2021 na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, Issa Maige (Kiongozi wa jopo), Jaji Deo John Nangela na Jaji Edwin Kakolaki, kufuatia rufaa aliyoikata Karume akipinga uamuzi huo wa Kamati ya Mawakili.
Karume alifutiwa uwakili na kamati hiyo Septemba 23, 2020 kufuatia malalamiko yaliyowasilihwa kwake na Adelardus Kilangi, akimtuhumu kukiuka maadili ya taaluma kwa kutumia lugha ya kumdhalilisha wakati akiwasili hoja za maandishi katika shauri alilokuwa akimwakilisha mteja wake Ado Shaibu.
Hata hivyo, hakukubaliana na uamuzi huo badala yake kupitia kwa wakili wake Peter Kibadala alikata rufaa Mahakama Kuu Masjala Kuu akiwasilisha kadhaaa za kupinga uamuzi huo.
Mahakama kuu katika uamuzi wake imekubaliana na sababu moja tu ya rufaa hiyo ambayo imetosha kutengua uamuzi wa kamati hiyo.
Katika sababu hiyo ambayo Mahakama Kuu imekubaliana nayo, Karume kupitia kwa wakili wake alidai kuwa kamati hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza malalamiko ya Profesa Kilangi kwa kuwa ilikuwa inakiuka uamuzi wa Jaji Kiongozi.
Awali Jaji Kiongozi alimsimamisha Karume uwakili kwa muda kufuatia malalamiko hayo yaliyowasilishwa na mawakili wa Serikali katika kesi waliyokuwa wakimwakilisha Profesa Kilangi na Dk. John Pombe Magufuli,
Katika kesi hiyo, Karume alikuwa akimwakilisha Shaibu aliyekuwa akipinga uteuzi wa Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.