Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yatoa amri mpya mashahidi kesi ya Tundu Lissu

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akiwa katika chumba cha Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Mahakama imeamuru mashahidi kutoa ushahidi mahakamani kwa kificho (bila kuonekana), huku ikizuia majina yao kutajwa wala kuwekwa wazi taarifa zinazoweza kufanya wakatambulika.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetoa amri ya ulinzi dhidi ya mashahidi wa Jamhuri ambao ni raia wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Katika uamuzi uliotolewa leo, Agosti 4, 2025, na Jaji Hussein Mtembwa, Mahakama imeamuru mashahidi hao kutoa ushahidi mahakamani kwa kificho (bila kuonekana), huku ikizuia majina yao kutajwa wala kuwekwa wazi taarifa zinazoweza kufanya wakatambulika.

Vilevile, imepiga marufuku kusambazwa taarifa zinazoweza kufanya majina ya mashahidi hao kufahamika ama kwa ndugu, marafiki au watu wao wa karibu, pia kuchapishwa au kutangazwa na vyombo vya habari.

Mahakama imefikia uamuzi huo kutokana na maombi ya Jamhuri iliyoomba ulinzi dhidi ya mashahidi wake chini ya Kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na Marekebisho ya mwaka 2025.

Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilikofunguliwa ili kukamilisha taratibu za awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza na kuamua shauri hilo.

Baada ya upelelezi kukamilika na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuridhika na ushahidi uliopatikana, alifungua shauri la maombi ya ulinzi wa mashahidi wa Jamhuri katika kesi hiyo kabla ya mwenendo wa uhamishaji kesi kutoka Mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu.

Shauri hilo lililosikilizwa upande mmoja kwa mujibu wa sheria kuhusu maombi ya ulinzi wa mashahidi, DPP aliomba amri ya ulinzi wa mashahidi ambao ni raia kwa ajili ya usalama wao.

Maombi hayo yaliambatanishwa na kiapo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Amini Mahamba.

Jamhuri imeomba ulinzi wa mashahidi hao, ikieleza ni kutokana na asili ya kesi hiyo kwamba, mshtakiwa anakabiliwa na shtaka kubwa. Pia kwa sababu mshtakiwa ana wafuasi wengi ndani na nje ya nchi.

Imeeleza kulingana na taarifa ambazo ACP Mahamba alizipata katika upelelezi, mashahidi hao wamekuwa wakitishwa na watu wa karibu wa mshtakiwa ili wasifike mahakamani kutoa ushahidi.

Kutokana na maelezo hayo, Jamhuri ilieleza hali hiyo inaweza kuhatarisha usalama wao.

Mbali ya hayo, Jamhuri ilidai kuna Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi zilizotolewa Julai 2025 ambazo zinaruhusu ulinzi kwa mashahidi katika mazingira hayo.


Uamuzi wa Mahakama

Akitoa uamuzi leo, Jaji Mtembwa amesema alichokiona ni kweli kosa analokabiliwa nalo mshtakiwa ni kati ya makosa makubwa na mashahidi wanaotarajiwa, kwa mujibu wa kiapo cha ACP Mahamba, wanatishwa.

Amesema katika hali hiyo, Mahakama inapaswa kuangalia sheria inasemaje.

Amebainisha kuwa, sheria inaruhusu kuwalinda mashahidi na mtoa taarifa, hasa pale ambapo yeye au familia yake iko katika hatari ya kudhuriwa. Pia inazingatia kuwa mshtakiwa ana haki ya kumuona shahidi na kumhoji.

Vilevile, Jaji Mtembwa amesema Mahakama ina wajibu wa kulinganisha haki hizo mbili kwa uwiano kwa lengo la kutenda haki.

Hivyo, amesema kwa kuzingatia yote hayo, anayakubali maombi ya ulinzi wa mashahidi ambao ni raia, kuficha majina na taarifa zozote zinazowahusu zinazoweza kufanya watambulike.

“Kwa hiyo mashahidi wote ambao ni raia, wasiwekwe wazi majina yao, anuani zao, location zao (mahali wanakoweza kupatikana) wakati wa committal (mwenendo wa uhamishaji kesi kutoka Mahakama ya chini kwenda Mahakama Kuu) na wakati wa ushahidi,” ameamuru Jaji Mtembwa na kuongeza:

“Kama shahidi si raia (yaani ni askari), atatoa ushahidi katika hali ya kawaida (kwa kuonekana) na bila kufichwa jina na taarifa zake nyingine zinazomhusu.”

Amesisitiza kuwa katika hatua hizo zote mbili, haitaruhusiwa kusambaza au kutangaza taarifa zozote ambazo zinaweza kufanya jamii ikajua huyu ni fulani.

“Haitakuwa na maana unaficha mahakamani lakini chombo cha habari kimoja kinasema huyu ni fulani, isipokuwa vyombo vya habari vitaruhusiwa kufanya hivyo kwa kuruhusiwa na Mahakama, wapate ridhaa ya Mahakama husika,” amesema, akibainisha kuwa vyombo vya habari navyo vina namna yake ya kupata taarifa.

“Hivyo, hakutakuwa na ruhusa kusambaza na kuchapisha taarifa zinazoweza kufanya jamii ikafahamu jina, location au makazi yake, au ndugu zake, marafiki zake na watu wa karibu, isipokuwa kwa kibali cha Mahakama,” amesema.

Kutokana na uamuzi huo, Jaji Mtembwa ameielekeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kuweka utaratibu wa kuondoa katika nyaraka mbalimbali majina na taarifa za mashahidi zinazoweza kufanya wakajulikana.

Hata hivyo, ameielekeza ofisi hiyo kuandaa taarifa ambazo zitamwezesha mshtakiwa kujua kiini cha kesi.


Mashtaka dhidi ya Lissu

Katika kesi inayosikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswaga, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume cha Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025, ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Anadaiwa siku hiyo, kwa nia ya uchochezi, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli..., kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko..., kwa hiyo tunaenda kukinukisha..., sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana...”

Mara ya mwisho kesi hiyo ilitajwa mahakamani hapo Julai 30, 2025 kwa ajili ya upande wa mashtaka kutoa taarifa kama ulikuwa umeshawasilisha hati ya mashtaka Mahakama Kuu ili kesi hiyo ihamishiwe huko kwa ajili ya kuanza kusikilizwa katika hatua ya ushahidi.

Hata hivyo, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa bado ulikuwa haujapeleka hati ya mashtaka Mahakama Kuu kwa kuwa shauri la maombi ya ulinzi wa mashahidi lilikuwa bado halijatolewa uamuzi.

Upande wa mashtaka uliomba ahirisho la kesi hiyo mpaka tarehe nyingine kusubiri uamuzi wa shauri hilo Mahakama Kuu, ombi ambalo lilipingwa na Lissu aliyeiomba Mahakama isitoe ahirisho hilo, bali iamuru aachiliwe huru kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kupeleka hati ya mashtaka Mahakama Kuu.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hiyo ya awali, Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswaga, baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 13, 2025 kwa ajili ya uamuzi wa pingamizi la Lissu.

Pia ameutaka upande wa mashtaka kufuatilia uamuzi huo ili kesi hiyo ihamishiwe Mahakama Kuu haraka kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Lissu ataendelea kubaki mahabusu wakati kesi hiyo ikiendelea mpaka itakapoisha au itakapoamuliwa vinginevyo kwa kuwa shtaka hilo halina dhamana.