Mahakama yawaongeza muda watoto wa Hans Poppe kupeleka orodha ya mali
Muktasari:
- Katika kesi hiyo, watoto wa marehemu Hans Poppe, wanaiomba iamuru wakurugenzi wa kampuni alizokuwa akimiliki baba yao, wawasilishe mahakamani taarifa ya mapato na matumizi tangu baba yao alipofariki dunia.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia, Temeke, imewaongezea muda watoto wa Zacharia Hans Poppe ili wapeleke orodha ya mali ya ziada alizokuwa anamiliki baba yao na ambazo hazikuwemo katika orodha ya awali waliyoiwasilisha mahakamani.
Watoto hao, Angel na Abel ambao ni wasimamizi wa mirathi hiyo, ambapo katika kesi ya mirathi ya Zacharia Hans Poppe namba 177/2022, waliwasilisha ombi hilo wakati shauri hilo lililoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mawakili wa wawasilisha maombi, Emmanuel Msengezi na Regina Helman wamewasilisha ombi hilo leo Septemba 13, 2024 mbele ya Jaji Glady’s Nancy Barthy, anayesikiliza shauri hilo.
Wakili Msengezi amesema wateja wake wanaomba waongezewe muda ili waweze kuona kama watapeleka orodha ya mali ya ziada alizokuwa anamiliki Hans Poppe, enzi za uhai wake ambazo hazikuorodheshwa kwenye orodha ya awali ambayo iliwasilisha mahakamani hapo.
Amedai kuwa mali hizo zinatokana na Hans Poppe kuwa na hisa katika kampuni nyingine zenye ubia na yeye, ambazo zinatakiwa kuwasilishwa mahakamani hapo ili ziunganishwe kwenye orodha ya mali ya awali iliyopo mahakamani hapo.
Msengezi baada ya kuwasilisha ombi hilo, Jaji Nancy Barthy alikubaliana nalo na kuahirisha shauri hilo hadi Oktoba Mosi kwa ajili ya kutajwa.
Wasimamizi wa mirathi ya marehemu Hans Poppe, wanaomba wakurugenzi wa kampuni za Z.H.P Ltd, Hans Poppe Hotels Ltd na Z.H. Poppe Limited, zinazomilikiwa na Zacharia Hans Poppe wawasilishe orodha ya mali zilizopo katika kampuni hizo.
Wakurungenzi watendaji wa kampuni hizo ni Caeser Hans Poppe na mwanaye Adam Caeser Hans.
Caeser ni mdogo wake, Zacharia Hans Poppe ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba na Adamu ni mtoto wa Caeser ambao kwa pamoja ni Wakurugenzi katika kampuni ya Z. H. Poppe Ltd inayomilikiwa na marehemu Zacharia kwa asilimia 90 ya hisa zote.
Vilevile, waombaji hao wanaomba wasomewa orodha ya mali iliyokusanywa na kutoa taarifa ya hesabu ya fedha tangu baba yao alipofariki hadi sasa.
Pia, wanaiomba Mahakama hiyo ielekeze wakurugenzi hao waeleze hali ya mali za marehemu Zacharia zilizopo katika kampuni zake ikiwemo taarifa ya mapato na matumizi.
Zacharia HansPoppe alifariki dunia Septemba 10, 2021 katika Hospitali ya Aga Khan alikokuwa akipatiwa matibabu na mazishi yake yalifanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.
Hans Poppe alikuwa mwanachama kindakindaki wa klabu ya wekundu wa Msimbazi na atakumbukwa na wanachama kwa kuleta mafanikio makubwa ndani ya klabu ya Simba, kwa uhamasishaji aliofanya baada ya kuteuliwa pia kuwa mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba (Friends of Simba).