Prime
Mirathi ya Hans Poppe yaibua mapya kortini

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Caeser HansPoppe, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Z.H.Poppe na mwanawe Adam, wanadaiwa kuidharau Mahakama Kuu kwa kushindwa kufika mahakamani kutoa orodha ya mali iliyokusanywa na kampuni hiyo.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC Temeke), jijini Dar es Salaam, imetoa hati ya kukamatwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Z. H. Poppe Ltd, Caeser Hans Poppe na mwanawe Adam Caeser Hans Poppe kwa kuidharau mahakama.
Imeelezwa Caeser na Adam ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo wakamatwe na wapelekwe mahakamani hapo Julai 19, 2024, ili washtakiwe kwa kosa la kuidharau mahakama.
Caeser ni mdogo wake Zacharia Hans Poppe, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, ametakiwa afike mahakamani hapo kutokana na kukaidi amri ya mahakama kwa kushindwa kuitikia wito wa kwenye shauri la mirathi ya marehemu Zacharia Hans Poppe.
Hati hiyo ya kukamatwa wawili hao ambayo Mwananchi imefanikiwa kuiona, imetolewa Julai 4, 2024 na Jaji Glady’s Nancy Barthy, baada ya kushindwa kufika mahakamani kwa tarehe iliyopangwa.
Caeser alitakiwa kufika mahakamani hapo kueleza hali ya mali za Zacharia Hans Poppe, ikiwemo taarifa ya mapato na matumizi lakini hakutokea.
Jaji Barthy amefikia uamuzi huo baada ya watoto wa marehemu Zacharia, Angel na Abel pamoja na kuiomba mahakama hiyo iamuru na kumuita baba yao mdogo (Adam Caeser Hans Poppe) aende kutoa taarifa ya fedha, ikiwemo mapato na matumizi yaliyopo katika kampuni ya baba yao mzazi iitwayo, Z. H. Poppe Ltd ambayo kwa sasa inasimamiwa na Adam.
Katika maombi hayo, Wakili Regina Herman anayemsimamia Analisa Zacharia Poppe, mtoto mkubwa wa marehemu Zacharia Hans Poppe, ameiomba mahakama hiyo itoa adhabu kali dhidi ya wakurugenzi hao kwa kuaidi amri hiyo ya mahakama.
Wakili Herman amedai mteja wake ameomba Caeser na Adam waitwe mahakamani kwa sababu wao ndio wanashikilia hisa na mali za Zacharia Hans Poppe katika kampuni zake na pia wanadaiwa kuendesha kampuni hiyo bila kuwashirikisha warithi ambao ni watoto.
Ombi la kukamatwa kwa wakurugenzi hao limeungwa mkono na Wakili Emmanuel Msengezi anayewatetea wasimamizi wawili wa mirathi ya Zacharia ambao ni Angel Zacharia Poppe na Abel Zacharia Poppe.
Msengezi amedai katika kampuni hizo, Zacharia Hans Poppe anamiliki hisa kwa asilimia 90 wakati Caeser ana hisa asilimia 10.
Wakili Msengezi amedai baada ya kuwasilisha maombi hayo, waliomba mahakama itoe hati ya wito, ili Adam afike mahakamani hapo kwa kuwa mkurugenzi huyo anaendelea kushikilia mali za marehemu Zacharia, huku akiendelea kukopa kwa jina la kampuni na kushindwa kulipa madeni ya kampuni hizo.
Amedai kuwa kampuni za Hans Poppe zinaingiza fedha nyingi, lakini halipi madeni huku warithi wa kampuni hiyo ambao ni Abel na Angel, akikataa kuwaingiza katika kampuni hiyo wawe wasimamizi.
Chimbuko la hati hiyo ya kukamatwa inatokana na kesi ya mirathi ya marehemu Hans Poppe, namba 177 ya mwaka 2022 iliyofunguliwa katika mahakama hiyo.
Kesi hiyo ipo hatua ya usikilizwaji ambapo Julai 4, 2024 iliitwa kusomewa orodha ya mali iliyokusanywa na kutoa taarifa ya kufungwa kwa hesabu na namna mali hizo zilivyogawanywa, lakini wakurugenzi hao hawakufika mahakamani, ndipo mawakili wa wasimamizi wa mirathi walipowasilisha ombi kwa mahakama itoe hati ya kuwakamata.
Zacharia Hans Poppe alifariki dunia Septemba 10, 2021 katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. Maziko yake yalifanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.
Hans Poppe anakumbukwa na wanachama wa Simba na klabu hiyo kwa kuleta mafanikio makubwa ndani ya klabu ya Simba kwa uhamasishaji aliofanya baada ya kuteuliwa, pia kuwa mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba ‘ Friend of Simba’ ambalo lilijizolea umaarufu mkubwa ndani ya klabu hiyo.