Huyu ndiye Zacharia Hans Poppe usiyemfahamu

Wednesday September 15 2021
hansspopepicc
By Luqman Maloto

Leo, Kihesa, Iringa, mfanyabiashara maarufu Tanzania, Zacharia Hans Poppe atapumzishwa kwenye nyumba yake ya dawamu. Zacharia alifikwa na mauti akibakiza takriban mwezi mmoja atimize umri wa miaka 66.

Maisha ya Zacharia yana mafundisho mengi kwa wakati mmoja kuhusu maisha. Kwanza ni kutokata tamaa, pili ni kwamba kama dunia haijasimama na pumzi unayo, mafanikio yanahitaji juhudi na maarifa yako tu. Tatu, kwa umuhimu mkubwa, kila binadamu anahitaji nafasi ya pili.

Kama Mwenyezi Mungu alivyompa Yona (Yunus) nafasi ya pili kwenye tumbo la samaki, ndivyo Zacharia alivyotendewa na Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi. Ndio maana leo hii, Zacharia leo anatambuliwa katika sura nyingi. Kuanzia kwenye siasa na tukio la kutisha na kustaajabisha hadi mtu mashuhuri kwenye biashara na michezo.

Soma zaidi:Zacharia Hanspoppe aacha historia ya kusisimua

Wapo wanaomshangaa Zacharia; alitoka jela mwaka 1995, halafu ndani ya miaka tisa, akawa tajiri hadi kuitwa mfadhili wa Simba. Hili limethibitishwa bila kuacha shaka na simulizi kuhusu marehemu, alipokuwa akiagwa viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.

Crecentius Magori ni mshauri wa Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohammed Dewji ‘MO’. Magori alisimulia kuwa kuanzia mwaka 2004 mpaka mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Simba yalipofanyika, mfadhili mkuu wa Simba alikuwa Zacharia.

Advertisement

Soma zaidi:Mo Dewji: Hans Poppe ulikua wa kwanza kuilinda Simba

Magori alisema, mwaka 2003, aliyekuwa mfadhili wa Simba, MO, alijitoa kwa sababu wanachama walikataa mawazo ya kuibinafsisha klabu hiyo, hasa baada ya kuwafunga waliokuwa mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika, Zamalek na kuingia robo fainali.

Magori na Kaimu Mkuu wa Mawasiliano Simba, Ezekiel Kamwaga walitoa simulizi ya jinsi ambavyo Zacharia alipewa gari moja, lori aliloanza kuendesha mwenyewe, akifanya kazi pia kama utingo na fundi. Akawa anaendesha mwenyewe kutoka Tanzania kwenda Zambia, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Gari hilo moja likazaa magari mengine mengi. Akamiliki malori, magari ya kusafirisha mafuta, gereji na biashara nyingine.

Biashara hizo zimetoa ajira nyingi kwa Watanzania, kodi inayolipwa imechochea maendeleo ya nchi.

Ni mafanikio hayo yaliyomwezesha Zacharia kuwa na jeuri ya kuwa mfadhili wa Simba, aliyetumia fedha nyingi kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu ya moyo wake.

Zacharia aliheshimu nafasi ya pili aliyopewa. Bila shaka aliamini uhuru aliopewa kwa msamaha wa Rais ni fursa muhimu ya kuonesha kipaji _kingine alichokuwanacho kuhusu biashara. Bila shaka alikidhihirisha. Vipi Zacharia angefia jela, angeimbwa kishujaa kama sasa?

Ni kwa sababu Zacharia alitumia vema nafasi ya pili aliyopewa, ndio maana leo anatambuliwa kwa sura nyingi. Kwanza ni mtoto wa Hans Poppe, Kamishana Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP), aliyeuawa na askari wa Nduli Idi Amin Dada. SACP Hans Pope alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera.

Hans Poppe aliuawa Agosti 24, 1971 kwenye mpaka Uganda. Baada ya hapo, wanajeshi wa Uganda waliuchukua mwili wake na kwenda kuuhifadhi nchini kwao. Hata hivyo, baada ya Vita ya Kagera na Jeshi la Tanzania kufanikiwa kumwondoa madarakani Amin, mwili wa Poppe ulirejeshwa Tanzania na kuzikwa kwa heshima zote.

Poppe alizikwa rasmi Mei 26, 1979. Wakati huo, Zacharia alikuwa hajatimiza hata umri wa miaka 23, tayari alishakuwa ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). Na alikuwa Uwanja wa Ndege wa Entebbe, akishiriki kikamilifu usafirishaji wa mwili wa baba yake kurejea Tanzania kwa mazishi rasmi.

Soma zaidi:Kifo cha Hans Poppe chakumbusha historia ya baba yake

Zacharia alipigana Vita ya Kagera, hivyo ni mmoja wa mashujaa walioipigania nchi na kufanikiwa kumwondoa Amin madarakani, aliyelazimika kutoroka. Baada ya ushindi wa Tanzania, Zacharia alifanya upelelezi kuhusu mahali mwili wa baba yake ulipozikwa nchini Uganda, akabaini hakuzikwa. Mwili ulikuwa umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti, Hospitali ya Taifa la Uganda, Mulago.

Yupo anayemfahamu Zacharia kwa rekodi yake ya kuwa na cheo cha Luteni Usu, ndani ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), akiwa na umri wa miaka 19 tu. Kabla yake, hakukuwa na askari yeyote wa JWTZ aliyepata kufikia ngazi hiyo katika umri sawa na huo au chini yake.

Wapo wengi wanamtambua Zacharia kwa ule utambulisho wake wa kushiriki jaribio la mapinduzi. Ndiyo, Zacharia alikuwa mmoja wa washitakiwa wa kesi ya uhaini, baada ya kushiriki kula njama za kumpindua Rais wa Kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Tukio hilo limeacha historia kubwa kwenye siasa za nchi. Zacharia yupo kwenye historia ya Tanzania, sawa na baba yake, SACP Poppe.

Mashabiki wa Simba hawaambiwi kitu kuhusu uhusika wake kwenye klabu yao. Alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na nafasi hiyo ikamfanya aingie kwenye kesi ambayo hukumu yake bado. Mashtaka ni uhujumu uchumi, ikiwemo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na utakatishaji wa fedha.

Aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, walipandishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 27, 2017. Ilipofika Aprili 16, 2018, Zacharia aliunganishwa kwenye kesi hiyo.

Kilichotokea; siku taarifa ya Zacharia inatoka, tayari alikuwa ameshaondoka nchini. Zikafuata zama za kutoa hati na ahadi kemkem kwa ambaye angetoa taarifa ambazo zingefanikisha kukamatwa kwa Zacharia, ili afikishwe mahakamani kujibu mshitaka.

Oktoba 15, 2018, Zacharia alirejea nchini, akakamatwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kisha Oktoba 16, 2018, alifikishwa mahakamani, akaunganishwa na Aveva pamoja na Kaburu. Hata hivyo, siku hiyo hiyo Zacharia aliachiwa kwa dhamana.

Swali likabaki, iliwezekana vipi Zacharia apate dhamana kabla ya Aveva na Kaburu walioendelea kusota? Ilikuwaje atoroke muda mfupi kabla hajaunganishwa kwenye kesi? Miezi sita ambayo Zacharia alitafutwa bila kupatikana, kwa mahakama hilo tukio litakalosomwa kwa vizazi na vizazi.

Ni funzo kwa Serikali kuwapa nafasi ya pili wakosefu. Kama si Rais Mwinyi kusamehe wafungwa wa uhaini waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela, upande wa pili wa Zacharia usingejulikana. Asingetambulika leo kama mfanyabiashara aliyefanikiwa. Asingeajiri aliowaajiri. Muhimu pia wanaopewa nafasi za pili, kuzitumia ipasavyo.

Advertisement