Kifo cha Hans Poppe chakumbusha historia ya baba yake

Kifo cha Hans Poppe chakumbusha historia ya baba yake

Muktasari:

  • Uhai wa Hans Pope, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa Ziwa Magharibi (sasa Kagera), ulikatizwa na wanajeshi wa Idi Amin walioivamia Tanzania Agosti, 1971.

Dar es Salaam. Uhai wa Hans Pope, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa Ziwa Magharibi (sasa Kagera), ulikatizwa na wanajeshi wa Idi Amin walioivamia Tanzania Agosti, 1971.

Hans Pope ndiye baba mzazi wa mfanyabiashara maarufu nchini, Zacharia Hans Poppe aliyefariki jijini Dar es Salaam.

Mgogoro kati ya Uganda na Tanzania ambao baadaye ulisababisha mauaji ya Hans Pope ulianza Jumatatu ya Januari 25, 1971 wakati Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Idi Amin, alipompindua Rais wa Uganda, Dk Milton Obote.

Obote alikimbilia Tanzania ambako aliungana na wanajeshi zaidi ya 1,000 waliokuwa wakimtii. Kutokana na Dk Obote kuwa nchini, Amin aliichukulia Tanzania kama kituo cha kijeshi dhidi ya utawala wake na hivyo uhasimu mkubwa uliibuka kati ya Rais Julius Nyerere wa Tanzania na Idi Amin wa Uganda.

Jumatano ya Julai 7, 1971 Amin alifunga mpaka wake na Tanzania. Siku chache baadaye aliituhumu Tanzania kwamba inawalinda waasi wa Uganda.

Jumanne ya Agosti 24, 1971 majeshi ya Idi Amin yalivuka mpaka na kuingia Tanzania eneo la Mutukulan wakiongozwa na Luteni Kanali Abdul Kisule.

Ingawa wanajeshi hao walikuwa wachache, waliingia nchini na vifaru viwili wakidai wamekuja kuwaokoa wenzao waliokuwa wamekamatwa upande wa Tanzania.

Katika kuwatafuta hao waliodai kuwa wameshikiliwa Tanzania, walimkuta RPC Hans Pope akiwa na dereva wake kwenye gari aina ya Land Rover.

Hans Pope alipoona anafuatwa na wanajeshi wa Uganda, alikimbilia redio ya upepo (radio call) ili awasiliane na makao makuu kuhusu uvamizi wa wanajeshi wa Uganda.

Lakini kabla hajaifikia, alipigwa risasi ya paja na kuanguka. Dereva wake alijaribu kushika bunduki ili apambane na wavamizi, lakini naye akapigwa risasi mkononi.

Wanajeshi hao wa Uganda walimteka Hans Pope na kuondoka naye. Nchini Uganda Idi Amin alitangaza kupitia vyombo vya habari vya nchi hiyo kwamba Hans Pope ni mamluki wa Kichina aliyevamia Uganda.

Aliuawa Jumanne Agosti 24, 1971 na mwili wake kuwekwa maonyesho kwa siku tatu.

Baada ya hapo, wanajeshi wa Amin waliupeleka mwili wa Hans pope huko Hospitali ya Mulago.

Dk James Makumbi alikuwa daktari katika hospitali ya Mulago 1971 wakati mwili wa Hans Pope ulipofikishwa hospitalini hapo ukiwa na majeraha ya risasi.

Mwili wa Hans Pope, ambaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 53, uliendelea kuhifadhiwa hadi pale Tanzania ilipoingia vitani dhidi ya Uganda na kuikomboa.

Mwaka 1979 serikali mpya ya Uganda iliukabidhi mwili kwa Serikali ya Tanzania katika hafla iliyofanyika jijini Kampala, iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Otema Alimadi.

Mwenzake wa Tanzania, Benjamin Mkapa, ambaye miaka kadhaa baadaye alikuja kuwa Rais, alikuwa nchini Uganda kupokea mwili wa mwanausalama huyo aliyekufa akiwa katika harakati za kuilinda nchi yake.