Hanspope augua, kesi yashindwa kuendelea

Hanspope augua, kesi yashindwa kuendelea

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  imeshindwa kuendelea kusikiliza utetezi katika  kesi ya kughushi  inayowakabili waliokuwa viongozi wa tatu wa timu wa Simba.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  imeshindwa kuendelea kusikiliza utetezi katika  kesi ya kughushi  inayowakabili waliokuwa viongozi wa tatu wa timu wa Simba.


Ni baada ya mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Zacharia Hanspope, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa timu hiyo, kuugua.

Mbali na Hanspope, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa rais wa timu hiyo Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu Kaburu.


Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka nane yakiweno ya kughushi, matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha bila kamati ya utendaji ya Simba, kukaa kikao.


Hayo yameelezwa leo, Agosti 31, 2021 na wakili wa Hanspope, Benedict Ishabakaki, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati shauri hilo liliripotiwa kwa ajili ya washtakiwa kujitetea.

Wakili Ishabakaki amedai kuwa mteja wake ambaye ni Hanspope ni mngojwa na leo ameshindwa kufika mahakamani hapo kwa ajili kusikiliza shauri hilo, hivyo anaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine.


Kabla ya kuahirisha kwa kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Maghela Ndimbo ameieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili washtakiwa kujitetea, baada ya kukutwa na kesi ya kujibu Septemba 20, 2019.


Hata hivyo kutoka na mshtakiwa mmoja kuwa mgonjwa, Ndimbo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na kesi hiyo.


Hakimu Simba alikubaliana na hoja hizo na kuhiridha shauri hilo hadi Septemba 3, 2021 itakapoendelea.


Washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili, ambapo kila mdhamini  alisaini dhamana ya Sh30 milioni.

Imeandikwa na Hadija Jumenne, Kifrago Ibrahim na Rukia Kiswamba