Mawakili wakwamisha kesi ya Aveva, Hans Pope

Muktasari:

Kesi ya kughushi na kutakatisha fedha inayowakabili  vigogo watatu wa klabu ya Simba imeahirishwa baada ya mawakili kutofika mahakamani

Dar es Salaam. Kesi ya kughushi na kutakatisha fedha inayowakabili vigogo watatu wa klabu ya Simba ya Tanzania imekwama kuendelea na ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hali hiyo imetokana na mawakili wa utetezi wa mshtakiwa wa kwanza,  Evans Aveva kushindwa kufika mahakamani hapo.

Mbali na Aveva ambaye ni rais wa zamani wa klabu hiyo, wengine ni Makamu wake,  Geofrey Nyange na Mwenyekiti wa  Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Pope.

Wakili wa Takukuru, Leonard Swai amedai leo Jumatano Desemba 19,  2018 mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

" Shauri hili limekuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi na upande wa mashtaka,  tayari tuna mashahidi wawili na tuko tayari kuendelea," amedai Swai.

Swai baada ya kueleza hayo wakili wa utetezi, Nestory Wandiba alisimama na kueleza mahakama kuwa mawakili wawili wanaomtetea Aveva wapo Mahakama Kuu.

"Mawakili Nehemia Nkoko na Wabea wapo Mahakama Kuu  wana kesi nyingine huko. Tunaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi" amedai Wandiba anayemtetea Nyange.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote , amewataka mawakili hao kuhakikisha wanafika mahakamani bila kukosa siku ambayo kesi hiyo itaendelea.

Kesi hiyo imeahirishwa  hadi Januari 3, 2019 na washtakiwa Aveva na Nyange wamerudishwa rumande kutoka mashtaka yao kutokuwa na dhamana.

Tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka ameshatoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.

Kesi hiyo inatokana na matumizi ya pesa za uhamisho wa mchezaji wa klabu hiyo, Emmanuel Okwi kwenda Klabu ya Soka ya Etoile Sportive Du Dahel ya Tunisia, kwa madai ya kutumia pesa hizo kununulia nyasi bandia na gharama za ujenzi wa uwanja huo.

Katika kesi hiyo Hans Pope anakabiliwa na mashtaka mawili; ya kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uongo yeye pamoja na wenzake.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka mengine zaidi ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kujipatia pesa isivyo halali (Aveva) na utakatishaji fedha yanayowakabili  Aveva na Kaburu.

Washtakiwa Aveva na Nyange wanatetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Nestory Wandiba wakati Hans Pope akitetewa na wakili Agostino Shio, Benedict Ishabakaki na Jebra Kambole.