Mahakama yapokea cheti cha maziko cha Hans Poppe

Muktasari:
- Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepokea cheti cha maziko cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya klabu ya Simba, marehemu Zacharia Hans Poppe.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepokea cheti cha maziko cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya klabu ya Simba, marehemu Zacharia Hans Poppe.
Hans Pope alifariki dunia Septemba 10, 2021 katika hospitali ya Aga Khan, wakati akipatiwa matibabu na mazishi yake yalifanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.
Cheti hicho cha maziko, kimewasilishwa mahakamani hapo leo, Septemba 22, 2021 na wakili wa Hans Poppe, Benedict Ishabakaki, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na utetezi.
"Mheshimiwa Hakimu, kama mahakama yako ilivyoelekeza, leo naomba kuwasilisha cheti cha maziko cha mteja wangu mahakamani hapa, ili kudhinitisha kifo chake," amesema Ishabakaki.
Ishabakaki baada ya kueleza hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Maghela Ndimbo amesema kuwa hana pingamizi juu ya cheti hicho na hivyo kuomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na utetezi kwa washtakiwa waliobaki katika kesi hiyo.
Hans Poppe na wenzake wawili ambao ni aliyekuwa rais wa klabu hiyo, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu Kaburu, wanakabiliwa na mashtaka manane yakiweno ya kughushi, matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha bila Kamati ya Utendaji ya Simba kukaa kikao.
Tayari Aveva ameanza kujitetea katika kesi hiyo, baada ya mahakama kuwakuta na kesi ya kujibu washtakiwa wote.