Mahakimu 200 wafundwa kukabili kesi za rushwa, utakatishaji fedha

Muktasari:

Mahakimu wakazi wametakiwa kuwa na uelewa, maarifa na uwezo wa kukabiliana na kesi za rushwa na utakatishaji fedha.

Lushoto. Mahakimu wakazi wametakiwa kuwa na uelewa, maarifa na uwezo wa kukabiliana na kesi za rushwa na utakatishaji fedha.

Wito huo umetolewa na Jaji wa Makama Kuu ya Tanzania, Edwin Kakolaki wakati akifungua mafunzo juu ya uendeshaji wa mashauri ya rushwa, utakatishaji fedha na urejeshaji mali zilizopatikana kwa fedha haramu kwa mahakimu wakazi, yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Jaji Kakolaki amesema makosa hayo ya rushwa na utakatishaji fedha hufanywa na watu wenye uelewa mkubwa katika maeneo waliyoyafanyia makosa na hata wanaweza kuwa wataalamu wa sheria.

Amewaambia mahakimu wakazi 200 ambao wamehudhuria mafunzo hayo kuwa Mahakama imekuwa ikipambana na makossa hayo na wao wasisisite kutoa elimu juu ya madhara ya rushwa na utakatishaji fedha kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa kesi za rushwa na utakatishaji fedha zipo katika maeneo mengi akieleza matumaini yake kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu katika kutatua migogoro mbalimbali watakayokutana nayo katika uendeshaji wa mashauri hayo.

Amewakumbusha kuutumia vizuri uhuru wao na uhuru wa Mahakama katika kuamua mashauri yaliyopo mbele yao bila woga na kutoegemea upande wowote.

“Mkiwa imara na madhubuti katika kazi zenu, mtakuwa mmetimiza malengo ya Mahakama na ya nchi. Nitumie fursa hii kusisitiza kwamba muwe mstari wa mbele katika kuleta amani, upendo, matumaini na faraja kwa watu mahakamani na nje ya mahakama,” amesisitiza.

Jaji Kakoloaki pia amewakumbusha mahakimu na watumishi wote wa mahakama juu ya umuhimu wa kuzingatia maadili katika utumishi wa Mahakama na utumishi wa umma kwa ujumla.

“Kazi yenu ya kutoa haki iende sambamba na uwepo wa maadili mema. Katika maisha yenu ya utendaji kazi, muendelee kuwa kioo na kielelezo cha maadili mema, hofu ya Mungu na kutotengeneza mazingira ya kuwa na tabia zisizofaa katika utumishi wa umma,” amesema.

Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Wilbert Chuma ameonya kuwa kama vita dhidi ya rushwa, uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha isipopigwa vyema kutakuwa na madhara makubwa sana katika nchi.

Amesema jumla ya Mahakimu wapatao 200 wanahudhuri amafunzo hayo ambayo yamepangwa kuhitimishwa Jumamosi ijayo ambayo yameandaliwa na Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Kitengo cha Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania.