Mahona aeleza siri ya mafanikio yake uchaguzi mkuu uliopita

Mahona aeleza siri ya mafanikio yake uchaguzi mkuu uliopita

Muktasari:

Uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 ulikuwa wa aina yake katika historia ya Tanzania baada ya wagombea 15 kujitokeza.

Uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 ulikuwa wa aina yake katika historia ya Tanzania baada ya wagombea 15 kujitokeza.

Idadi hiyo ya wagombea ndio kubwa zaidi kuwahi kutokea katika uchaguzi mmoja nchini.

Kati ya wagombea hao, alikuwapo Leopold Mahona wa chama cha NRA. Yeye alikuwa ndiye mdogo zaidi kati ya wote waliopitishwa na vyama vyao.

Baada mchakato mzima kukamilika, Mahona alishika nafasi ya nne na kumpita Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyeshika nafasi ya tano licha kugombea urais kwa mara ya tano sasa.

Akivuna kura 80,787 Mahona alikuwa nyuma ya Membe aliyepata 81,129 akitanguliwa na Lissu mwenye kura 1,933,271 katika uchaguzi ambao Dk Magufuli aliibuka kidedea kwa kura 12,516,252. Mahona alimzidi Profesa Lipumba aliyepata kura 72,885.

“Hayo ni mafanikio makubwa kwangu ukizingatia nimegombea urais kwa mara ya kwanza,” anasema Mahona.

Mahona ameeleza siri ya mafanikio aliyoyapata kwenye uchaguzi huo uliowafanya watu kutaka kumfahamu zaidi na siasa zake za “chini kwa chini.”

Anasema alikuwa mgombea pekee ambaye amewahi kuwa katibu mkuu wa vyama vitatu tofauti, jambo lililomfanya awe na mtaji mkubwa wa wapigakura kwa sababu tayari wanamfahamu.

“Hiyo ndiyo sifa kubwa niliyokuwa nayo kuliko wagombea wengine, maana yake nilikuwa nafahamika na wanachama wa vyama tofauti,” anasema Mahona.

Anasema yeye ndiye katibu mkuu wa kwanza wa ACT Wazalendo kabla hajatimkia Sauti ya Umma (Sau) alikodumu kwa mwaka mmoja kama katibu mkuu pia. Mahona ni miongoni mwa waasisi wa chama cha ADC ambacho alikuwa katibu mkuu wake pia.

Mahona ambaye ni mwalimu kitaaluma, anasema siri nyingine ya kufanya vizuri ni aina ya kampeni alizokuwa akifanya kwa kukutana na wananchi katika maeneo yao badala ya mikutano ya kampeni kama wagombea wengine.

“Nilikuwa nawafuata watu katika maeneo yao, nikiweka mafuta ya laki moja, nilikuwa nazunguka Dar es Salaam nzima. Nimefanya hivyo katika mikoa yote na kuwafikia wananchi wengi,” anasema Mahona.

Anasema mfumo huo anaouita “mobile campaigning system” hauna gharama kubwa kwa sababu anafunga kila kitu kwenye gari lake ili aweze kuweka kambi popote na kuzungumza na wananchi.

“Nilikuwa nakutana na wananchi moja kwa moja, nawaeleza sera zangu. Wengi walikuwa wananielewa na wengine tulikuwa tunakubaliana kutokukubaliana,” anasema Mahona.


Changamoto katika uchaguzi

Mahona anasema changamoto kubwa aliyoiona kwenye uchaguzi mkuu ni muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambao hautoi mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea wote bali unampendelea mmoja.

Anataka muundo wa tume ubadilishwe na iwe huru itakayosimamia uchaguzi katika mazingira yatakayowawezesha kutenda haki kwa wagombea wote.

“Ninaposema tume huru ya uchaguzi, simaanishi uongozi wa juu tu. Tunataka mabadiliko kuanzia ngazi ya chini ya wasimamizi mpaka Taifa,” anasema mgombea huyo.

Anasema kulikuwa na uhusiano kati ya watendaji wa NEC na Serikali, na kati ya watendaji wa tume na CCM jambo analosema linaondoa uhuru katika kutekeleza majukumu yake.

“Naipongeza Serikali kwa kuandaa uchaguzi mkuu kwa kutumia fedha za ndani lakini hiyo peke yake haitoshi. Tunahitaji Tume huru ya uchaguzi,” anasema Mahona.

Changamoto nyingine aliyoiona wakati wa uchaguzi anasema ni vyombo vya habari kutotoa nafasi sawa kwa wagombea wote kwani vilijikita kwa wagombea wawili tu.

“Watu wa habari hamjawa fair, mimi mpaka namaliza kampeni zangu sijawahi kuhojiwa na kituo chochote cha televisheni,” anasema Mahona na kuongeza kuwa gazeti la Mwananchi lilijitahidi kidogo katika kuwafikia wagombea wengi zaidi.

Uhaba wa rasilimali fedha ni changamoto nyingine aliyokutana nayo kipindi cha kampeni. Anasema alikuwa akichangiwa fedha na marafiki pamoja na chama chake kumwezesha kuwafikia wananchi kunadi sera zake.

Pia, anasema alikumbana na wananchi waliotaka kupewa fedha ili siku ya uchaguzi wakampigie kura hivyo kulazimika kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kura zao.

Mahona anasema baadhi ya maeneo yalikuwa na changamoto ya usalama kwa sababu makamanda wa mikoa hiyo hawakutoa ulinzi wakati wa kampeni zake akitolea mfano Mkoa wa Tanga.

Vilevile, anasema baadhi ya maelekezo ya NEC yalikuwa yanachanganya na kusababisha kero siku ya uchaguzi. Anasema maelekezo yaliyotolewa yalisababisha mawakala wengi kuondolewa vituoni na wengine kuruhusiwa muda ukiwa umeenda.


Familia

Mahona anasema suala la kugombea urais ilikuwa ni ndoto yake tangu akiwa mdogo na aliwahi kuwaeleza wazazi wake hivyo waliposikia anachukua fomu hawakushangaa ingawa walijua haitawezekana.

Anasema baada ya kukamilisha mchakato wote mpaka kuteuliwa na NEC ndipo familia yake ikaamini lakini swali likabaki atapata wapi fedha za kampeni.

“Mimi nilikuwa mmoja wa wagombea waliojaza fomu zao vizuri. Zile fomu zina zaidi ya kurasa 40, zinahitaji umakini mkubwa. Walipoona nimepitishwa, ndipo wakaamini,” anasema.

Kutokana na mwenendo wa baadhi ya wapinzani kuhamia CCM kwa maelezo ya kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli, Mahona anasema yeye hafikirii kufanya hivyo kwa sababu hajaona kinachoweza kumpeleka huko.

Anasema anakifahamu vizuri chama hicho na amewahi kuwa mwanachama wake.

“Bado sijashawishika kwenda CCM. Kwa sasa naona wanavyotofautiana na kufanya mambo ambayo mimi siyaamini. Wao wanasema wanafuata siasa za ujamaa lakini mimi naamini katika ujamaa wa jamii shirikishi,” anasema.