Mahudhurio, madarasa, vifaa,  walimu tatizo  shule zikifunguliwa leo

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Wakati shule za msingi na sekondari zikifunguliwa nchini kote, upungufu wa madarasa, vifaa na walimu vimetajwa kuwa changamoto inayosababisha mazingira magumu ya ufundishaji.

Shinyanga. Upungufu wa madarasa, vifaa na walimu vimetajwa kuwa changamoto waliyoikuta wanafunzi wakati shule za msingi na sekondari zikifunguliwa kote nchini.

Hayo yamebainishwa leo Januari 8, 2024 na walimu wakati wakiendelea na upokeaji wa wanafunzi baada ya shule kufunguliwa.

Jijini Mbeya, wanafunzi watano tu miongoni mwa wengine 32 wenye ulemavu wa akili na usonji wameripoti katika shule ya msingi Itiji Mchanganyiko.

Shule hiyo ni ya pili mkoani hapa inayotoa elimu kwa makundi maalum. Nyingine ni  Katumba II iliyopo Wilaya ya Rungwe.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Januari 8, 2023 mwalimu wa wanafunzi wenye ulemavu wa akili na usonji, Nihuvila Raphael amesema hali za kiuchumi kutoka familia walizotoka pia zinachangia utoro.

 “Kuna changamoto zinazokwamisha wanafunzi kuhudhuria masomo kutokana na sababu za kiuchumi kutoka kwenye ngazi ya familia, kwani mpaka wafikishwe ni lazima rasilimali fedha zitumike wakati wa kuja na kurejea majumbani,” amesema.

Nihuvila amesema mbali na idadi hiyo ndogo ya wanafunzi kuripoti, wana chumba kimoja tu cha darasa wakati vinahitajika vitatu na walimu wanaohitajika ni sita, lakini yuko peke yake.

“Wanafunzi wa elimu maalum wanasoma katika awamu mbili, lakini wanalazimika wote kujifunzia chumba kimoja, kutokana na ukosefu wa walimu miundombinu ya vyumba vya madarasa,” amesema.

Kwa upande wa Mkuu wa Shule, Stephano Haule amesema changamoto kubwa ya wanafunzi kundi maalum kushindwa kuripoti kwa wakati ni kutokana na umbali wa makazi na wakati mwingine kupitilizwa vituo wanapotumia usafiri wa umma, kutokana na kukosekana kwa wakalimani wa lugha za alama.

“Kwa sasa shule ina wanafunzi 52 wenye ulemavu wa akili na usonji kati ya hao 32 bado wako kwenye hatua ya daraja la kwanza na la pili huko 20 wako kwenye madarasa mchanganyiko na wanafunzi wengine,” amesema.

Akizungumza changamoto hizo, Ofisa Taaluma Msingi Jiji la Mbeya ambaye pia ni kaimu Ofisa Elimu wa jiji hilo, Dk Julius Lwinga amesema shule hiyo inayohudumiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, inatambuliwa changamoto zake na wanazifanyia kazi kwa awamu.

"Tumewapa kipaumbele ndio maana hata madarasa mapya tunayojenga wanaingia wao sawa na vyoo kwa kuviwekea mazingira rafiki. Tunaendelea kuzijengea miundombinu bora shule hiyo na nyingine kadri bajeti inavyoruhusu.

"Tumeanza na shule ya Mwenge kwa kujenga bweni ikiwa ni awamu ya kwanza, baada ya hapo tutageukia hiyo Itiji ambayo idadi ya wanafunzi wake siyo wengi, tumejipanga kuhakikisha watoto wote wanapata elimu kwa mazingira mazuri" alisema Dk Lwinga.


Shinyanga

Mkoani Shinyanga, wanafunzi 217 walioandikishwa kuanza darasa la kwanza shule ya Msingi Mwenge Manispaa ya Shinyanga,  wameripoti katika shule hiyo kongwe iliyojengwa mwaka 1938.

Akitoa taarifa ya wanafunzi walioripoti kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme aliyetembelea shule hiyo leo Januari 8, Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mwenge, Abdalah Hemed amesema changamoto kubwa ni uchakavu wa miundombinu ya majengo.

Amesema lengo ni kuandikisha wanafunzi 230 wa darasa la kwanza idadi ambayo inaonekana itazidi kutokana na mwitikio mkubwa wa wazazi kupeleka watoto katika shule hiyo idadi ambayo inakuwa kubwa kuliko iliyopangwa na kusababisha msongamano ambapo shule ina jumla ya wanafunzi 2026.

Kwa upande wa darasa la awali amesema lengo ni kuandikisha wanafunzi 150 lakini ambapo mpaka sasa wameandikisha wanafunzi 80 na nchakato wa uandikishaji unaendelea na mwitikio wa wazazi ni mkubwa kuleta watoto.

Akizungumzia changamoto ya miundombinu ya majengo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme amesema suala hilo litafanyiwa kazi ili kuiweka shule kuwa na muonekano mzuri kutokana na kujengwa miaka mingi hivyo kuhitaji maboresho.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka shule watoto wote wenye umri wa kuandikishwa darasa la awali na darasa la kwanza, huku akiwaonya wenye tabia ya kuwaficha nyumbani watoto wenye ulemavu kwani wote wana haki sawa.

Naye Ofisa elimu Mkoa wa Shinyanga, Dafroza Ndalichako amesema wamelenga kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 69,792 ambapo mpaka sasa wameshaandikisha wanafunzi 44,432, huku awali matarajio yakiwa wanafunzi 75,079 na walioandikishwa mpaka sasa ni 47,182.

Jijini Arusha, jumla ya wanafunzi 32,040 miongoni mwa wanafunzi 34,152 wameanza masomo katika shule za msingi na sekondari katika Jiji la Arusha.

Licha ya uwepo wa mvua, wanafunzi walionekana maeneo mbalimbali wakienda shule walizoandikishwa.

Kwa mujibu wa taarifa za jiji hilo, jumla ya wanafunzi 14,471 wamejiunga na shule za sekondari, wanafunzi 11,521 wameandikishwa kujiunga na darasa la kwanza na wanafunzi 8,160 wakiandikishwa kujiunga shule za awali.

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini amesema leo Januari 8, 2024, kuwa hadi mchana wanafunzi takriban 32,000 walikuwa tayari wamepokelewa katika shule za msingi na sekondari

"Bado uandikishaji unaendelea tuna imani wote ambao wamejiandikisha awali wataendelea na masomo ao katika shule zetu," amesema.

Baadhi ya wazazi akiwamo Anita Mollel amesema bei ya madaftari makubwa na saRe zimepanda sana tofauti na miaka ya nyuma kwa wastani kati ya Sh3, 000 hadi Sh6,000.

"Tunapongeza Serikali kweli tumepata nafasi, hakuna malipo kuandikishwa lakini shida ni vifaa mfano madaftari makubwa bei imepanda kutoka 2,500 hadi 3,500 jambo ambalo limeongeza gharama," amesema.

Naye Philipo John amesema sare za shule zimepanda kutoka wastani wa Sh35, 000 kwa suruali na shati hadi kufikia Sh47, 000.

Mkoani Pwani, uandikishaji wa wanafunzi wanaoanza elimu ya awali na msingi kwenye shule za Serikali unatarajia kuendelea hadi ifikapo Machi mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Januari 8, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge wakati wa ziara yake ya kukagaua mapokezi ya wanafunzi wa darasa la kwanza, awali na kidato cha kwanza kwenye baadhi ya shule mkoani humo.

Amesema kuwa mkoa huo unatarajia kupokea wanafunzi 55,771 kwa darasa la awali, huku 51,446 wa darasa la kwanza na 40,796 kidato cha kwanza.

Kwa darasa la kwanza, amesema mkoa huo umefikia asilimia 75.8 ya uandikishaji mpaka kufikia mapema Januari mwaka huu na kwamba wataendelea hadi Machi.

Amewataka walimu mkoani humo kuendelea kuwapokea wanafunzi hata kama hawana sare za shule kwa kuwa wanaweza kununua huku wakiendelea na masomo.

Baadhi ya wazazi mkoani humo wamesema kuwa kuna umuhimu wa serikali kuzifuatilia baadhi ya shule kwani ingawa kuna msemo unaosma elimu bure lakini michango imeendelea kuongezeka kila kukicha

"Michango bado ni changamoto ni vema Serikali ikafanya ufuatiliaji kwenye shule zake maana wazazi wanaumia ikilinganisha na hali ya uchumi wa sasa," amesema Sheila Mussa.

Kwa upande wake Hadija Omary amesema kuwa ni vema Serikali ikaainisha michango inayoruhusiwa wazazi kuchangia shuleni, ili kusaidia kuondoa kero hiyo kwani jambo hilo limeendelea kuwapa kero wengi.

Imeandikwa na Mussa Juma, Anania Kajuni, Sanjito Msafiri, Hawa Mathias na Saddam Sadick, Stella Ibengwe