Majaji watakiwa kutafuta suluhu migogoro ya wahamiaji

Rais wa mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano huo jijini Arusha leo.

Muktasari:

Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud amekitaka chama cha majaji wanaoshughulikia masuala ya wakimbizi na wahamiaji Afrika kutafakari na kutafuta suluhu ya migogoro inayochangia kuwepo kwa wahamiaji katika nchi za Afrika na kuondokana na changamoto hizo.

Arusha. Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud amekitaka chama cha majaji wanaoshughulikia masuala ya wakimbizi na wahamiaji Afrika kutafakari na kutafuta suluhu ya migogoro inayochangia kuwepo kwa wahamiaji katika nchi za Afrika na kuondokana na changamoto hizo.

Ameyasema hayo leo Novemba 16, 2022 jijini Arusha wakati akizungumza katika mkutano wa Kimataifa wa Chama cha Majaji wanaoshughulika na masuala ya wakimbizi na wahamiaji unaofanyika jijini Arusha.

Jaji Imani amesema kuwa, changamoto ya kuwepo kwa wahamiaji katika nchi za Afrika zimekuwa zikichangiwa na uwepo wa migogoro ya kisiasa pamoja na mabadiliko ya tabia nchi ambayo husababisha wananchi wengi kukimbia nchi zao kwenda nchi zingine kutafuta amani. 

Amesema kuwa kutokana na changamoto  hizo ni lazima nchi za Afrika zijitafakari na kutafuta suluhu ya changamoto  hizo ambazo zinachangia  wahamiaji hao kutoka nchi moja  kwenda nchi nyingine  ili waweze kutulia  katika nchi zao. 

"Kupitia mkutano huu  tukae chini tuangalie vyanzo hivyo vinavyosababisha kuwepo kwa wahamiaji hao na tuweka mikakati ni namna gani ya kuondokana na changamoto  hizo na tuwaangalie ndugu zetu hawa kwa jicho la huruma na haki za binadamu kwani wanavyofanya hivyo hawafanyi makusudi bali  ni mazingira ndo yanachangia wao kufanya hivyo"amesema Jaji Imani.

Aidha amefafanua kuwa, ni  vizuri wakajadili kwa pamoja kuangalia migogoro  ya kisiasa inaathiri vipi  nchi za  Afrika na kuja na mikakati ya kukabiliana na migogoro  hiyo huku kwa upande wa mabadiliko ya tabia ya nchi wakiangalia namna ya kujipanga  mapema  katika kukabiliana na maswala ya njaa na ukame kwa wananchi .

Kwa upande wake Rais wa chama cha majaji wanaoshughulikia masuala ya wakimbizi  na wahamiaji  Afrika (IARMJ),Jaji  Isaac Lenaola amesema kuwa,lengo la mkutano huo ni kupanua uelewa wa masuala ya wakimbizi kwa maafisa wa serikali, majaji, mahakimu na watoa maamuzi wengine barani Afrika kupitia ufafanuzi wa kina kuhusu sheria ya wakimbizi na namna bora ya kuwahudumia pamoja na kutambua kwa kina umuhimu wa hifadhi ya wakimbizi na namna bora ya kuboresha mazingira. 

Jaji Lenaola amesema kuwa, kupitia mkutano huo majaji hao watazungumzia  kuhusiana na haki za wahamiaji ,na kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili na kuwafanya kukimbia  nchi zao  ikiwemo maswala ya mabadiliko  ya tabia ya nchi.

Ameongeza kuwa ,kupitia mkutano huo wataongeza ujuzi na ufanisi katika maswala ya wakimbizi na wahamiaji ndani ya Tanzania na barani Afrika kwa ujumla pamoja na kuwa na uratibu wa pamoja kuhusu namna bora za kushughulikia changamoto  maswala ya wakimbizi ndani na nje ya ukanda wa Afrika Mashariki.