Majaliwa aonya wanaoanzisha migogoro mipakani

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua eneo ambalo malori yameegeshwa kufuatia mgogoro wa madereva kudai kuongezewa stahiki zao na kuegesha malori hayo katika mpaka wa Tunduma.
Muktasari:
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa iliyopo mipakani watekeleze maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya ufuatiliaji wa watu waliounda vikundi visivyo rasmi vinavyosababisha migogoro katika sekta ya usafirishaji.
Songwe. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa iliyopo mipakani watekeleze maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya ufuatiliaji wa watu waliounda vikundi visivyo rasmi vinavyosababisha migogoro katika sekta ya usafirishaji.
Majaliwa amesema hayo leo Jumatano Julai 27, 2022 alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua mwenendo na shughuli za usafirishaji katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma katika wilaya ya Momba Mkoani Songwe.
"Serikali haitomvumilia mtu yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo vilivyo kinyume na sheria na taratibu za nchi" amesema Majaliwa.
Ameonya watu au vikundi vinavyojiingiza katika kufanya vitendo viovu na migogoro, kuwa wajiepushe na mgogoro hiyo.
Amesema iwapo kuna changamoto yoyote katika sekta ya usafiri inayowahusisha madereva na waajiri wao wasisite kuziwasilisha Serikalini.
“Kama zipo shida njooni sisi tutawapokea na kuwasikiliza ili kutatua shida zenu, malori yanayotoka na kuingia nchini yaachwe, tusijihusishe na migogoro ambayo inatatulika.”
Waziri Mkuu huyo amewapongeza madereva kwa kuamua kuisikiliza Serikali na kurejea kwenye shughuli za usafirishaji kama awali.
Amesema hivi sasa Taifa linakua kiuchumi katika sekta nyingi ikiwemo sekta ya usafirishaji, hivyo kuzuia wengine kufanya kazi ya usafirishaji ni uhujumu uchumi, kwani magari hayo yanaletea fedha na yanahudumiwa na wananchi wengi ambao kwa kufanya hivyo wanajipatia fedha na kuendesha maisha yao
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba amesema licha ya kuwepo mgomo huo lakini mkoa upo shwari na wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Amesema mkoa umeendelea vizuri ambapo katika kipindi cha mwaka jana ulifanya vizuri katika ukusanyaji mapato kwa kukusanya asilimia 116, huku mapato ya ndani pia halmashauri zilifanya vizuri ikiongozwa na halmashauri ya Tunduma ambayo ilikusanya zaidi ya Sh 8 bilioni na kuvuka lengo la kukusanya Sh5 bilioni.
Huu si mgomo wa kwanza kutokea unaowahusu madereva migomo kadhaa imetokea tangu mwanzoni mwa mwaka 2000 na mgomo wa mwisho ulifanyika mwezi machi mwaka huu ambapo madai ya madereva yamekuwa ni yaleyale ya kutaka kuongezewa mishahara, posho za safari na nyongeza ya posho ya kukaa zaidi ya siku 20 dereva akiwa nje ya nchi.