Majaliwa ataka bandari zimudu ushindani

Muktasari:
- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema lengo la Serikali kufanya upanuzi wa bandari ya Tanga ni kuiwezesha kumudu ushindani na bandari za nchi jirani.
Tanga. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa bandari ya Tanga ili iweze kumudu uhudumiaji wa sehena kubwa kwa haraka.
Amesema hayo leo Julai Mosi alipotembelea bandari ya Tanga kushuhudia maendeleo ya mradi wa uchimbaji kina na upanuzi wa gati ambao utagharimu Sh429.2 bilioni.
Amesema lengo la Serikali ni kuiwezesha bandari ya Tanga na bandari nyingine kuhudumia shehena nyingi kwa wakati mmoja na kuwawezesha wateja kuendesha biashara kwa wakati.
"Waelezeni wananchi kwamba Serikali imetoa fedha nyingi za upanuzi wa bandari ya Tanga ili iweze kupakua na kupakia shehena nyingib kwa muda mfupi zaidi ili kumudu ushindani na bandari za nchi jirani na kuwavutia wateja wengi zaidi," amesema Majaliwa.
Akitoa taarifa ya upanuzi wa bandari hiyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Juma Kajavala amesema awamu ya kwanza ilikuwa ya uchimbaji wa kina kutoka mita tatu hadi kufikia mita 13.
Ametaja pia awamu nyingine iliyokuwa ya upanuzi wa gati hadi kufikia mita 450 ndani ya maji na hivyo kuiwezesha bandari hiyo kupokea na kuhifadhi shehena nyingi kwa wakati mmoja.
Amesema Serikali imeahidi kutoa fedha nyingine kwa ajili ya upanuzi wa gati nyingine ya mita 250 itaksyokuwa na uwezo wa kuhudumia meli tatu za abiria zenye urefu wa mita 209 kila moja.