Majaliwa ataka shule ibadilishwe kuwa ya wasichana

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassimu Majaliwa ameendelea na mapumziko mafupi nyumbani kwake, Ruangwa mkoani Lindi ambapo ametembelea shule ya sekondari ya Liuguru iliyopo wilayani Ruangwa na kuahidi kutimiza ndoto yake ya kuibadili kutoka kuwa ya kutwa hadi ya bweni kwa wanafunzi wa kike.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameeleza ndoto yake ya muda mrefu ya kuibadilisha Shule ya Sekondari Liuguru kuwa shule ya bweni kwa wasichana pekee ili kuongeza idadi ya wanawake wasomi.

Majaliwa aliyasema hayo jana Jumatatu Julai 29, 2019 wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Liuguru, kata ya Narungombe, wilayani Ruangwa mkoani Lindi mara baada ya kukagua shule hiyo. Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa mapumziko mafupi.

“Ndoto yangu ni kuona shule hii inakuwa ya wasichana peke yao. Na tukifanikiwa, tutatengeneza akina mama wasomi, wanaojitambua, wenye maadili mema na wachapakazi,” alisema Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa (CCM).

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa leo Jumanne Julia 30,2019 imesema Majaliwa amechagua shule za Mnacho na Liuguru ziwe ni za bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike tu kama njia ya kuwaongezea fursa za masomo katika wilaya hiyo.

“Leo nimekuja kuwaeleza ndoto yangu. Tunahitaji kuona kila mtoto anayeenda shule, anakuwa na uhakika wa kumaliza masomo yake ya elimu ya juu. Wilaya hii tuna shida ya idadi kubwa ya mimba kwa watoto wa kike na mimi hili jambo linanikera sana,” alisema.

“Tulikubaliana tuwe na kaulimbiu yetu kwamba ‘Ruangwa kwa maendeleo inawezekana’ lakini kwenye elimu tumekwama kuleta maendeleo kwa sababu dada zetu hawamalizi shule na sisi ndiyo wasababishaji. Tumeweka sheria ya kuwafunga watu wanaowapa mimba wanafunzi, lakini bado haisaidii.”

“Njia pekee ya kuondokana na tatizo hili ni kufanya shule hizi ziwe za bweni ili wakae hapa shuleni, wafundishwe bila kupoteza muda wa kwenda nyumbani au kukutana na vikwazo wawapo njiani kuja shule au kurejea nyumbani,” alisema.

Alisema kwa kuanzia zitatuma Sh100 milioni ili zitumike kujenga nyumba nne za walimu, kisha atatafuta fedha nyingine ajili ya ujenzi wa mabweni, bwalo la chakula, jiko na mahitaji mengine kadri fedha zitakavyopatikana.

Awali, akiwasilisha taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Samuel Diwani alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007, hivi sasa ina walimu 11 ambapo watatu kati yao wanafundisha masomo ya sayansi na wanane waliobakia wanafundisha masomo ya lugha na sanaa.

Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 109 ambapo 51 kati yao ni wavulana na 59 ni wasichana, inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa nyumba tisa za walimu, ukosefu wa maabara mbili na iliyopo moja haijakamilika kwa asilimia 100.

 Mwalimu huyo alibainisha changamoto nyingine ni ukosefu wa mabweni, maabara ya kompyuta, mfumo wa umemejua, maktaba, jengo la utawala na stoo.