Majaliwa atoa mwezi mmoja madini ya Tanzanite kuanza kuuzwa Mirerani

Majaliwa atoa mwezi mmoja madini ya Tanzanite kuanza kuuzwa Mirerani

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amempa mwezi mmoja katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila  kuhakiki kanuni zinabadilishwa ili ununuzi wa madini ya Tanzanite ufanyike katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Mirerani. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amempa mwezi mmoja katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila  kuhakiki kanuni zinabadilishwa ili ununuzi wa madini ya Tanzanite ufanyike katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Jumatano Julai 7, 2021 wakati akizindua kituo cha Tanzanite Magufuli na kumtaka Profesa Msanjila kuhakikisha hadi Agosti 10, 2021  utaratibu wa kununua madini ya Tanzanite kupitia soko la madini Mirerani uanze.

"Tunataka madini ya Tanzanite yanunuliwe Mirerani kisha kama ni kusafirishwa kwenda nje ya nchi utaratibu ufanyike kutoka Mirerani baada ya kuongezwa thamani," amesema Majaliwa.

Amesema Serikali imefanya kazi kubwa  kujenga ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite hivyo inapaswa kuuzwa hapo Mirerani yanapochimbwa madini hayo.

"Tukishaungana kwenye hili tutafanikiwa na umasikini utatoweka kwani hata Rais Samia Suluhu Hassan amesema kila mtu anufaike kupitia rasilimali yao hivyo wana Mirerani wanufaike na Tanzanite," amesema Majaliwa.