Majaliwa atoa neno kwa wizara ushiriki wa hafla

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza kwenye kongamano la Kurasa 365 za Samia lenye lengo la kutangaza mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani lililofanyika leo kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Muktasari:

  • Serikali kuunga mkono na kuyafanyia kazi maoni ya wananchi yaliyotolewa katika kampeni ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Dar e Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka wizara kushiriki hafla zinazoandaliwa kuhusu utendaji kazi wa Serikali.

Amesema tangu kuanza kampeni ya Kurasa 365 za mama, ushiriki wa wizara umekuwa hafifu kwa mujibu wa wahusika. Kampeni hiyo imeandaliwa na Clouds Media ikitoa fursa kwa wizara kuelezea mafanikio ya Serikali.

Amesema kwa mujibu wa taarifa alizopewa mwaka jana 2023 zilishiriki wizara mbili na mwaka huu zimefikia saba.

Majaliwa amesema wizara zinapoelekea kwenye bajeti itabidi zitenge kiasi kidogo cha fedha, ili kusiwe na ugumu wa uandaaji wa kampeni za mafanikio ya miaka minne hadi miaka mitano ya Serikali.

Amezitaka wizara kushiriki katika hafla zinazoandaliwa kwa sababu zinafuatiliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, zikihusisha utendaji wa Serikali ya awamu ya sita.

Majaliwa amesema hayo leo Jumatano Machi 27, 2024 wakati wa kongamano la Kurasa 365 za mama lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema anatambua yapo mashirika mengine ya habari ambayo yameshiriki kampeni ya miaka mitatu ya utendaji wa Serikali ya awamu ya sita kwa kuwahoji watu ili kupata maoni yao.

“Hii yote ilikuwa ni kuungana na Clouds Media ili kuwafikia Watanzania wote kwa ajili ya kuchukua maoni yao, na sisi kama Serikali tumeyasikia na kuyachukua kwa ajili ya kuyafanyia kazi kwa kipindi kilichobaki,” amesema Majaliwa.

Amesema wataunga mkono na kuyafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na wananchi katika kampeni ya miaka mitatu ya Rais Samia, akiwataka viongozi wa Serikali kutumia fursa zinazopatikana kwenye hafla mbalimbali.

“Watanzania wote kumuunga mkono Rais Samia kwa ajili ya kumuhamasisha kubuni mambo mengine ili anapotoa maelekezo kwa watendaji wake tuweze kutekeleza kikamilifu,” amesema.

Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali kufanya kazi kwa kuzingatia falsafa ya Rais, na kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, haki za binadamu, uadilifu, uaminifu na uwajibikaji wenye matokeo chanya.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kazi ya vyombo vya habari ni kubwa, ambayo imesababisha watumishi wa Serikali kuwajibika.

“Tunashukuru vyombo vyote vya habari nchini katika kuadhimisha miaka mitatu ya Rais Samia, lakini katika kufanikiwa hili kuna uwajibikaji umetokea. Pia wamemtendea haki kwa kujadili kwa kina na wamehakikisha wananchi wanasema na Serikali yao,” amesema Nape.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema kumekuwa na ongezeko la uuzwaji wa nyama na samaki nje ya nchi ambalo limetokana na ushirikiano mzuri wa Rais Samia.

Amesema awali ilikuwa vigumu kukuta nyama ya Tanzania kwenye soko la nje.

“Miaka ya nyuma ukienda nje ya nchi ukaingia kwenye maduka huwezi kukuta nyama ya Tanzania inauzwa lakini leo hii ukienda Dubai utakuta nyama yenye bendera ya Tanzania,” amesema.