Majaliwa atoa siku saba kuchunguza chanzo cha moto K’koo

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa timu hiyo pia itatoa ushauri wa kitaalamu.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameunda Kamati maalumu kwa ajili ya kuchunguza ajali ya moto iliyotokea jana usiku kwenye Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Pia, ametoa agizo kwa benki na taasisi za fedha kuangalia namna ya kuwaongezea muda wa kurejesha mikopo wafanyabiashara walioathirika na ajali hiyo ya moto.

Kamati hiyo imepewa siku saba kukamilisha uchunguzi wake kuhusu chanzo cha moto huo ambao, umeteketeza sehemu kubwa ya soko hilo pamoja na mali za wafanyabiashara.

Moto huo ulioanza jana Julai 10,2021 saa 2:30 usiku ukianza sehemu ya juu ya jengo kisha kusambaa maeneo mengine ya soko hilo.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye amefika eneo la tukio leo Jumapili Julai 11,2021 kujionea uharibifu uliotokea kisha akazungumza na wafanyabiashara.

Amesema kamati hiyo itahusisha wajumbe kutoka Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi, Kitengo cha Maafa, Tamisemi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DPP).

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa kamati hiyo itahusisha pia wajumbe kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Kamati hii itaihusisha Takukuru kuchunguza wale viongozi waliotenguliwa baada ya ziara ya Rais (Samia Suluhu Hassan) huenda wakawa chanzo, lakini hatusemi wanahusika moja kwa moja,” amesema Majaliwa.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla aliyetembelea eneo la tukio juzi usiku, aliunda kamati kuchunguza tukio hilo ambayo itafanya kazi sambamba na iliyoundwa na Majaliwa.

Hata hivyo, Kamati ya Makalla imepangwa kufanya kazi hiyo kwa siku 10.  

Kuhusu wafanyabiashara walionguliwa mali zao, Waziri Mkuu ameyaagiza mabenki na taasisi za fedha kuangalia uwezekano wa kusogeza mbele muda wa urejeshaji wa mikopo ili kuwapa fursa ya kujipanga upya.

Pia, ameagiza sehemu za biashara na maduka kwenye soko kutoruhusiwa kuanza shughuli hadi hapo watakaporuhusiwa.